UKOSEFU MAENEO YA MALISHO UNAVYOITESA MIFUGO,WAFUGAJI TARIME
>Wafugaji walazimika kuswaga Ng'ombe usiku kusaka malisho
>Watembea zaidi ya km 5 kusaka malisho
>Waliwa na Mamba wakienda malishoni
Na Dinna Maningo, Tarime
MIFUGO ni hitaji kubwa katikaTaifa na Jamii, ni chanzo mojawapo cha mapato na imekuwa ikiwezesha wananchi kujipatia mahitaji mbalimbali ya kijamii pamoja na shughuli za kilimo.
Vilevile upatikanaji mbolea ya Samadi, mazao ya mifugo kama maziwa, nyama na hutumika kutoa mahari kwa watu wanaofikia umri wa kuoa mwanamke.
Pamoja na umuhimu wa mifugo, kumekuwepo na ufugaji usio bora kama kupigwa mijeredi inapokuwa inalima na kupelekwa malishoni, hulala nje kwenye mazizi yaliyojaa vinyesi vyao na kupigwa baridi, kunyeshewa mvua kupigwa jua wamezoea, inapopata magonjwa kupata kinga na tiba ni adimu.
Ukosefu wa maeneo ya malisho ni tatizo linalozidi kuongezeka siku hadi siku katika vijiji mbalimbali hapa nchini jambo ambalo limekuwa likivunja mahusiano mazuri baina ya wafugaji na wakulima na kusababisha kuibuka migogoro.
Migogoro hiyo hutokea wakati mifugo inapoingia kwenye mashamba na makazi ya watu kwa lengo la kujipatia chakula kwakuwa baadhi ya mifugo hufanya uharibifu wa mimea yakiwemo mashamba ya wakulima yenye mazao.
Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, ukosefu wa malisho umesababisha baadhi ya wafugaji kubuni mbinu ya kulisha mifugo yao nyakati za usiku, huamka usiku kuswaga ng'ombe kwenda kutafuta malisho kwenye maeneo ya watu yenye nyasi kwakuwa muda huo wenye mashamba wanakuwa wamelala.
Wanafanya hivyo kwasababu baadhi ya vijiji havina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho, msimu wa kilimo unapofika hali ni mbaya kwa mifugo mashamba mengi yanakuwa hayana nyasi yamelimwa mazao, hivyo hutegea nyakati za usiku watu wakiwa wamelala kupeleka mifugo maeneo ya watu yenye malisho.
DIMA Online inafunga safari hadi Nyamongo katika baadhi ya vijiji vinavyokabiliwa na ukosefu wa maeneo ya malisho, Mwandishi anapata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji kufahamu hali ilivyo kuhusu ukosefu/uhaba wa malisho na njia zipi wanazozitumia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa malisho, nao walikuwa na haya yakusema;
Marwa Chacha mkazi wa Kijiji cha Nyabichune anasema kuwa mifugo inakabiliwa na ukosefu wa malisho kwakuwa maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa ajili ya malisho yamegeuzwa kuwa maeneo ya makazi.
"Tunahangaika sana mahali pakuchungia mifugo, watu wanaongezeka wanajenga kweye maeneo yaliyokuwa wazi ambayo tuliyatumia kulisha mifugo, tunalazimika kwenda porini kupeleka mifugo ili ikapate nyasi za kula" anasema.
Marwa Matiko mkazi wa kijiji cha Kerende anasema kuwa ukosefu wa maeneo ya malisho umesababisha mifugo kula mazao kwenye mashamba ya watu na hivyo kuibua migogoro baina ya wafugaji na wakulima na kusababisha chuki dhidi yao lakini pia mifugo kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga inapokutwa kwenye mashamba ya watu.
Wafugaji waswaga mifugo usiku kusaka malisho
Mwita Ryoba mkazi wa kijiji cha Kerende anasema maeneo yaliyotumika kulisha mifugo yamegeuka kuwa makazi ya watu nakusababisha ukosefu wa malisho jambo ambalo limesababisha baadhi yao kuamka usiku kulisha mifugo kwenye maeneo ya watu.
"Maeneo ya malisho ni shida kila eneo ukienda kuchunga unaambiwa ni la mtu tofauti na zamani tulikuwa tukichunga eneo lolote bila kuzuiliwa, inabidi uvizie wakati watu wamelala majira ya saa tisa usiku unaamka unaswaga ng'ombe kwenda kwenye mashamba ya watu ambayo hayana mazao unalisha ikishiba unarudisha nyumbani kukikucha hakuna wakujua kuwa wewe ndiyo ulienda kulisha/kuchunga kwenye shamba lake"anasema.
Joseph Chacha mkazi wa kitongoji cha Kegonga B kijiji cha Matongo anasema wanalazimika kuchunga usiku kama njia ya kuwezesha mifugo kupata chakula kwakuwa wakichunga mchana kwenye maeneo ya watu huzuiliwa.
" Wakati wa serikali ya Hayati Julius Nyerere ilikuwa inatenga maeneo ya malisho na serikali ya awamu ya kwanza ilijali wafugaji ilikuwa ikitoa bure dawa za mifugo na chanjo tofauti na serikali za awamu zilizofuata hazijaweka mkazo kwenye suala la malisho,hakuna maeneo ya malisho ukiuguliwa mfugo ununue dawa zako bado umgharamie usafiri afisa mifugo kuja kukutembelea.
Anaongeza" Serikali inasema kuwa tufuge ng'ombe wachache hivi wafugaji wote nchini tukisema tufuge ng'ombe 5 kila mtu, watapata wapi nyama, ngozi maziwa ya kutosha? msibani lazima ukute nyama,arusi,majumbani mikutano na hotelini.
"Wabunge wanashindwa kutetea wafugaji lakini wakitoka kwenye vikao vya bunge wakiingia hotelini wao ndiyo wa kwanza kuomba nyama nzuri na maziwa,hii mifugo ndio imewakuza watanzania walio wengi"anasema Joseph.
Watembea zaidi ya km 5 kusaka malisho.
Tatizo la malisho limeelezwa kuwa ni changamoto kubwa ambayo imesababisha baadhi ya wafugaji kuishi mbali na mifugo yao na kuipeleka kuishi porini ili kupata malisho kama njia ya kuinusuru mifugo kutokumbwa na balaa la njaa.
Ketemba Ketemba mkazi wa kijiji cha Matongo kata ya Matongo anasema"Baada ya maeneo ya malisho kuwa shida wafugaji wenye mifugo mingi wamehamisha mifugo yao na kuipeleka eneo moja linaitwa Mkora, lenye nyasi ambalo ni maeneo ya watu ambayo bado hayajatumika kwenye kilimo zaidi ya malisho ya mifugo.
"Kwenda huko ni mwendo wa km 5 ukienda kwa pikipiki ni 6,000 kwenda na kurudi, ukifika unanunua eneo nusu eka unatoa ng'ombe mbili unapewa eneo la kulaza mifugo yako tumejenga vibanda watu wanaishi kwa ajili ya kulinda mifugo mnaungana watu watatu au wawili mnachanga pesa ya kumlipa mlinzi ukiwa na ng'ombe 50 unamlipa mlinzi 30,000 ,ukiwa na ng'ombe 10 malipo ni elfu 20,000 kwa mwezi" anasema Ketemba.
Ketemba anasema kuwa wakati wa mvua wafugaji hulazimika kuondoa mifugo na kuirejesha nyumbani kwakuwa eneo hilo wanalolisha mifugo wakati wa mvua maji hujaa na kufunika malisho hivyo kukosa malisho.
Marwa mkami anasema kuwa umbali mrefu kwenda kuchunga mifugo husababisha mifugo kukonda"unatembea km 5 hadi 10 kuswaga mifugo kwenda malishoni mchungaji anachoka lakini hata chakula wanachokula mifugo wanapotembea umbali mrefu wanachoka sana kuja ifike nyumbani chakula chote kinakuwa kimeisha tumboni"anasema.
Marwa Chacha anasema kuwa eneo la Turuturu lililotengwa kwa ajili ya malisho nalo limevamiwa na wakulima ambao hulima mazao lakini pia migogoro ya mipaka kati ya kijiji cha Matongo na kijiji jirani cha Nyarwana kata ya Kibasuka ilisababisha watu kutopeleka mifugo kwenye malisho eneo hilo.
"Serikali ilitenga eneo la malisho lakini migogoro ya mipaka kwenye eneo hilo kati ya kijiji cha Matongo na Kitongoji cha Mwara ilisababisha kuzuka kwa mapigano baadhi ya watu kujeruhiwa na hata kufa hali iliyopelekea wafugaji wengine kuogopa kwenda kulisha mifugo kwenye eneo hilo.
"Baadhi ya watu wamevamia hilo eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho na kulima mashamba, kwa sasa maeneo ya malisho hayatoshelezi mahitaji ya mifugo tunachunga kwa kupenyapenya sehemu zenye uwazi kiukweli malisho sio ya uhakika ni yakubahatisha "anasema Chacha.
Daniel Charles mkazi wa Matongo anasema kijiji hicho hakina eneo rasmi la malisho, wafugaji huchunga mifugo yao eneo la Turuturu ambalo lilikuwa pori lakini kwa sasa limekuwa ni changanyikeni watu wanalitumia kulima mashamba na makazi.
"Eneo la kwinyunyi ndio lilikuwa linatumika kwa malisho lilichukuliwa na Mgodi wa North Mara kwa ajili ya shughuli za mgodi watu wakahamishwa, kwa sasa wanapeleka mifugo yao Turuturu ambalo nalo si salama lina uhasama kijiji cha Matongo na Nyarwana wanaligombania lilishasababisha kuzuka kwa vita na watu wakajeruhiwa wengine kuuwawa wakigombania hiyo ardhi"anasema Daniel.
Daniel anashauri kuwa ni vyema Serikali ikatenga maeneo rasmi kwa ajili ya malisho ili kuepusha changamoto za malisho na inapotenga iweke alama za mipaka ili kupunguza uvamizi wa maeneo ya malisho.
Anaongeza kwamba Nyamongo ina changamoto kubwa ya ukosefu wa malisho hali inayolazimu baadhi ya wafugaji kwenda kuchunga mifugo yao wilaya jirani ya Serengeti, nako huzuiliwa kwakuwa wanatoka wilaya nyingine.
Waliwa na mamba wakisaka malisho
Mwenyekiti wa kijiji cha Kerende Mniko Magabe anasema kuwa ukosefu wa malisho unawalazimu wafugaji kuivusha Mifugo mto Mara kuipeleka vijiji jirani wilaya ya Serengeti kutafuta malisho.
Anasema kuwa hali hiyo imesababisha baadhi ya mifugo na wachungaji kuliwa na mamba wakati wakivuka mto na wengine kusombwa na maji na kufa wakati wakivuka mto.
"Malisho ni shida sana,makazi ya watu yameongezeka maeneo ya kuchungia mifugo hayapo ,watu wanalazimika kuvuka mto Mara kupeleka ng'ombe kula nyasi wilaya jirani ya Serengeti,mifugo inaliwa na mamba.
"Mingine inasombwa na maji inakufa,maji yakiwa mengi wachungaji nao wanazama na kupoteza maisha,tunaomba serikali ije na mbinu mpya ili kuondoa changamoto hii ya malisho mifugo inateseka na wafugaji wanateseka"anasema Mniko.
Ng'ombe,Mbuzi na Kondoo ni hitaji kubwa katika maisha ya mwanadamu wanastahili haki zote kama wazipatazo binadamu ikiwemo malisho ya uhakika na tiba ili kuongeza thamani itokanayo na mifugo.
.....Itaendelea
Post a Comment