HEADER AD

HEADER AD

MVUA YA EL NIÑO YAANZA MKOANI MARA NYUMBA 30, DARAJA MOJA VYAHARIBIWA


>> RC Mara awataka wananchi kuchukua tahadhari 

Na  Jovina Massano Musoma

MVUA ya El Niño yaanza mkoani Mara na kusababisha nyumba 30 na daraja moja kubomolewa katika Kata ya Kabasa na Mcharo wilayani Bunda mkoani Mara.

Hayo yamesemwa Oktoba 23, 2026 na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Evans Mtambi wakati akizungumza na viongozi wa dini mbalimbali katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya mkuu wa mkoa Manispaa ya Musoma.

       Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Evans Mtambi wakati akizungumza na viongozi wa dini mbalimbali katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya mkuu wa mkoa Manispaa ya Musoma.

Brigedia Mtambi amesema Oktoba 22, 2026 majira ya jioni mvua zilinyesha wilayani Bunda na kubomoa nyumba 30 na daraja moja.

Mkuu huyo wa mkoa amewaasa wananchi  kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua hizo huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwakumbusha waumini wao kuendelea kuchukua tahadhali. 

Ameongeza kusema kuwa , kufuatia uwepo wa mvua hizo watoto waliokuwa wamekwenda kuchunga mifugo wamenusurika baada ya wazazi kuona hali sio nzuri na kuamua kuchukua maamuzi ya kuwafuata shuleni na kwamba wakati wanarudi walikuta eneo wanalohitaji kuvuka maji ni mengi na endapo wasingekuwa na mtu mzima huenda wangepata madhara. 

Amewasisitiza viongozi hao wa dini kuendelea kuwakumbusha waumini  kuchukua tahadhari katika kipindi hiki na kuwakumbusha wazazi na walezi kutowaacha watoto peke yao mara baada ya kuona dalili za uwepo wa mvua.

        Viongozi wa Dini wakiwa katika kikao cha mkuu wa mkoa Mara

RC Mtambi amesema tayari  mamlaka husika imekwishachukua hatua kwa kujenga daraja hilo na huduma za usafiri zinaendelea katika eneo hilo.

"Katika kuhakikisha athari zinapungua katika mkoa serikali inafanya mchakato wa kujenga Bwawa kubwa katika eneo la Borega lililopo wilayani Tarime ikiwa ni sehemu ya kuzuia mafuriko wakati mto huo unapokuwa umefurika".

Ujengaji wa Bwawa hilo ni mradi wa kiitifaki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo tayari nchi ya Kenya imekwishatekeleza ujenzi huo utakaokwenda kuimarisha shughuli za Umwagiliaji katika maeneo yanayozunguka mto huo na utasaidia kuondoa madhara ya mafuriko katika maeneo ya pembezoni.

Masuala mbalimbali yamejadiliwa katika kikao hicho yakiwemo maendeleo na maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika huduma za kijamii. 

>>Mvua za El Niño ni mvua zinazohusishwa na hali ya hewa iitwayo El Niño, ambayo hutokea pale joto la maji katika sehemu ya kati na mashariki ya Bahari ya Pasifiki linapoongezeka kuliko kawaida.

Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko ya mvua katika maeneo mbalimbali duniani na kusababisha kuwepo mvua nyingi kuliko kawaida, mafuriko yanayoweza kuharibu nyumba, barabara na mashamba.

Pia Mazao kuathirika kutokana na maji mengi, ingawa baadhi ya maeneo yanaweza kunufaika na mvua hizo.
Ni Mvua zisizotabirika, kwa sababu athari zake hutofautiana kulingana na eneo na msimu.

           Wadau wa masuala mbalimbali ya kijamii wakiwa katika kikao cha mkuu wa mkoa wa Mara.

Wakati huohuo , Mtambi amewaomba viongozi  hao kutumia nyumba za Ibada kukemea mambo yanayochafua mkoa vikiwemo vitendo vya ukeketaji na ukatili katika jamii kwa kuwa wanamchango mkubwa wa kuleta mabadiliko kupitia huduma wanazozitoa.

"Suala la maadili  ni la muhimu endeleeni kuijenga jamii yetu iwe na hofu ya Mungu,hivyo ushirikiano wa viongozi wa dini,mila na vyombo vya dola ni muhimu katika uhai wa Taifa".

Nao viongozi wa dini wameuomba uongozi wa mkoa kuwawezesha kufanya ziara kwenye wilaya ambazo zina matukio ya ukatili hasa ukeketaji kwa kuwajenga kiroho na kutoa elimu katika wilaya za Tarime,Butiama na Serengeti.

Mwananchi mkazi wa Musoma, Kudra Issa amesema suala la ukeketaji watashiriki kikamilifu kuhamasisha kwa kuwajenga waumini kiroho juu ya umuhimu wa kuacha ukeketaji kwa kuwa ni mojawapo ya ukatili.

       Mwananchi mkazi wa Musoma, Kudra Issa akizungumza.

Veronica Mayanzi mkazi wa Kitaji ambaye ni mjumbe wa kamati ya amani, amesema ni jukumu la kila mmoja kuwa mabalozi kwa jamii kwa kuwajenga  kimaadili kwa kuwa vitendo vingi vya ukatili vinatokea katika jamii.

  Veronica Mayanzi mkazi wa Kitaji ambaye ni mjumbe wa kamati ya amani.

Akihitimisha kikao hicho Brigedia Mtambi amewasihi viongozi hao kuchukua tahadhari na kuwahamasisha waumini wao dhidi uwepo wa ugonjwa wa Ebora katika mataifa ya jirani kwa kuwa mkoa huo upo mpakani na kuna hali ya mwingiliano wa watu kijamii na kiuchumi hivyo tahadhari ni muhimu.

No comments