WANANCHI,MADIWANI WAKERWA NA VUMBI BARABARA ILIYOKARABATIWA
Na Jovina Massano,Musoma
WANANCHI wa Mtaa wa Shabani Kata ya Kitaji wilaya ya Musoma mkoa wa Mara,wamesema wanapata kero ya Vumbi baada ya kufanyika ukarabati wa barabara kwa kiwango cha changarawe ambayo awali ilijengwa kwa kiwango cha lami.
Wakizungumza na Mwandishi wa DIMA Online wananchi wamesema ukarabati huo umesababisha kuwepo kwa vumbi katika barabara hiyo na hivyo kuathiri shughuli za biashara huku wakitaka kufahamu hatma ya marekebisho hayo kwa kiwango cha Lami.
Miongoni wanaodai kuathiriwa na vumbi Madina Zaidi amesema anapata shida anapofika kwenye duka lake la biashara ambapo analazimika kutafuta maji kumwagilia barabara ili kupunguza vumbi lakini baada ya saa chache vumbi inarejea tena.
"Binafsi napata shida sana ya vumbi inanilazimu nimwagilie maji ya kutosha na ni ya bomba bili inaongezeka na gharama za matumizi zinaongezeka sioni kinachoendelea viongozi watuambie hili vumbi tutaendelea nalo hivyohivyo au bado ukarabati kwa kiwango cha Lami utaendelea?.
"Tuna biashara zetu hapa wafanyabiashara tunateseka na hii vumbi bidhaa zinachafuka zinajaa vumbi wateja wakifika wanaona kama vyombo vimechakaa wateja wanapungua, nina mkopo nitakwama kulipa fedha za watu nitafirisiwa amesema", Madina.
Prisca Petro amesema, " Vumbi lina tuumiza sana hata tunashindwa kufanya biashara zetu kwa amani, isitoshe haya ni maeneo ya mjini vyombo vya moto vinapita kwa kasi sana tutaathirika afya zetu wahusika viongozi watueleze kinachoendelea kama ndio tayari au kuna mpango mwingine.
"Hii ni aibu kwa wahusika kwasababu hii ndio ilikuwa barabara ya kwanza ya mtaa kuwa na lami ni barabara iliyotumika kupitisha mwili wa baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wananchi walijipanga kuuaga mwili ukielekea Butiama,tunaona wametengeneza barabara ya vumbi hajiwekwa lami kami ilivyokuwa zamani iliyojengwa kwa kiwango cha lami", anasema Prisca.
DIMAONLINE imezungumza na viongozi wa kata ili kufahamu hatma ya ukarabati huo wa barabara ambapo viongozi hao wamesema hawakuwa na taarifa ya ukarabati wa barabara zaidi ya kuona Katapila likitengeneza barabara.
Diwani wa Kata ya Kitaji kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Golden Marcus amesema taarifa za ukarabati huo hakuzipata na kwamba alimuuliza Mtendaji wa Kata hiyo kama alipokea taarifa ya ukarabati wa barabara hiyo naye hakupata taarifa zaidi ya kuona Katapila likikwangua lami iliyokuwepo na kukarabatiwa kwa kuwekwa udongo pekee.
"Ukarabati huu umefanyika bila kushirikisha viongozi wa Kata binafsi nilivyoona zoezi linaendelea nikawapigia viongozi wenzangu kama wanataarifa ya ukarabati huu,mtendaji alisema hajui chochote nikamuuliza Diwani wa viti Maalum nae hakuwa na taarifa sikuishia hapo nikamuuliza Injinia wa Halmashauri nae hakuwa anajua chochote kuhusu ukarabati huu nikafika TARURA wakasema kuwa suala hili lilibarikiwa kwenye Baraza", amesema Golden.
Ameongeza" lilikuwa Baraza la dharura lililosimamiwa na Meya wa Manispaa pamoja na TARURA lilihusu uendelezaji na ukarabati wa kazi za TARURA katika manispaa, miongoni mwa ukarabati huo ni hii barabara ya Shabani wakiwa kwenye kikao hicho viongozi wa Kata hawakuafiki ukarabati wa kiwango cha Changalawe.
" Waliomba fedha hizo zitumike kufungua barabara mpya inayotokea mahakama ya Mwanzo kuelekea Tupendane huku barabara ya Shabani ikisubiria mradi mkubwa wa World Bank ambao muda wowote unaweza kuanza ", amesema Golden.
Diwani wa viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Asha Mohammed amesema "Huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa upande wetu sisi viongozi wa Kata tulitoa mapendekezo yetu na walisema wanatuunga mkono lakini sasa ukarabati umefanyika bila kutushirikisha tumekuwa tunasumbuliwa na wananchi juu ya adha wanayoipata ya vumbi.
", Wanapata shida sana japo kuna gari linapita kumwagilia maji mara moja moja bado changamoto ya vumbi ipo niombe kama mradi wa lami upo uwahishwe ili kupunguza kero na malalamiko kutoka kwa wananchi naiomba mamlaka husika ifanye kazi kwa wakati na tujue lini lami itawekwa.
,"Naelewa huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini ukarabati wa namna hii hauonyeshi kama lami itawekwa kwa wakati sisi tulisema ingesubiri mradi huo mkubwa ikwanguliwe na kuwekewa lami moja kwa moja tofauti na walichokifanya sasa"Amesema Asha.
DIMA Online inaendelea kumtafuta Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kufahamu kama barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha Lami au itabaki kwa kiwango cha changarawe! na kinachoelezwa na Madiwani kuhusu ujenzi huo.
Post a Comment