HEADER AD

HEADER AD

RC PWANI ATOA MWEZI MMOJA MKANDARASI DIMETOCLASSA REAL HOPE LIMITED KUKAMILISHA MIRADI

Na Gustaphu Haule, Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo ametoa mwezi mmoja kwa Mkandarasi Dimetoclassa Real Hope Limited anayetekeleza miradi mitano ya TACTIC katika Manispaa ya Kibaha kuhakikisha ifikapo Novemba 22,2026 angalau awe amekabidhi mradi mmoja.

Nyongo ametoa kauli hiyo Oktoba 22/2026 wakati alipotembelea  na kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la Mnarani linalojengwa katika eneo la Loliondo Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha chini ya mkandarasi huyo.

   Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akiwa katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa soko la Kisasa la Mnarani Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeiamini kampuni hiyo na ndio maana ikaridhia kumpa nafasi ya kutekeleza miradi yote mitano ya Tactic kwahiyo anataka angalau Novemba 22 azindue japo mradi mmoja.

Nyongo amesema kuwa upande wa Serikali upo vizuri na utoa fedha kwa wakati na hakuna sababu ya kuchelewesha miradi huku akisema kama Serikali inapongezwa kwa kutoa fedha na wao wajitahidi kufanyakazi ili na wao wapongezwe pia.
        Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa soko la Mnarani Emmanuel Mahimbo akitoa taarifa ya ujenzi wa soko hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo aliyetembelea na kukagua mradi huo Oktoba 22/2026.

"Serikali imekupa miradi yote mitano ya Tactic kwakuwa imekuamini kwahiyo leo ni Oktoba 22/2026 nataka hadi ifikapo Novemba 22/2026 nikabidhiwe angalau mradi mmoja na hapo ndipo tutaelewana vizuri,"amesema Nyongo.

Nyongo amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha anafanyakazi usiku na mchana na ikiwezekana aongeze idadi ya wafanyakazi kutoka eneo la karibu na mradi huo ili waweze kumsaidia kufanyakazi kwa haraka zaidi.

      Mkuu wa Mkoa wa Pwani na viongozi mbalimbali wakitembelea mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Mnarani Oktoba 22/2026.

"Chukua mafundi wengine na vijana wa Mtaani ili waweze kukusaidia kazi ambazo zipo chini ya uwezo wao maana Serikali inataka kuona kazi inafanyika kwakuwa makusudio ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma sahihi katika mazingira mazuri,"amesema Nyongo.

Meneja miradi wa kampuni ya ujenzi ya Dimetoclassa Real Hope Limited mhandisi Shaban Kaswaka amesema amepokea maelezo ya Mkuu wa Mkoa na wanakwenda kuyafanyia kazi ili kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi hiyo.

          Meneja Miradi wa kampuni ya ujenzi ya Dimetoclassa Real Hope Limited Mhandisi Shaban Kaswaka (kushoto) akimuongoza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kutembelea na kukagua ujenzi wa soko la Mnarani -Loliondo Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha.

Kaswaka amemtoa wasiwasi Mkuu huyo wa Mkoa kwa kusema ifikapo Novemba 22/2026 atakuwa tayari amekamilisha mradi mmoja kama alivyoagiza na kwamba inawezekana pia kwa tarehe hiyo miradi mingine itakuwa imefikia hatua kubwa.

"Mheshimiwa Mkuu wa mkoa nina uhakika ikifika Novemba 22/2026 nitakuwa tayari kukukabidhi mradi mmoja kama ambavyo umetuagiza na hata miradi mingine itakamilika kwa wakati kwakuwa tayari tumetengeneza mazingira yakufanyakazi hata wakati wa mvua,"amesema Kaswaka.

Amesema kwa mujibu wa mkataba mkandarasi anatakiwa kukabidhi kazi Ifikapo Februari 2027 na kwamba kwa kasi ya ujenzi inayofanyika sasa anaimani miradi yote mitano itakwenda kukamilika kwa wakati.

Hata hivyo, miradi ya Tactic inayotekelezwa katika Manispaa ya Kibaha ni pamoja na ujenzi wa Soko la kisasa Mnarani, ujenzi wa eneo la burudani, ujenzi wa kiwango cha lami katika barabara ya Tughe- Anglican - Tumbi, ujenzi wa barabara ya Picha ya Ndege - Lulanzi na ujenzi wa ofisi ya utawala kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ambapo inagharimu zaidi ya Sh. Blioni 19.

        Shughuli za ujenzi wa soko la Mnarani Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha zikiwa zinaendelea .

No comments