HEADER AD

HEADER AD

WAFANYABIASHARA STENDI YA CHALINZE, MADEREVA WA PIKIPIKI, WAJASIRIAMALI WAPATA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA


Na Gustaphu Haule, Chalinze 

WAFANYABIASHARA wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Chalinze,madereva wa pikipiki (Bodaboda),Mama lishe na wajasiriamali mbalimbali wamenufaika na elimu ya msaada wa kisheria inayotolewa na timu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia( Mama Samia Legal Aid Campaign).

Elimu hiyo imetolewa Novemba 01,2026 na  wataalamu hao wakiwemo wanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay, Prosper Maghaibuni, Asela Tesha,Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Moses Matiko, Afisa ustawi wa jamii wa Halmashauri hiyo Atuganile Chisunga,Afisa maendeleo ya Jamii Michael Mwakanjuki.

       Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Chalinze Michael Mwakanjuki akitoa elimu kwa wafanyabiashara wa stendi ya mabasi Chalinze ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia inayoendelea kufanyika Katika Halmashauri hiyo.

Miongoni mwa elimu waliyoitoa katka kampeni hiyo ni pamoja na elimu ya ukatili wa Kijinsia,elimu kuhusu Sheria za mikataba ya kazi kwa bodaboda,namna ya utatuzi wa migogoro ya ndoa,na migogoro ya ardhi.

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Chalinze Atuganile Chisunga amesema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria imekuja kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika kutatua changamoto na migogoro iliyopo katika maeneo yao.

        Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Chalinze Atuganile Chisunga akitoa elimu ya ukatili wa Kijinsia kwa wafanyabiashara wa stendi ya Chalinze ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada kisheria ya Mama Samia iliyofanyika Novemba 01,2026.

Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameanzisha programu ya msaada wa kisheria na kuunda timu mbalimbali na Chalinze ni miongoni mwa Halmashauri zilizofanikiwa kupata timu inayofanyakazi hiyo.

Chisunga ,amewaomba wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kutumia fursa hiyo kuhakikisha wanapeleka malalamiko yao na kwamba hata kama kuna mwanamke au Mwanaume ananyimwa haki ya ndoa timu hiyo ipo tayari kutatua mgogoro huo.

Mwenyekiti wa soko la Chalinze Athumani Maneno ,amepongeza hatua ya Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo muhimu.

       Moja ya sehemu ya kupumzikia wafanyabiashara katika eneo la stendi ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Maneno amesema kuwa wafanyabiashara wengi na baadhi ya Bodaboda hawana uelewa juu ya mikataba ya kibiashara lakini kwasasa wamepata uelewa ambao utasaidia kupunguza migogoro ya kibiashara.

Shaban Hamisi mfanyabiashara wa mahindi katika stendi ya mabasi Chalinze amesema kuwa awali hakujua namna ya kufuatilia haki zake pale ambapo migogoro inatokea lakini kwasasa amepata ufahamu wa kutosha ambao utakwenda kumsasidia .

Hata hivyo,Hamisi ameiomba Serikali kuhakikisha kampeni hiyo inakuwa endelevu ili kuhakikisha inazidi kuwasaidia wananchi katika kutatua migogoro katika maeneo yao.

        Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Moses Matiko akitoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa Kijinsia kwa wanafunzi wa shule mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyofanyika Novemba 01,2026 Kata ya Bwilingu.

        Wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia wakiwa katika stendi ya Chalinze katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa stendi hiyo Novemba 01,2026.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay akitoa elimu kwa wafanyabiashara wa stendi ya mabasi Chalinze ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyofanyika Novemba 01 katika Kata ya Bwilingu.

No comments