HEADER AD

HEADER AD

CHAMA CHA WANASHERIA CHAWAFUNDA WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE


Na Dinna Maningo,Dodoma

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetoa mafunzo kwa baadhi ya Waandishi wa Habari Wanawake nchini namna ya kuandika habari za utetezi wa Sera na Sheria zinazozingatia mahitaji ya haki, kuandika habari za ukiukwaji wa Sera na Sheria,Utawala wa Kidemocrasia pamoja na kutoa elimu juu ya haki za wananchi kikatiba na kisheria.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Rafiki Hoteli Jijini Dodoma ambapo mwezeshaji wa mafunzo hayo Wakili Mery Mwita ambaye pia ni Mwandishi wa Habari aliwasisitiza waandishi wa habari kuandika habari hizo ili kusaidia wananchi kupata haki zao kwa mujibu wa Sera,Sheria na Katiba.



"Sisi Waandishi wa Habari ndio wakuleta Mapinduzi ya kutetea wananchi, tuibue habari kujua je yaliyopo kwenye Sera, Sheria na Katiba yetu ya nchi yanazingatiwa na kutekelezwa? je mikataba inayofanyika imezingatia sheria, miongozo na Katiba?waandishi wa habari wana mchango mkubwa katika kuhakikisha Sera na Sheria zinatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo.

"Baadhi ya Sheria zinazotungwa ni zile za kuminya Uhuru wa Habari, Taasisi za Kidemocrasia zimekuwa zikitunga Sheria za kuwabana Waandishi wa Habari, waandishi tuwasaidie wananchi kujua haki zao, matatizo mengi yanayohusu haki za wananchi yanazidi kwakuwa hawajui wapi  pakuanzia" Wakili Mery Mwita.

"Vyombo vya Habari kupitia Waandishi wa Habari Mahiri na wenye maadili ya uandishi wa habari vina uwezo mkubwa wa kufanya ushawishi na kusababisha Serikali kupitia Bunge likatunga sheria ambazo zinahitajika kwa maendeleo ya nchi ambazo zimebainika hazijatungwa."



"Vyombo  vya habari kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali wana uwezo wa kupinga sheria na sera kandamizi hatimaye kuwezesha kutungwa kwa sheria." alisema Wakili Mery Mwita.

Afisa ufuatiliaji na tathmini Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Selemani Pingoni alisema kuwa mafunzo hayo ya uandishi wa habari za utetezi wa sera na sheria kwa Waandishi wa Habari Wanawake yamefanyika kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza na lengo la mradi ni kusaidia kupeleka elimu kwa wananchi juu ya sheria na haki na kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari Wanawake wanapokuwa wanaandika habari zao warejee kwenye Sera,Sheria na Katiba.



RAIS wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)Deogratius Nsokolo amewahimiza Waandishi wa Habari Wanawake waliopata mafunzo ya uandishi wa habari za Utetezi wa Sera na Sheria zinazozingatia mahitaji ya haki yaliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kuyatumia vyema mafunzo hayo kuandika habari ili wananchi waweze kufahamu haki zao Kisera,kisheria na Kikatiba na kwamba baada ya mafunzo hayo UTPC itafuatilia kuona kile kilichofanyika katika uandishi wa habari hizo.

No comments