HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI KATA YA LUGOBA WAPATA MATUMAINI YA KUONDOKANA NA MIGOGORO YA ARDHI BAADA YA KUPATA ELIMU KUTOKA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA

Na Gustaphu Haule, Pwani

WANANCHI wa Kijijii cha Lugoba Kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamesema wameanza kupata matumaini ya kuondokana na migogoro ya ardhi kutokana na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuanzisha kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Kauli ya wananchi hao imekuja katika mkutano baina yao na wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili uliofanyika Novemba 05,2026 katika ofisi ya Kijiji cha Lugoba.

      Wananchi wa Kijiji cha Lugoba Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani wakiwa katika mkutano wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika Novemba 05,2026 katika ofisi ya Kijiji hicho.

Mmoja wa Wananchi hao Catherine Kimelemeta amesema kuwa wanaKijiji wengi wamekuwa wakidhurumiwa haki zao kutokana na umaskini pamoja na kukosa uelewa wa kisheria.

Amesema  kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbuana na mfugaji Folike Mtumia na wamejaribu kwenda katika hatua zote za kimamlaka lakini bado wamekosa nguvu kwakuwa Folike ana uwezo wa kifedha.

Amesema mgogoro huo unawajumuisha zaidi ya wanaKijiji 42 lakini kila yanapotoka maamuzi ushindi unakuwa upande wa Wananchi lakini pamoja na ushindi huo lakini bado mfugaji huyo amekuwa na nguvu na hivyo kushindwa kulima katika mashamba yao.

        Mwananchi wa Kijiji cha Lugoba Elizabeth Emily akieleza namna alivyodhurumiwa ardhi na jirani yake.

Catherine, amesema ujio wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia anaona kama wamepata mkombozi ambaye atasaidia wanaKijiji kupata haki zao ikiwemo kumalizika kwa mgogoro huo.

"Kwakweli angalau sasa nimeanza kupata matumaini ya mgogoro wetu kumalizika maana tumeletewa wataalamu bure na wamechukua mgogoro wetu kwa ajili ya kwenda kushughulikia ," amesema Kimelemeta.

Kimelemeta amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo muhimu na kuwapeleka wataalamu wa kisheria ambao wanafanyakazi ya kuwasaidia wananchi kutatua migogoro yao.

Ally Mbweto Mkazi wa Kijiji cha Lugoba amesema kuwa anawaamini wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwa watafanya jitihada za kutatua migogoro ya ardhi.

      Mwananchi wa Kijiji cha Lugoba Ally Mbweto akieleza namna mgogoro kati ya Folike Mtumia na wakulima wa Kijiji hicho unavyosumbua.

Amesema wananchi wa Kijiji cha Lugoba wakati mwingine wakienda shambani kulima huwa wanapigwa na kutishiwa kukatwa mapanga na wao wanaogopa kwenda katika mashamba yao kwakuwa jamii ya wafugaji wamekuwa wakitumia silaha kali.

"Tunaomba wataalamu wetu mliofika hapa mtusaidie maana huku Lugoba tunateseka na migogoro ya ardhi na watu ambao wanatutesa ni hawa wafugaji ambao wanashirikiana na baadhi ya wenyeji kuporwa ardhi za Wanakijiji,"amesema Mbweto.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni amewatoa wasiwasi wananchi wa Kijiji cha Lugoba kuwa migogoro ya ardhi iliyochukuliwa katika mkutano huo inakwenda kupata ufumbuzi .

        Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Asela Tesha akitoa msaada wa kisheria kwa Mwananchi wa Kijiji cha Lugoba Mwashabani Kharid Novemba 05/2026 katika ofisi ya Kijiji cha Lugoba.

Maghaibuni amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi lakini chanzo ni kukosa wasimamizi wa mirathi lakini pia hata huyo msimamizi wa mirathi anapoteuliwa  aendi kuthibitishwa Mahakamani na inapotokea migogoro ya ardhi wakienda Mahakamani msimamizi wa mirathi anakuwa hatambuliki.

Amewahimiza wananchi wa Kijiji cha Lugoba kuhakikisha wanamteua msimamizi wa mirathi ili aweze kusimamia ardhi zao kwani bila hivyo wakienda Mahakamani wanarudishwa waanzie upya au kupoteza haki zao.

      Wataalamu wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya mama Samia akiwemo mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Prosper Maghaibuni na SGT Saida Hamis kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Chalinze wakitoa msaada wa kisheria kwa Mwananchi wa Lugoba katika eneo la ofisi ya Kijiji hicho Novemba 05/2026.

Afisa ardhi wa Halmashauri ya Chalinze Baltazar Miti ametoa wito kwa wanaKijiji na wananchi wengine wanaotaka kununua ardhi kuwa wafuate utaratibu.

Hata hivyo,Miti amesema kuwa wanatakiwa kujiridhisha katika mamlaka ya Serikali ya Kijiji na ikiwezekana wawatafute majirani ambao wanajua historia ya eneo husika na ndipo waweze kununua viwanja au mashamba.


No comments