WANANCHI WA KATA YA KIWANGWA WAPIGWA MSASA NA WATAALAMU KUTOKA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA
Na Gustaphu Haule, Chalinze
WATAALAMU wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia awamu ya pili( Mama Samia Legal Aid Campaign) wamepiga kambi ya siku moja katika Kata ya Kiwangwa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani na kufanikiwa kuwapiga msasa wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa.
Mbali na kuwapiga msasa wajumbe wa bodi hiyo lakini pia wataalamu hao, wamefanikiwa kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wanafunzi wa shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Sekondari Ridhiwani Kikwete,Shule ya Sekondari Mselele,Shule ya Msingi Masuguru, Shule ya Msingi Kiwangwa na Shule ya Msingi kwa Wema pamoja na kusikiliza na kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi.
Awali akizungumza wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa yaliyofanyika Novemba 03 ,2026 katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Kiwangwa, mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay amewataka wajumbe hao kuacha kuvunja ndoa hovyo.
Lukumay amesema kuwa baadhi ya wajumbe wa bodi za usuluhishi zimekuwa na tabia ya kukimbilia kuvunja ndoa za watu kwakuwa tu wanamaslahi binafsi na kwamba kufanya hivyo hakuleti afya.
Amesema kuwa kazi kubwa inayotakiwa kufanywa na wajumbe wa bodi ya usuluhishi ni kufanya usuluhishaji na endapo ikishindikana basi wanaweza kutoa fomu namba 3 ambayo itawapa nafasi ya kwenda ngazi za juu ikiwemo Mahakamani.
Amesema kitendo cha kuvunja ndoa za watu hovyo hovyo kunasababisha kuwepo na ongezeko la watoto wengi wa Mitaani ambao mwisho wa siku wanakosa malezi ya baba na mama na hivyo kupelekea watoto hao kukatisha ndoto zao za maisha ya baadae.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay akiwaelekeza wajumbe wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa namna ya kujaza fomu za usuluhishi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika Novemba 03,2026 katika ofisi ya Mtendaji Kata Kiwangwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
"Msiwe mnavunja ndoa hovyo hovyo lakini ni vyema mkasuluhisha,kwa mfano utakuta ndoa nyingine ni za vijana halafu wamezaa watoto watatu wakifika katika bodi ndoa inavunjika na mwisho wa siku watoto wanakosa malezi ya wazazi wao na hivyo kuwa watoto wa Mitaani,"amesema Lukumay.
Lukumay ameongeza kuwa wajibu wa Msingi wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa ni kudumisha amani na mshikamano katika Kata na kutatua migogoro kwa misingi ya amani ili kufikia haki.
Amesema kazi ya usuluhishi ni kusaidia wananchi kwahiyo wasifanyekazi ya usuluhishi wa migogoro kwa kuangalia maslahi ya mtu binafsi na kwamba mwenyekiti wa bodi anapaswa kumuondoa mjumbe mwenye tabia ya kuangalia maslahi huku akisema haki ya Mwananchi inaanzia katika baraza la Kata.
Wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika Kata ya Kiwangwa Halmashauri ya Chalinze wakijengewa uwezo na wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, mafunzo hayo yamefanyika Novemba 03,2026 katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Kiwangwa.
Amesema mabaraza ya Kata yapo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1985 na ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa mabaraza hayo ameona ni vyema kuyajengea uwezo mabaraza hayo ili yamsaidie kutatua changamoto na migogoro kwa wananchi.
Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere amewataka wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa kuhakikisha Mashehe wanaofungisha ndoa watambulike kwakuwa na leseni ya Serikali.
Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere akiwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa Kata ya Kiwangwa,mafunzo hayo yamefanyika Novemba 03,2026.
Mohere,amesema ni makosa makubwa endapo Shehe anafungisha ndoa bila kutambulika kwani mwisho wa siku kunapotokea na mfarakano wa baba na mama wakienda Mahakamani kudai haki vyeti vya ndoa walivyopewa havitatambulika kisheria.
Amesema ni vyema wakifunga ndoa kupitia Bakwata au Kikristo waende kusajili serikalini ili wapate cheti kinachotambulika na kwamba wanaohusika na kutoa vyeti hivyo ni Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo( RITA).
Mohere,amewaelekeza wajumbe wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa kuhakikisha wanasikiliza migogoro hiyo angalau wiki mbili kwani ipo migogoro inasikilizwa siku moja na kutolewa maamuzi siku hiyo hiyo jambo ambalo sio sawa .
Mwenyekiti wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa Kata ya Kiwangwa Idd Magira ,amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea mafunzo hayo kwakuwa wamepata mwanga wa namna ya kufanya usuluhishi katika migogoro ya ndoa.
Magira,amesema awali alikuwa hajui chochote kuhusu bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa lakini kwasasa amejifunza mengi na atakwenda kuyafanyiakazi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Kata ya Kiwangwa.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Kiwangwa Kwaga Malota, amemshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuanzisha kampeni ya Msaada wa Kisheria huku akiwataka wajumbe hao kwenda kutumia mafunzo hayo kutenda haki kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kiwangwa Kwaga Malota akifunga mafunzo kwa wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Kiwangwa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Novemba 03,2026.






Post a Comment