WAZIRI ULEGA AWATAKA WAKUU WA WILAYA , HALMASHAURI KUWAHAMASIHA WANANCHI WAJITOKEZE KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA

Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega amewataka Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi mbalimbali wa Halmashauri kuhakikisha wanakwenda kuwahamasisha wananchi ili waweze kujitokeza na kushiriki katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) itaanza Oktoba 29/2026 na itamalizika Novemba 10/2026 ikiwa ni muda wa siku 10 ikiwa na kauli mbiu ya msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na Maendeleo.
Ulega ametoa wito huo Oktoba 28/2026 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali katika ufunguzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia( Mama Samia Legal Aid Campaign) uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Kibaha Mailimoja.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika Kibaha Mailioja Oktoba 28/2026.
Ulega, amesema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ni daraja na mkombozi kwa wananchi wanyonge hivyo ni vyema kila Mwananchi akapata fursa ya kuhakikisha anawasilisha malalamiko au mgogoro wake ili uweze kutatuliwa.
Ulega amesema kuwa wapo wananchi wamekuwa na malalamiko pamoja na migogoro lakini huwa wanashindwa kujua wapi pa kuanzia lakini kupitia kampeni hiyo ni lazima wananchi wahamasishwe kikamilifu ili kusudi kila mmoja aweze kunufaika na kampeni hiyo.
Amesema Mkoa wa Pwani ni awamu yake ya pili kufikiwa na kampeni hiyo kwani awamu ya kwanza walifikiwa watu 20,243 ambapo kati ya hao wanawake ni 1,1967 na watu 98,276 ni wanaume huku sensa ya mwaka 2022 inaonyesha Mkoa wa Pwani ina watu 2,24,947 ambapo ni sawa na asilimia 9 hadi 10.
Waziri wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega akitembelea mabanda ya msaada wa kisheria ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika katika viwanja vya stendi ya Mailimoja Oktoba 28/2026.
Ameongeza kuwa kutokana na hiyo Rais Samia akasisitiza na kuitaka Wizara ya Katiba na Sheria iendelee na kampeni ili kusudi ambao hawakufikiwa awamu ya kwanza basi waweze kufikiwa awamu ya pili.
Ulega amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuanzisha kampeni hiyo kwakua kwasasa imekuwa kampeni yenye kuwasaidia wanyonge kupata haki zao bila gharama yoyote.
Amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imekuja kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao ni wanyonge wasiokuwa na uwezo ndio maana imeamua kuwafuata hukohuko.
wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani wakishiriki uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika Kibaha Oktoba 28/2026.
Amesema serikali inatambua uchache wa mawakili wa kujitegemea katika ngazi ya Halmashauri kwakuwa wengi wao wapo Mijini hivyo Wizara inaweka mpango wa kuwaruhusu mawakili wa serikali kushughulika na kusimamia mashauri ya wananchi yasiyokuwa na mgongano wa kimaslahi na serikali.
Ulega amesema mpango huo utawawezesha mawakili wa serikali na wale wa kujitegemea kufanyakazi kwa karibu na kupanua wigo wa kisheria kwa wananchi wanyonge waishio Vijijini.
Amesema pia, Serikali imejenga mfumo wa kidigitali unaowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kupata mrejesho juu ya masuala yanayowakabili na kwamba kufanya hivyo ni kuwarahisishia wananchi kupata haki zao.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua Kampeni hiyo ya awamu ya pili na kwamba Mkoa wa Pwani umekuwa wa kwanza ikifuatiwa na Zanzibar.
Waziri wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega (katikati) Mwenye tai nyekundu akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kuzindua kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia awamu ya pili.
Nyongo amesema kuwa kampeni hiyo inasaidia kupinga unyonyaji wa haki, kutatua migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake na watoto na mambo ya ndoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Seif Shekilaghe amesema kuwa kampeni hiyo ilitokana na uhitaji mkubwa wa wananchi kutaka kufahamu haki wajibu wao na kupata haki zao.
Shekilaghe, amesema kuwa kampeni hiyo itakuwa endelevu kwa muda wa miaka minne hadi 2030 ambapo kauli mbiu yake ni Msaada wa Kisheria kwa haki, usawa, amani na Maendeleo.
Amesema kauli mbiu hiyo inatekeleza maono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa kupata haki kwasababu ya umaskini, umbali au kutokuwepo kwa huduma ya Kisheria katika maeneo yao.
Amesema kauli mbiu hiyo pia, inakwenda sambamba na kuweka misingi imara kwa dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ili kufikia malengo ni lazima kuwepo kwa jamii inayotawaliwa na misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na utawala wa sheria.




Post a Comment