HEADER AD

HEADER AD

SINTOFAHAMU YA CCM KUMFUTA UANACHAMA MWENYEKITI WA KIJIJI

 


Na Dinna Maningo, Tarime

KAMATI ya Siasa ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapindizi (CCM)Tawi la Nyangoto kata ya Matongo-Nyamongo wilaya ya Tarime mkoani Mara, imemfutia uanachama Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi ambapo pia Kamati ya Siasa Kata ya Matongo imebariki kufutiwa uanachama.

Hata hivyo Mwandishi wa Habari alipotaka ufafanuzi kutoka kwa viongozi hao ngazi ya Tawi na Kata kufahamu nini sababu za kumfutia uanachana hawakuwa tayari kueleza sababu za kufutiwa uanachana.

Habari kutoka kwa baadhi ya Wanachama wa CCM zinasema sababu ya mwenyekiti Mwita Msegi kufutwa uanachama ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Chama kumtuhumu kuwa amekuwa na utovu wa nidhamu pamoja na kujihusisha na vitendo vya Rushwa.

Wana CCM wengine wamedai kuwa kuwepo kwa Makundi ndani ya CCM na Serikali ya kijiji wenye maslahi binafsi kwa lengo la kunufaika na miradi ya Jamii inayojengwa kwa fedha za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Gazeti hili limezungumza na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Matongo-Nyamongo wilaya ya Tarime Boniphace Mwita Waitaro kutaka kufahamu sababu za Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi kufutwa uanachama alisema

"Hayo yapo nje ya uwezo wangu waulize viongozi wa Tawi, kamati ya siasa ya kata haina mamlaka ya kumfuta uanachama sisi tuliletewa taarifa tukaa kikao cha pamoja tukapitia tukaamua na kabariki kufutwa uanachama"alisema Boniphace.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Nyangoto Emanuel Boazi alipoulizwa sababu ya kumfutia uanachama Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi alisema 
"Mimi ni Mwenyekiti ni mwendesha vikao sina majibu ya kukupatia naomba uongee na Katibu wa Tawi yeye ndiye anahusika na shughuli za utendaji wote wa ofisi"alisema Emanuel.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Nyangoto- Nyamongo wilayani Tarime Selina Muhiri, alisema kuwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama hicho Tawi ilitoa mapendekezo ya kufutwa uanachama Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi japo hakutaka kuzitaja sababu zilizosababisha kumfuta uanachama.

"Kamati ya Siasa ina wajumbe 9 yumo na Diwani ambaye ni mkazi wa Tawi hili, mapendekezo ya kumfutia uanachama tulipeleka kwenye Chama Kata nao wakajadili wakapitisha wakapeleka na wilayani,bado hajapewa barua ya kufutiwa uanachama na anaendelea na nafasi yake ya uenyekiti tunasubiri uongozi wa wilaya ndio utatoa majibu"alisema Selina. 

Dima Online ilimtafuta Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime Varentine Maganga kufahamu kama ana taarifa za kufutwa uanachama Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi.

"Ni kweli nimepokea taarifa za kufutwa uanachama Mwenyekiti wa Kijiji,nitaenda Nyangoto nitakuwa na kikao na viongozi wa Chama Tawi na Kata kufahamu tatizo ni nini"alisema Valentine.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto kata ya Matongo-Nyamongo wilaya ya Tarime Mwita Msegi,amesema kuwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Nyangoto imemfuta uanachama kwa kile alichoelezwa kuwa amekuwa na utovu wa nidhamu baada ya kutohudhulia kikao cha Chama.

"Tangu uchaguzi wa chama ufanyike vimefanyika vikao vitatu kati ya vikao hivyo kikao kimoja ndio sikuhudhulia na nilitoa taarifa kwakuwa nilikuwa na kikao cha Serikali ya kijiji,kamati ya Siasa ya Tawi ilinifuta uanachama Septemba,12,2022 ilipofika Septemba,13,2022 Kamati ya Siasa Kata walikuja kujitambulisha kwenye Tawi na kuangalia uhai wa Chama.

"Baada ya mazungumzo Katibu wa CCM kata akiongea mbele ya viongozi wa kata na Halmshauri ya Tawi aliniambia kuwa nimefutwa uanachama,mimi sijawahi kuitwa kokote kuwa nimetenda kosa wala kuitwa kwenye kamati ya maadili nimefutwa uanachama kwa mdomo bila kupewa barua"alisema.

Katiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 14 imempa haki Mwanachama kujitetea nakueleza kuwa Mwanachama yeyote atakuwa na haki ya kujitetea au kutoa maelezo yake mbele ya kikao cha CCM kinachohusika katika mashtaka yoyote yaliyotolewa juu yake,pamoja na haki ya kukata rufaa ya kwenda katika kikao cha juu zaidi cha CCM kama kipo endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa.

No comments