HEADER AD

HEADER AD

NYARAKA ZA SIRI ZA POLISI ZAVUJA, MTU WA NDANI AHUSISHWA


PRETORIA, AFRIKA KUSINI 

TUME ya Uchunguzi ya Madlanga nchini Afrika Kusini imesikiliza ushahidi kwamba Oupa “Bafana” Sindane  ambaye ni mfanyabiashara na tajiri wa sekta ya teksi nchini Afrika Kusini alikuwa na nyaraka za siri za Jeshi la Polisi la Afrika Kusini (SAPS), hali iliyozua uwezekano kwamba mtu kutoka ndani ya jeshi hilo alikuwa akimpatia taarifa za siri.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mbele ya tume, Sindane alikuwa na nyaraka mbalimbali za ndani za SAPS, zikiwemo ripoti za matukio ya ufyatuaji risasi yaliyohusisha polisi, taarifa kuhusu uchunguzi wa mauaji ya askari wa polisi pamoja na mawasiliano yaliyodaiwa kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Polisi, General Fannie Masemola.

Tume ilisikia pia kuhusu ripoti ya ndani iliyohusiana na uchunguzi wa mauaji ya Sergeant Marcus Lekalakala.

Kwa mujibu wa wakili wa ushahidi wa tume, Matthew Chaskalson, aina ya nyaraka zilizokuwa mikononi mwa Sindane iliibua swali kuhusu namna alivyopata taarifa hizo ambazo zilipaswa kuwa za siri.

Ushahidi huo haujathibitisha bado ni nani aliyekuwa akimpatia Sindane nyaraka hizo.

Ujumbe, nyaraka za Siri zachunguzwa

Tume pia imekuwa ikichunguza ujumbe wa WhatsApp na nyaraka zinazohusishwa na Sindane kama sehemu ya ushahidi unaohusu mahusiano yake na watu mbalimbali pamoja na upatikanaji wa taarifa za polisi.

Miongoni mwa taarifa zilizotajwa ni ripoti ya ndani ya SAPS kuhusu operesheni iliyohusisha kundi linalojulikana kama “Kwagga 20”.

Taarifa hizo zimekuwa sehemu ya ushahidi mpana unaochunguzwa na tume kuhusu madai ya uhalifu uliopangwa, rushwa na kuingiliwa kwa mifumo ya haki jinai nchini Afrika Kusini.

Swali la nani alivujisha taarifa ?

Ushahidi huo umeibua swali muhimu kuhusu iwapo kulikuwa na mtu ndani ya SAPS aliyekuwa akimpelekea Sindane taarifa hizo za siri na sababu iliyokuwa nyuma ya utoaji wa taarifa hizo.

Hata hivyo, tume bado haijatoa hitimisho la mwisho kuhusu suala hilo. Watu wanaohusishwa na madai hayo wanapaswa kuchukuliwa kuwa hawajapatikana na hatia hadi ushahidi utakapothibitishwa na mchakato wa kisheria kukamilika.

Ushahidi kusikilizwa faragha

Wakati huohuo, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi wa Uhalifu cha SAPS, Major-General Feroz Khan, anatarajiwa kutoa ushahidi mbele ya Tume ya Madlanga.

Tume imeamua kwamba sehemu ya ushahidi wake isikilizwe kwa faragha ili kulinda watoa taarifa wa polisi, utambulisho unaohusishwa na uchunguzi wa uhalifu uliopangwa na uchunguzi mwingine unaoendelea.

Kwa mujibu wa SABC News, ushahidi wa Khan uliopangwa kusikilizwa kwa faragha unatarajiwa kuanza Jumanne, Oktoba 6, 2026.

Khan pia amekuwa akikabiliwa na hatua za kisheria baada ya kutofika mbele ya tume licha ya kuitwa kwa amri rasmi ya subpoena. Mwenyekiti wa tume, Jaji Mbuyiseli Madlanga, aliamuru hatua za kufunguliwa mashtaka ya jinai zichukuliwe kutokana na kutofika kwake.

Tume ya Madlanga inaendelea kuchunguza madai mbalimbali yanayohusu uhalifu, rushwa na kuingiliwa kwa mifumo ya haki jinai nchini Afrika Kusini.

Chanzo: NovaNews na SABC News, Afrika Kusini.

No comments