Home
/
MAJI
/
MAKALA
/
BOMBA LA MAJI LIMEPITA MTAA WA BUJINGWA, KILABELA LAKINI WANANCHI HAWAJANUFAIKA NA MRADI
BOMBA LA MAJI LIMEPITA MTAA WA BUJINGWA, KILABELA LAKINI WANANCHI HAWAJANUFAIKA NA MRADI
•Waamka usiku kutafuta maji
•Wanafunzi wafikisha kilio kwa Aweso
•Wachangia maji na mifugo
Na Dinna Maningo, Mwanza
NI majira ya saa mbili asubuhi nawasili stendi ya magari iliyopo makutano ya Barabara ya Rwagasore na Kenyatta, magari yaendayo Igombe kata ya Bugogwa iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza, dakika chache tunainza safari, tunatumia dakika 56 hadi kufika stendi yanakoishia magari ya Igombe mwendo wa Takribani Km 16.
Nashuka kutoka ndani ya gari na kusogea kituo cha maegesho ya pikipiki, namuomba mwendesha pikipiki anipeleke mtaa wa Bujingwa kata ya Bugogwa, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kufika kwenye mtaa huo, tunaianza safari na kufika Bujingwa mwendo wa Takribani km 1.5 toka stendi.
Nikiwa simfahamu mtu yeyote katika mtaa huo ndipo namuuliza mwananchi mmoja anioneshe ilipo ofisi ya Mwenyekiti wa mtaa, bila hiyana ananionesha ofisi, kwa bahati nzuri namkuta Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa Shaban Nkungu najitambulisha kwa majina na kazi yangu nakumweleza sababu ya kufika kwenye mtaa huo.
Tukiwa tumeketi, punde si punde wanafika na viongozi wengine wa Chama cha CCM tunatambulishana, kwakweli watu wa Bujingwa ni wakarimu kwa wageni licha ya kuonana kwa mara ya kwanza lakini wananipa ushirikiano huku nyuso zao zikiwa na furaha.
Sababu ya kufika kwenye mtaa huo ni kufahamu hali ya huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa mtaa wa Bujingwa kama inaendana na Sera ya Maji ya Taifa ya mwaka 2002 ambayo imetokana na mapitio ya Sera ya mwaka 1991.
Sera ya maji inaeleza kuwa maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai,maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.Kiwango cha maendeleo ya maji yoyote kinategemea kuwepo kwa maji ya kutosha yenye ubora unaotakiwa.
Je hali ya upatikanaji wa maji ikoje kwenye mtaa wa Bujingwa?. Wananchi na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa wanasema kuwa mtaa huo unakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama kwakuwa hakuna maji ya bomba ambayo ni safi na salama.
Wananchi wa mtaa huo licha ya bomba kubwa la maji kupita kwenye ardhi yao lakini hawajanufaika na maji ya bomba na badala yake wamekuwa wakiendelea kutumia maji ya sio safi na salama ya visima na madimbwi vinavyomilikiwa na wananchi ambavyo wanachangia na wanyama wa kufugwa wakiwemo ng'ombe, Mbuzi, mbwa, kondoo na wanyama wa porini kama fisi, wadudu, watambaao na ndege.
Viongozi wa CCM Tawi wafunguka kuhusu bomba la maji
Shaban Nkungu ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa anasema kuwa suala la uhitaji wa maji ya bomba kwenye mtaa ni la muda mrefu na wamekuwa wakifuatilia kwenye mamlaka zinazohusika na huduma ya maji lakini hupewa ahadi ya kuvutiwa maji isiyotekelezeka.
"Bomba la maji limetoka pale mtaa wa Kabangaja ambako kuna tenki la maji limepita hapa kwenye ardhi yetu lakini hatuna maji limekwenda hadi mtaa wa Igogwe km 3 ambako kuna tenki, wao wana maji ila sisi tumerukwa mradi umepita kwetu lakini hatunufaiki nao.
"Tunatumia maji ya kwenye visima vya asili na madimbwi tunachangia na wanyama kama Fisi, Mbwa,Tumbili,Ng'ombe,Mbuzi na Kondoo,tunatumia maji machafu, maji yameishia mtaa jirani wa Kigote, hatuna hata kituo kimoja cha maji ya Bomba hata cha kutuzubaishazubaisha Serikali imetutenga"anasema Shabani.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Bujingwa Yurita Lutema anasema kuwa changamoto ya maji inawasumbua viongozi na kusababisha wananchi wawadharau na kuonekana waongo, wasiofuatilia kuhakikisha mtaa unapata maji ya bomba ya kutoka ziwa Victoria ambalo lipo umbali wa Km1.5
"Tatizo la maji hapa kwenye mtaa wetu limeshakuwa ni la kudumu limetusumbua sana sisi viongozi wa Chama na mtaa imepelekea tudharauliwe tunaonekana waongo na tusiofuatilia, wenzetu wa mtaa jirani walipopata maji tulipoenda kuchota walikuwa wanatuambia kuwa sisi haturuhusiwi kuchota maji, wananchi wetu wanaambiwa si mkawaambie viongozi wenu wawaletee maji,manyanyaso yakatushinda tukaacha kuchota.
"Wananchi wetu nao wakadharauliwa wakawa wanaambiwa mbona viongozi wenu hawawasemei ndio maana hampati maji, sasa hivi visima vingi vimekauka kutokana na kiangazi tunafuata maji ziwani, kufua kuoga wengine wanaenda kwenye visima kusubiria maji yavuje, wanapanga foleni na wakati mwingine wanakosa maji, kama una pesa unanunua maji kwa wenye toroli kwa sh.2000-3000 dumu sita"anasema Yurita.
Katibu wa CCM Tawi la Bujingwa Robert Bukindu anasema kuwa yeye ni mkulima wa mbogamboga analazimika kuamka saa tisa usiku yeye na mke wake kwenda kutafuta maji kisimani na kuwaacha watoto wakiwa wamelala wenyewe.
"Tatizo likitokea tunalalamikiwa wazazi kuwa tumewaacha watoto wenyewe ndani, huwezi kumwacha mwanamke usiku saa tisa aende mwenyewe kutafuta maji, serikali ndio tatizo hawataki kutuletea maji, kuna siku tulienda kutafuta maji usiku tuliporudi tukakuta siafu wameingia ndani, unaondoka unaacha familia yenyewe ndani ni hatari, matukio ya wizi yanatokea wakati wanapojua mmeenda kutafuta maji watu wanaibiwa kuku na mali zingine.
"Maji tunayotumia sio safi na salama kwa afya zetu ni machafu watoto wana matumbo makubwa kutokana na maji wanayotumia wanakuwa na minyoo, watu wanalalamika kuumwa tumbo, na watu wa huku hawana desturi ya kuchemsha maji ya kunywa"anasema Robert.
Anaongeza"Watu wamenunua viwanja wameshindwa kujenga kwakuwa wanaogopa gharama za kununua maji, tungekuwa na maji serikali ingepata mapato, mtaa unakosa maendeleo kwa sababu ya ukosefu wa maji"anasema Katibu.
Suzana Toryo mwenye umri wa miaka 59 mkazi wa mtaa huo anasema kuwa wakati wa mvua hakuna changamoto ya maji kwakuwa visima vinakuwa na maji ya kutosha japo ni maji yasio safi na salama lakini inapofika msimu wa kiangazi ni karaha kwao kwakuwa wanatumia muda mwingi kuhangaikia maji na unaweza ukawahi usiku kwenda kutafuta maji lakini usiyapate na ukibahatisha ni ndoo moja au mbili.
"Unaamka usiku saa kumi unatembea km moja kutafuta maji ukibahatisha ni ndoo moja au mbili na una familia ya Watoto wengi hayohayo upikie ufulie nguo na shughuli zingine inakulazimu urundike nguo mpaka utakapopata maji, baadhi ya nguo inabidi usizivae hasa nyeupe maana zinabagua maji"anasema Suzana.
Anaongeza kuwa wakati wa kampeni wagombea hujinadi kutatua changamoto hiyo ya maji lakini wakishapata uongozi hawaoni mabadiliko yoyote " ikifika kweye kampeni wanavyojinadi unasema ngoja tumpe akipata uongozi hana habari tena, bomba limepita hapahapa kweye ardhi yetu tunalikanyaga lakini tukavukwa wakaenda kupeleka maji mitaa mingine tunaomba Serikali ituletee maji ili tusiugue magonjwa ya kuhara" anasema.
Muhangwa Malambu anasema kuwa maji ya kununua hayatoshelezi mahitaji ya familia kutokana na ukubwa wa baadhi ya familia ambazo kwa siku zinatumia maji ndoo 10 na kila ndoo moja ya maji ni sh 300 wengine hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua maji.
"Sisi wanaume hasa huku kwetu mazingira ni ya kijijini japo ni mtaa tunazaa watoto wengi na tuna wake zaidi ya mmoja mpaka uwe na maji ya kutosha zaidi ya ndoo kumi, utatoa wapi pesa za kununua tu maji inabidi wake zetu wakatafute maji kwenye visima vya asili ndoo sh.100 au kwenye madimbwi na maji ni ya shida wanawake wanapigania maji hadi wanaumizana.
"Watu wa maji walishafika mtaani kufanya tathmini wakatuambia tukate miti ili wapitishe mabomba ya maji, tukakata miti na mazao yetu lakini baada ya bomba kupita hatujawahi kuletewa maji wakapeleka huko mbele" anasema.
Anaongeza " tukiuliza majibu tunayoambiwa nikwamba bomba hili ni kubwa hatuwezi kusambaziwa maji eti mpaka yatoke Igogwe ndio yarudi tena huku kwetu ambako ndio bomba limepita, tupo karibu na ziwa lakini maji ya ziwani sio safi na salama na sisi tunataka tutumie maji safi na salama ya bomba ambayo yanawekewa dawa "anasema Muhangwa.
Ghati Nyamhanga anasema tatizo la maji linaleta ugomvi kwa wanandoa kwakuwa uamka alfajiri kwenda kutafuta maji huyasotea kwa saa zaidi ya tano wakisubiri maji na wanapochelewa kurudi nyumbani waume wao uhisi kuwa huwenda wanawasaliti na kusingizia foleni kubwa ya maji.
"Unaamka saa kumi na moja alfajiri unaenda kisimani unakuta foleni ni kubwa unasubiri inafika hadi saa nne asubuhi hujapata maji unarudi nyumbani mme hakuelewi anahisi ulienda kuchepuka na mwanaume mwingine maana hauna maji" anasema.
Ghati anaongeza kuwa ukosefu wa maji ni mateso kwa wajawazito kwakuwa nao huamka usiku kwenda kutafuta maji huku wazazi waliojifungua wakihaha kwa kukosa maji yakufulia vitambaa vya Watoto, vichanga nao wakiogeshwa maji yasiyo safi na salama na hivyo kukumbwa na maradhi.
"Wajawazito wanahangaika sana wanawahi saa tisa usiku kwenda kupanga foleni isiyo na uhakika wa kupata majina, pia mzazi aliyejifungua anachota maji machafu anafulia madaso na kumuogeshea mtoto mchanga ndani ya siku mbili mtoto anaanza kuharisha.
"Una mfunika mtoto nguo iliyofuliwa na maji machafu, hayo maji tunayochota watoto wanakunywa, huku kwetu wananchi hawachemshi maji utatoa wapi pesa ya kununua kuni za kuchemsha maji kila mara wakati unashinda ukizunguka kutafuta maji na una familia ya watu wengi.
Ili kujiridhisha na kauli za wananchi hao kuhusu utumiaji wa maji yasio safi na salama, Mwandishi nikauchapa mwendo kuvitembelea visima kujionea uhalisia wa maji hayo na changamoto ya uhaba wa maji.
Baadhi ya visima vilikuwa havina maji yamekauka kutokana na kiangazi, visima vingine vikiwa vimefungwa kwa kufuli ili kupisha maji yavuje , wenye visima nao wakipanga masharti ya muda wa kuchota maji kwa siku mara moja huku Kisima cha mtaa ambacho ni chakupampu wananchi wakichota maji mara moja kwa siku muda wa asubuhi pekee na visima vingine wananchi wanalazimika kushinda kisimani kusubiri maji yatoke ili wachote na vingine wananchi wakichangia na wanyama huku vinyesi vya wanyama vikiwa karibu na vyanzo vya maji.
Visima vingine vikiwa vimezungushiwa fensi aina ya mabingobingo ili kuzuia wanyama wasinywe maji huku wanyama nao wakipata changamoto ya maji kwakuwa maji ni haba mifugo hukosa maji ya kunywa kwakuwa dimbwi ambalo ni la maji kwa ajili ya mifugo wananchi nao wanachota maji hayo hayo kwenda kutumia majumbani, wananchi wengine wanalazimika kupeleka wanyama ziwani kwenda kunywa maji na wengine wakifuata maji ziwani kuwauzia wananchi.
Nazungumza na baadhi ya wanawake na watoto ambao ni wanafunzi niliowakuta wakiwa wamekaa pembezoni mwa kisima wakisubiri maji yavuje ili wachote nao wanaeleza changamoto zao.
Elizabeth Emanuel anasema kuwa ule msemo wa kumtua ndoo mama kichwani bado haujawafikia wanawake wa Bujingwa kwakuwa wanateseka kuamka saa tisa usiku kutafuta maji ambayo wanayatumia na wanyama.
Debora Musa anasema kuwa wanapokwenda kutafuta maji njiani hukutana na fisi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha yao" haya maji unayoyaona ni juhudi zetu wananchi tumechimba visima,maji ni ya shida tunamaliza siku tatu hatuogi, hatufui nguo tunarundika ndani, Bibi vizee na mababu wanahangaika kupata maji jamani serikali ituonee huruma na sisi ni wapiga kura"anasema Debora.
Japheti Revocatus ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Kilabela anasema kuwa ukosefu wa maji unarudisha nyuma taaluma ya wanafunzi kwakuwa muda mwingi wanashinda kisimani kusubiri maji, hali hiyo inasababisha wachelewe shule na kukosa baadhi ya vipindi na wengine kuwa watoro.
"Wanafunzi tunaamka saa tisa kuwasaidia wazazi wetu kutafuta maji shuleni tunakwenda tukiwa tumechelewa tunakosa vipindi jambo hili linarudisha nyuma taaluma ya wanafunzi tunafeli masomo, tunamuomba Waziri Jumaa Aweso atusaidie tupate maji tunateseka sana wazazi wahangaike kututafutia pesa ili kujikimu maisha bado wahangaike kutafuta maji wanashindwa kufanya kazi kutafuta pesa wanaenda kusotea maji Aweso tusaidie ili sisi wanafunzi tupate muda wa kusoma"anasema Japheti.
Sera ya Maji ya Taifa ya 2002 inaeleza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi, utumiaji wa maji ambayo sio salama na uhaba wa maji huchangia katika kusababisha milipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu.
Msingi wa Sera unasisitiza kuwa maji ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu, matumizi ya maji kwa ajili ya binadamu ni muhimu kwanza, maeneo yenye uhaba wa maji yanatakiwa kupewa kipaumbele cha miradi, maji ni bidhaa ya kiuchumi, maji yanatakiwa kulindwa na kuhifadhi vyanzo vya maji na maji ni huduma endelevu.
Kwa mujibu wa Sera hiyo ya maji jukumu la Serikali za mtaa ni kuhakikisha wanachi wanapata huduma ya maji safi na salama hivyo ni wasimamizi na wawezeshaji wa jamii, Serikali za mtaa zina jukumu la kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa maji, kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa na kufanyiwa matengenezo.
Je uongozi wa Serikali ya mtaa wa Bujingwa unasimamia vipi utekelezaji wa Sera ya maji?
Ndalawa Habari (Shija) ni Mwenyekiti wa mtaa wa Bujingwa anasema kuwa mtaa una kaya 216, anasema katika kuhakikisha wananchi wanapata maji mtaa una visima vya maji vilivyochimbwa na wananchi pamoja na cha mtaa kisima Cha kupampu ambavyo msimu wa kiangazi hukauka, na wamekuwa wakijitahidi kutunza miundombinu ya maji.
"Tulihamasisha wananchi tukachimba visima, vingine ni vya asili tunavilinda na vinafanyiwa usafi, kisima cha kupampu kiliharibika tukachukua fedha kweye mfuko wa mtaa sh. laki tatu kikafanyiwa ukarabati na watu wa RUWASA kwa kwakati huo walitutengenezea bomba lililokuwa limeharibika.
"Tatizo wakati wa kiangazi maji ni ya shida visima vingi ni vya asili na vilivyochimbwa na wananchi vimekauka na kusababisha watu wachote kwenye madimbwi ambayo yana maji machafu wanyama wanakunywa hayo maji,na vichache vilivyopo maji ni ya kugombania na si safi na salama " anasema Ndalawa.
Je Serikali ya Mtaa imefuatilia vipi kuhakikisha inatatua changamoto ya maji? Mwenyekiti huyo anasema kuwa wameshafuatilia mara kadhaa ofisi za MWAUWASA mkoani Mwanza lakini wamekuwa wakipewa ahadi zisizo tekelezeka.
"Kuna mradi wa maji wa Igombe lakini Baadhi ya mitaa haijafikiwa na maji, mtaa wangu Bomba kubwa la maji limepita likitokea mtaa wa Kabangaja kuliko na tenki la maji likapita hapa mtaani limeenda hadi kwenye tenki la Igogwe km 3 kutoka hapa mtaani na kupeleka maji Nyamwilolelwa kata ya Shibula.
"Kama ni ufuatiliaji nimefuatilia sana hata ule mradi wa maji wa Igombe niliambiwa kuwa ili tupate maji mpaka yatoke Igogwe ndio yarudi kwetu Diwani, Mbunge walishalifuatilia hadi tulishawahi kukaa vikao na wataalamu tukapewa muda wa mwezi mmoja kuwa shughuli ya kusambaza maji zitaanza.
"Baada ya mwezi mmoja walikuja kufanya savei wakaondoka ilikuwa 2021 mwezi wa sita, baadae alikuja mkuu wa wilaya kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Igogwe tulikaa kikao na wenyeviti wote na wataalamu wakasema bajeti ya maji haipo hivyo wanasubiri bajeti ya mwaka huu pesa ikiingia tutaletewa maji " anasema.
Ndalawa anasema kuwa ukosefu wa maji umesababisha kesi za ndoa zitokanazo na tatizo la maji, wanawake wanapokwenda kutafuta maji waume huamini wana mahusiano na wanaume wengine ndio maana wanachelewa kurudi nyumbani.
Diwani wa kata ya Bugogwa William Mashamba anasema kuwa tatizo hilo la maji ameshalizungumzia kwenye vikao mbalimbali vikiwemo vikao vya Baraza la Madiwani na kwamba mtaa huo umo kwenye bajeti utapata maji.
" Wataalamu walitumia ramani ya zamani ambapo wakati huo Bujingwa haikuwa mtaa ilikuwa ni kitongoji na ni eneo ambalo lilikuwa na wananchi wachache, ramani iliyotumika ni ya wakati ule Anthony Diallo akiwa mbunge wa jimbo la Mwanza Vijijiji 2005-2010 ni ya zamani tumeshazungumza kwenye vikao na maji yatakwenda naomba wavumilie changamoto hiyo itaisha " anasema William.
Tatizo la upatikanaji wa maji lipo pia mtaa wa Kilabela kata ya Bugogwa ambako bomba la maji limepita lakini wananchi hawana maji na uongozi wa mtaa huo umesema kuwa umefuatilia bila mafanikio kama anavyoeleza John Jonathani Mwenyekiti wa mtaa wa Kilabela.
"Kata hii ina mitaa 15 mtaa wa Bujingwa na Kilabela ndipo limepita bomba kubwa la maji limeenda Masemele -Igogwe,mitaa ambayo haina maji ni Bujingwa, Kilabela, Isanzu, Igogwe na Kisundi,mtaa wangu una kaya 300 zenye watu Kati ya 1800-2000, maji tunachota kwenye visima vya asili vingi vimekauka unaamka usiku kutafuta maji na ni ya kubahatisha.
"Tukiuliza MWAUWASA wanasema maji mpaka yatoke kweye tenki la Igogwe ndio yarudi kuja huku Kilabela, tulishawafuata wakaja wakafanya savei lakini hadi sasa hatuna maji tunatumia maji yasio safi na salama tunaomba Serikali itusaidie sisi viongozi tunalaumiwa na wanachi kuwa hatufuatilii ndio maana mitaa yetu haina maji mitaa mingine ina maji "anasema John.
DIMA ONLINE imezungumza na Kaimu Meneja Mahusiano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Oscar Twakazi ili kufahamu ni lini wananchi wa mtaa wa Bujingwa na Kilabela iliyopitiwa na bomba la maji watapata huduma ya maji ya bomba?Je ina mpango gani wa kuviboresha visima vya asili ili wananchi wapate maji safi na salama ? nini mkakati wao kuhakikisha inatekeleza Sera ya Maji ya Taifa mtaa wa Bujingwa na Kilabela?.
Oscar anasema kuwa mamlaka ya maji inatambua wajibu wa kutekeleza sera ya maji ambayo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya maji na Sheria nyingine na kwamba Mamlaka inaendelea kuweka mipango ya kuboresha huduma katika maeneo hayo na mengine hatua kwa hatua kulingana na uwezo wa fedha utakaokuwepo kwakushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya maji.
Akizungumzia tatizo la maji mtaa wa Bujingwa amesema kuwa MWAUWASA imekabidhiwa miradi iliyosanifiwa na kujengwa na halmashauri mwaka 2013 ambayo kwa sasa inasimamiwa na mamlaka hiyo na kwamba kwa kipindi hicho maeneo mengine hayakuwa na makazi wakati wa utekelezaji wake hivyo kuchangia changamoto zilizopo kwa sasa.
"Katika utaratibu wa uendeshaji huwa mamlaka zinatangazwa na Waziri wa Maji kupitia gazeti la Serikali na inapotangazwa mamlaka huwa inawekewa mipaka ya kufanya kazi, mamlaka ya maji Mwanza ilikuwa inatoa huduma ya maji Mwanza mjini tu, miaka inavyozidi kwenda huwa kuna mabadiliko sheria zinabadilika au wanatangaza matangazo mapya kuongeza maeneo mapya.
"Mfano sasa hivi tumeongezewa maeneo nje ya Mwanza mjini ikiwemo Magu na Misungwi, miaka ya nyuma kabla ya kuundwa kwa RUWASA maeneo ya pembezoni ya Mwanza yalikuwa yanasimamiwa na Wizara ya Maji kupitia Idara za maji Mikoa lakini kwa miaka michache iliyopita ikaundwa RUWASA ili kutoa huduma ya maji maeneo ya Vijijini kabla ya RUWASA miradi yote ilikuwa inasimamiwa na halmashauri za maeneo husika walikuwa wanadizaini wenyewe wanatumiwa fedha kujenga kulingana na wanavyoona mazingira yao yamekaaje " anasema Oscar.
Anaongeza kusema " Miradi yote unayoizungumzia kwa maana ya wilaya ya Ilemela ilikuwa inajengwa na halmashauri na ilikuwa imesuasua sana baadae ilikabidhiwa RUWASA na sasa inasimamiwa na MWAUWASA. Tulipokabidhiwa tuliikamilisha kwa jinsi ilivyokuwa imedizainiwa na kwa fedha zilizokuwepo, mfano kama mradi halmshauri ilitumia Milioni 500 zikabaki Milioni 250 tuliendelea kukamilisha kukamilisha kwa fedha hizo hizo, huwezi kubadili au kufanya chochote tofauti na ulivyopewa kwahiyo tunachangamoto kubwa ya maeneo hayo ile miradi ni ya muda mrefu na ilidizainiwa kabla ya 2010 na 2013 ikajengwa " anasema.
Oscar anasema kuwa serikali ina nia njema na wananchi wake,imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto za maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama na bado inaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuwasogezea wananchi huduma za maji safi na salama kama Sera ya Taifa inavyosisitiza.
Mwandishi wa makala hii akatembelea Tovuti ya Wizara ya Maji www.maji.go.tz kufahamu kama mitaa isiyokuwa na huduma ya maji safi na salama kata ya Bugogwa imeingizwa kwenye mpango wa bajeti ya 2022/2023 kwa ajili ya kupatiwa fedha za mradi wa maji kwenye mitaa hiyo.
Hotuba wa Waziri wa Maji Jumaa Aweso (MB) iliyowekwa kwenye Tovuti hiyo ya Wizara ya Maji aliyoiwasilisha Bungeni ya Makadilio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Wizara ya Maji kwa mwaka 2022/2023, ikionesha vipaumbele na mpango wa utekelezaji kwa mwaka huo wa fedha.
Bajeti hiyo inaonesha kuwa miradi 175 ya maji safi na usafi wa mazingira mijini itatekelezwa kwa mwaka 2022/2023 ambapo Mwanza Jiji utafanyika upanuzi wa mtandao wa maji safi katika maeneo ya pembezoni mwa mji wa Mwanza, Kayenze, Igombe,Shibula, Lwanhima na Sangabuye ambapo fedha za Serikalini kupitia mfuko wa maji wa Taifa (NWF) kiasi cha Tsh. 350,000,000 zitatumika.
Wananchi wanaiomba serikali kupitia Wizara ya Maji ambayo ni mtekelezaji wa Sera ya Maji ya Taifa kuwasaidia wapate maji safi na salama ili kuwaepusha na magonjwa yatokanayo na matumizi ya Maji machafu.
Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM) kina Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 -2025 inayoielekeza Serikali kutekeleza yale yaliyomo kwenye Ilani ikiwemo Ibara ya 9 inayosema kuwa Chama kitaielekeza Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya Afya, Elimu, Maji, Umeme na makazi Vijijini na Mjini.
Pia kuongeza kasi ya usambazaji maji safi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 Vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mjini kwa upande wa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025 imeeleza Ilani ya CCM.
Ilani hiyo Ibara ya 10 inasema kuwa CCM itahakikisha Serikalini yake inatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa katika ilani.
Post a Comment