CORDS YAJENGA DARASA KUWASAIDIA WANAFUNZI WA MEMKWA LONGIDO
MKURUGENZI wa Shirika la Utafiti,Maendeleo na Huduma kwa Jamii (CORDS) Lilian Looloitai amesema Darasa maalum lililojengwa ili litumike kwa wanafunzi wanaosoma kupitia mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto walioikosa (MEMKWA)litakuwa fursa ya pekee kuwezesha watoto hususani wakike kupata elimu ya msingi.
Mkurugenzi huyo amesema hayo wakati wa kukabidhi Darasa lililojengwa na CORDS katika shule ya msingi Ngoswak iliyopo kata ya Engareinabor wilaya ya Longido mkoani Arusha, kwa gharama ya Tsh. Milioni 33.5 lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45, lengo likiwa ni kuwezesha vijana wa Jamii ya Kimasai wa kike na kiume waliokosa fursa ya kusoma wapate elimu.
Amesema mazingira ya jamii za pembezoni hususani wafugaji wa kimasai yanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo hupelekea watoto kutopata nafasi ya kuanza masomo kutokana na kukosekana madarasa maalum ya MEMKWA hali inayosababisha baadhi yao kutojiunga na masomo ya elimu ya msingi.
Ameongeza kwamba mwaka 2019 na 2020 walikuwa na mradi wa kuandikisha wanafunzi wa MEMKWA wapatao 20 na kuanza kufundishwa shuleni hapo lakini hakukuwa na darasa la MEMKWA hivyo kukosa chumba maalum cha kuwafundishia na kupelekwa kusoma kwenye madarasa ya shule hiyo ya msingi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Longido, Simon Laizer amelishukuru shirika la CORDS na wafadhili shirika la Douglas Scott Foundation la nchini Australia kupitia mradi wa Action on poverty kujenga darasa .
"Darasa hili litasaidia sana vijana ambao hawakusoma katika mfumo rasmi litasaidia kupambana na ujinga na umasikini," amesema.
Mkurugenzi wa shirika la Douglas Scott foundation kutoka Australia, Adrian Scott amesema kuwa wanafurahi kusaidia ujenzi wa darasa kwani litasaidia kuondoa ujinga kwa watoto na pia kuwezesha kujikwamua kiuchumi.
Mkuu wa shule hiyo Kwamboka Nyanami Phirace amewashukuru Cords kwa kuwajengea darasa hilo na kuahidi kushirikiana na uongozi wa kijiji kuhamasisha wazazi kuandikisha wanafunzi wa kutosha darasa hilo na wataanza masomo yao rasmi January 2023.
Post a Comment