HEADER AD

HEADER AD

ALIYEKUWA MKURUGENZI MANISPAA YA KIBAHA AMKABIDHI OFISI WARDA MAULID


Na Gustaphu Haule, Pwani

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amekabidhi ofisi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Warda Maulid ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kuteua wakurugenzi wa Halmashauri.

Makabidhiano hayo yamefanyika  Oktoba 02, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa  na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa idara za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, viongozi wa chama, viongozi wa dini na wa taasisi zilizopo ndani ya Halmashauri  hiyo.

         Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ( kushoto) akikabidhi  vitendea kazi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda Maulid (kulia) katika hafla iliyofanyika Oktoba 02,2026 .

Akizungumza wakati akikabidhi ofisi hiyo, Dkt.Shemwelekwa amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kumuamini katika kipindi chote alichohudumu kama Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha hadi kuwa Manispaa.

Amesema, aliweza kuboresha Manispaa ya Kibaha kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuweza kujenga miradi ya kimkakati kupitia mapato ya ndani na tayari kuna miradi imekamilika na kuna mingine inaendelea na ujenzi.

 "Hadi kufikia tarehe 30 Septemba tayari tumeshafikia asilimia 50, ya ukusanyaji wa mapato na huwa ikifika Mwezi Desemba tunakuwa tumefika asilimia 100 na miezi iliyobaki ni kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo tunaenda kujenga miradi ya kimakati na kuwasogezea huduma karibu wananchi," amesema

Dkt. Shemwelekwa amelishukuru baraza la madiwani kwa ushirikiano alioupata kutoka kwao katika kipindi chote, viongozi wa chama cha mapinduzi na wakuu wa taasisi mbalimbali ambapo waliweza kushirikiana kwa moyo mmoja.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda Maulid amesema, anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa majukumu mapya ndani ya Manispaa ya Kibaha.

       Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ( kulia) akimtakia heri Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda Maulid mara baada ya kufanyika kwa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi.

Amesema, amekuja Kibaha kuendeleza pale ambapo Mkurugenzi aliyepita ameyafanya, na ameahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu mapya aliyopewa na Mhe. Rais.

Amesema, anaomba ushirikiano kutoka kwa wakuu wa Idara , ofisi ya Mkuu wa Wilaya, viongozi wa dini na viongozi wa Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha Kibaha inasongambele zaidi kimaendeleo.

Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma amempongeza Dkt. Rogers Shemwelekwa kwa mazuri yote aliyoyafanya ndani ya Manispaa ya Kibaha huku akimtakia majukumu mema huko aendako.

        Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma (Kulia) akimkabidhi tuzo ya heshima aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika hafla ya Makabidhiano ya ofisi iliyofanyika Oktoba 02,2026.

Amesema, Dkt Shemwelekwa ameweza kuwa na ushirikiano mzuri na Baraza la madiwani na wakuu wa idara jambo ambalo liliweza kufanikisha yale mazuri yote yaliyofanyika kwa kipindi kifupi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwajuma  Nyamka amesema anampongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais kwahiyo wanamkaribisha na watampa ushirikiano katika kila hatua.

Amesema, wanaamini watapata ushirikiano wa kutosha kwa Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa ilani  kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa mpya.

      Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda Maulid na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha hafla ya Makabidhiano ya ofisi na wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka.


No comments