TIMU YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA YATINGA KATA YA UBENA NA BWILINGU KUTOA ELIMU
Na Gustaphu Haule, Chalinze
TIMU ya wataalamu inayotekeleza kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia( Mama Samia Legal Aid Campain) imewafikia wananchi wa Kata ya Ubena na Bwilingu kwa kuwapa elimu mbalimbali sambamba na kutatua migogoro ya ardhi.
Utekelezaji wa kampeni hiyo katika Halmashauri ya Chalinze ilianza Oktoba 29/2026 ikiongozwa na Wakili wa Serikali ambaye ndio Mratibu wa timu hiyo Marwa Mohere.
Katika kampeni hiyo timu hiyo ilikutana na wananchi wa Kata ya Bwilingu na Kata ya Ubena ambapo kwa Kata Bwilingu Wakili Mohere alitoa elimu kuhusu namna ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, hatua za kupata haki pamoja na masuala ya utatuzi wa migogoro ya ndoa.
Kwa upande wa Kata ya Ubena timu hiyo ilitoe elimu ya ndoa kwa wajumbe wa baraza la usuluhishi, elimu kuhusu migogoro ya ardhi na elimu kuhusu masuala ya ukatili wa Kijinsia kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Ubena Ranch na shule ya Msingi Mgogodo.
Wanafunzi hao wamepewa elimu kuhusu ukatili wa Kijinsia na kujua madhara yake, kujua maeneo ya ukatili, makundi ya ukatili na njia mbalimbali za kutoa taarifa pale ambapo wanafanyiwa ukatili au kunapokuwa na viashiria vya ukatili.
SGT Saida Hamisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Chalinze amewaeleza wanafunzi wa shule ya Ubena Ranch kuhakikisha wanatoa taarifa za haraka pale ambapo wanafanyiwa ukatili.
SGT Saida Hamisi kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Chalinze akitoa elimu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia kwa wananchi wa Kata ya Ubena ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Amesema hata kama wanaona kuna ishara za matukio ya vitendo vya unyanyasaji wa Kijinsia na ukatili basi ni vyema wakawa wapesi wa kutoa taarifa mapema ili kuweza kuzuia mapema na hivyo kuepusha athari za vitendo vya ukatili.
Katika hatua nyingine SGT Saida amewataka akina mama na akina baba kuacha kukimbilia polisi pale ambapo kunatokea migogoro ya ndoa ikiwemo kunyimana unyumba na badala yake waanze kushughulikia migogoro hiyo katika ngazi za jamii.
Wakili wa Serikali na Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Marwa Mohere akitoa elimu kwa mabaraza ya usuluhishi Chalinze ikiwa ni utekelezaji wa Kampeni hiyo iliyoanza Oktoba 29/2026 katika Halmashauri ya Chalinze.
Amesema zipo ngazi za jamii na familia ambazo zinaweza kutatua migogoro hiyo huku akisema kwa upande wa dini ya kiislamu kuna utaratibu wake na upande wa dini kikristo kuna utaratibu wake kwahiyo ni vyema wakapitia hatua hizo kabla ya kufika dawati la jinsia.
Amesema kuwa mambo mengine yanaweza kumalizwa katika ngazi ya kijamii bila hata kufika Polisi na kama wakiona wamepita katika ngazi za kijamii na imeshindikana ndipo wachukue maamuzi ya kwenda ngazi ya juu ya dawati la jinsia.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Chalinze Atuganile Chisunga akitoa elimu ya kuhusu masuala ndoa kwa wananchi wa Kata ya Ubena ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya mama Samia.
Hata hivyo, SGT Saida amesema Wanaume wengi wamekuwa wakipigwa na Wake zao lakini wanaogopa kutoa taarifa ambapo amewataka wanaume hao kuhakikisha wanatoa taarifa mapema ili waweze kusaidiwa.
Amesema wanaume wanapigwa lakini wanaona aibu kusema kwa madai ya kuogopa kudharaulika jambo ambalo sio sawa ambapo amesema dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kutenda haki kwa watu wote.
Mjumbe wa baraza la Usuluhishi Chalinze akichangia mada katika mkutano wa Kampeni ya msaada wa Kisheria wa Mama Samia ulioanza kutekelezwa kwa awamu ya pili Mkoa wa Pwani Oktoba 29/2026.
"Akina baba wengi huwa mnapigwa na Wake zenu huko majumbani kwenu lakini hamsemi wala hamtoi taarifa kwasababu ya kuogopa aibu na kudharaulika kwahiyo niwaombe kuanzia leo toeni taarifa na dawati la Jinsia litawasaidia,"amesema SGT Saida.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia inafanyika kwa awamu ya pili Mkoani Pwani ambapo utekelezaji wake umeanza Oktoba 29/2026 na itamalizika Novemba 07/2026.
Wakili Asela Tesha (katikati) na mratibu wa Kampeni ya msaada wa Kisheria ya mama Samia Marwa Mohere (kushoto) wakitoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo iliyoanza Oktoba 29/2026.






Post a Comment