POLISI CHALINZE YAWATAKA WANAFUNZI KUTOOGOPA KUTOA TAARIFA WANAPOFANYIWA VITENDO VYA UKATILI

Na Gustaphu Haule, Chalinze
ASKARI wa Jeshi la polisi kupitia dawati la Jinsia katika Wilaya ya KiPolisi Chalinze SGT Saida Hamisi amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mselele iliyopo katika Kijiji cha Mwetemo Kata ya Kiwangwa Halmashauri ya Chalinze kuacha kuogopa kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Ametoa kauli hiyo Novemba 03,2026 wakati akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) awamu ya pili.
SGT Saida Hamis kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Chalinze ( kulia) na Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay ( kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Mselele ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.Amesema wapo wanafunzi wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini wanaogopa kutoa taarifa kwasababu ya kutishiwa kupigwa kitendo ambacho kinapelekea kuathirika kisaikolojia na hivyo kupoteza molari ya kusoma.
Amewaambia wanafunzi hao kuwa hata kama mwalimu wao,mzazi wake na mtu yeyote anawafanyia vitendo vya ukatili wala wasiogope mtu na badala yake watoe taarifa mapema ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mhusika.
SGT Saida amesema Jeshi la Polisi kupitia dawati la Jinsia kazi yake ni kupambana na vitendo vya ukatili na kwamba katika dawati hilo wanafunzi wamepewa kipaumbele kwahiyo kwa jambo lolote lazima watoe taarifa bila kumficha mtuhumiwa.
SGT Saida Hamis akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mselele Kata ya Kiwangwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia alipofika shuleni hapo Novemba 03,2026.Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatambua madhira na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanafunzi ndio maana akaanzisha kampeni ya Msaada wa Kisheria ili kusudi wanafunzi wapate sehemu ya kueleza changamoto zao.
"Sisi tumefika hapa tukiwa tunatekeleza kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kama ambavyo mnaona jina lenyewe maana yake kampeni imeanzishwa na Rais Samia mwenyewe ili iwasaidie ninyi wanafunzi kwahiyo niwaombe toeni taarifa za ukatili ili wahusika wachukuliwe hatua,"amesema Saida.
Saida amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi katika elimu kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo kujenga madarasa katika Shule zenye upungufu wa madarasa lakini pia amejenga shule mpya katika kila Kata hapa nchini lengo ni kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma.
",Mmeona kazi ambayo amefanya Mheshimiwa Rais Samia amejenga na kuimarisha miundombinu ya shule nchi nzima lengo ni kuhakikisha mnasoma katika mazingira mazuri lakini akaona haitoshi ameamua kuleta kampeni ya Msaada wa kisheria kwahiyo niwaombe msome lakini msisite kutoa taarifa kwa yeyote anawafanyia vitendo vya uhalifu,"ameongeza Saida.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay amesema anachotaka kuona wanafunzi wanakuwa na maadili mema sambamba na kuzingatia masomo yao.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay akitekeleza majukumu yake ya kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Novemba 03,2026.Lukumay, amesema kwakuwa Rais Samia amewatengenezea mazingira mazuri ya kusomea basi wanachotakiwa ni kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuweza kutimiza ndoto zao za baadae na kwakufanya hivyo watakuwa wametimiza adhma ya Rais yakuinua sekta ya elimu nchini Tanzania.
Nae Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria wa Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze Ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere amewafundisha wanafunzi wa shule ya Msingi Masuguru kutambua haki zao.
Amewaeleza wanafunzi hao kuwa wanahaki ya kusoma, haki ya kupata chakula,haki ya malezi,haki ya kulindwa na haki ya mavazi lakini na wao lazima watambue kuwa wanawajibu wa kusoma kikamilifu.
Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia awamu ya pili ambaye ni wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Masuguru ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni hiyo Novemba 03,2026.Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili ilizinduliwa Oktoba 28,2026 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani na Waziri wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega na ilianza utekelezaji wake Oktoba 29,2026 na itakamilika Novemba 07,2026.
Wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia akiwemo SGT Saida Hamis kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Wilaya ya KiPolisi Chalinze na Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay wakitoka kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Mselele Kata ya Kiwangwa Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.




Post a Comment