HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI KAGERA YAZINDUA KAMPENI YA PIKA SMART YA KUZUIA MATUMIZI YA MKAA, KUNI

Na Alodia Babara , Bukoba

SERIKALI imezindua kampeni ya kitaifa ya Pika Smart mkoani Kagera, ikilenga kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Kampeni hiyo inasisitiza matumizi ya umeme kama nishati safi ya kupikia, hatua inayotarajiwa kupunguza athari za kiafya, gharama za nishati na uharibifu wa mazingira.

       Wananchi manispaa ya Bukoba wakipata elimu jinsi ya kutumia jiko la umeme.

Kampeni hiyo imezinduliwa juzi katika Manispaa ya Bukoba na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abeli Nyamahanga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya kampeni hiyo inayotekelezwa katika mikoa saba nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Nyamahanga amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuboresha afya za wananchi, kuimarisha uchumi wa kaya, kulinda mazingira na kuokoa muda unaotumika katika shughuli za nyumbani.

      Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abeli Nyamahanga akiwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya Pika Smart.

Amesema matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakichangia athari za kiafya zinazotokana na moshi, hasa kwa wanawake na watoto, huku matumizi ya umeme yakitarajiwa kusaidia kupunguza changamoto hizo pamoja na kupunguza ukataji wa miti.

Kutokana na umuhimu wa kampeni hiyo, Dkt. Nyamahanga amewaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine mkoani humo kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya umeme wa kupikia inawafikia wananchi hadi ngazi ya vitongoji ili kuongeza uelewa na kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati.


     Mkuu wa wilaya ya Muleba Abel Nyamuhanga akikabidhi jiko la umeme kwa mwananchi.

"Katika kukabiliana na changamoto ya gharama za awali za ununuzi wa majiko ya umeme, serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeweka utaratibu wa On-Bill Financing, unaowawezesha wananchi kupata majiko hayo na kulipia gharama zake kwa awamu kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU.

Meneja wa shirika la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Stephen Mwembe ameeleza kuwa, shirika hili kupitia on-bill financing mteja anaweza kuchukua jiko la umeme ma kuanza kulilipia kidogokidogo kupitia luku hadi deni litakapokamilika.

"Tunawakaribisha wananchi wa Kagera kufika katika ofisi zetu kupata maelekezo jinsi ya kujiunga na mpango huu" amesema Mhandisi Mwembe .

Balozi wa kampeni ya Pika Smart, Mrisho Mpoto, amesema umeme wa kupikia haupaswi kuonekana kama anasa au kitu cha ziada katika kaya, bali ni fursa muhimu ya kuboresha maisha ya wananchi. 

      Msanii Mrisho Mpoto akihamasisha wananchi kutumia nishati ya umeme  katika kupika.

Amesema,matumizi ya umeme katika kupikia yanaweza kusaidia familia kuokoa muda, kupunguza gharama za matumizi ya nishati na kurahisisha shughuli za kila siku majumbani.

"Matumizi ya umeme wa kupikia yana mchango mkubwa katika kulinda afya za wananchi, hususan kwa kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, nahamasisha wananchi kutumia nishati safi kwani ni  hatua muhimu katika kujenga mazingira bora ya maisha na kupunguza changamoto za kiafya zinazohusiana na uchafuzi wa hewa majumbani" amesema Mpoto

Ametoa wito kwa wananchi kuachana na dhana kwamba umeme wa kupikia ni gharama kubwa au unapatikana kwa watu wenye kipato cha juu. Amesisitiza umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu faida zake na matumizi sahihi na kuwa kampeni ya Pika Smart .

Amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia na kuwahamasisha kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha maisha yao, kulinda afya na kuchangia utunzaji wa mazingira.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba wameipokea kampeni hiyo kwa mtazamo chanya, huku wakiiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya umeme wa kupikia ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuelewa umuhimu na manufaa ya nishati hiyo.

Alinda Byabusha mkazi wa manispaa ya Bukoba ameeleza kuwa, iwapo kampeini hii itafanyika kwa vitendo wananchi watafurahia uwepo wa nishati ya umeme na wataona manufaa yake.

No comments