DC MBONEKO : TANESCO ACHENI KUWATUMIA MAFUNDI VISHOKA
Na Suzy Luhende,Shinyanga
MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuacha kutumia vishoka kwa ajili ya kuwafungia umeme wananchi, badala yake watumie mafundi ambao wamesajiliwa na wana leseni zao ili kuepusha matukio mbalimbali yanayosababishwa na Umeme.
Aliyasema hayo wakati akiwa amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema kwenye ufunguzi wa semina ya mafundi umeme Kanda ya Ziwa ilyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliyofanyika mjini Shinyanga, ambayo imehusisha mafundi kutoka mikoa minne, Geita Mwanza Simiyu na Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (aliyesimama)
"Natoa maelekezo kwamba Tanesco Shinyanga acheni kuchukua mafundi ambao ni vishoka chukueni mafundi ambao wapo kwenye makundi waliosajiliwa na wana leseni ili wakawafungie umeme wananchi, ni kosa kubwa kuchukua mtu ambaye hana leseni, tukikuta fundi anafanya kazi huku akiwa hana leseni tunamshughulikia "amesema Mboneko.
"Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu hataki kuona umeme unapelekwa kwa wananchi unaleta madhara, hivyo pelekeni mafundi wanye leseni hata likitokea tatizo anajulikana ni nani aliyefanya kazi, na hili lifanyike kwenye maeneo yetu sitakubali katika wilaya yangu mafundi wasio na leseni,"amesema Mboneko.
Mafundi umeme kutoka mikoa mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja
Aliwaomba Ewura, Temesa, Veta na Tanesco wafanye kazi yao ipasavyo, kazi wanayoifanya ni kazi ya muhimu, kwani umeme unaleta madhara endapo utatengenezwa chini ya kiwango, pia aliwaomba wawaelimishe wananchi waweze kutumia watu wenye leseni na wawe wanakaguliwa.
Meneja wa Ewura kanda ya ziwa George Mhina amesema kazi ya Ewura ni kudhibiti bei kubwa ambayo mtu anajiwekea mwenyewe na kuachana na bei elekezi hiyo haitakiwi pia tunatoa leseni kwa mafundi wenye kiwango cha kufanya kazi.
Meneja wa Ewura kanda ya ziwa George Mhina akizungumza
"Lengo letu sisi Ewura ni kudhibiti ufungaji holela wa umeme na kuhakikisha kazi hiyo inafanywa kitaalamu, weledi na kwa ujuzi, ili kuondokana na matukio mengi ya kuungua kwa nyumba na kuteketeza mali za wananchi, hivyo tukaona tuwaunganishe mafundi kutoka mikoa hii tukutane nao ili tuweze kukumbushana jinsi ya kutoa huduma kwa wananchi ili kuondokana na matukio haya,"amesema Mhina.
Lucy James ambaye ni fundi umeme mkazi wa manispaa ya Shinyanga alisema ili kuondokana na matukio ya mara kwa mara ni vizuri serikali ikazingatia kutoa kazi kwa wakandarasi wenye leseni ambao wanaweza kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa.
Fundi umeme Lucy James akizungumza jinsi ya kujiepusha na vishoka.
Post a Comment