HEADER AD

HEADER AD

WATOTO MILIONI TATU WANA UDUMAVU



Na Annastazia Paul Simiyu.

IMEELEZWA kuwa hali ya lishe nchini Tanzania bado si nzuri licha ya nchi kua na uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula, ambapo bado idadi ya udumavu kwa watoto ni kubwa inayofikia zaidi ya watoto 3,000,000.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho kuelekea siku ya chakula duniani, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Simiyu, mwakilishi wa katibu mkuu wa wizara ya kilimo, Dk. Mashaka Eliud Mdangi amesema hali hiyo inasababishwa na jamii kutotambua umuhimu wa kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula kwa afya bora.

“Pamoja na kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula, bado hali ya lishe nchini si nzuri japokuwa taarifa zinaonesha kuwa maendeleo ni mazuri katika kupunguza utapiamlo, takwimu zinaonesha kuwa udumavu umepungua kutoka asilimia 42 hadi asilimia 32 kwa mwaka 2010 na mwaka 2018, na ukondefu umepungua kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 3.5 kutoka mwaka 2014 hadi 2018”  amesema Mdangi. 


      Mwakilishi wa katibu mkuu wa Wizara Dkt. Mashaka Eliud Mdangi

Amesema hali hiyo ipo chini ya kiwango cha malengo ya mkutano wa afya duniani cha asilimia 5, pamoja na mafanikio hayo bado idadi ya watoto wenye udumavu ni kubwa ambapo zaidi ya watoto 3,000,000 nchini wana udumavu.

“Hali hii iko chini ya kiwango cha malengo ya mkutano wa afya duniani cha asilimia 5, pamoja na mafanikio haya bado idadi ya watoto wenye udumavu ni kubwa mno zaidi ya 3,000,000 hali ambayo haikubaliki, hali hii imesababishwa na kiwango kikubwa cha jamii kutotambua umuhimu wa kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa makundi mabalimbali ya vyakula ili kuwa na afya bora.” amesema Mdangi.

Charles Tulahi ni mwakilishi wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO, ambaye anaeleza kuwa hali ya chakula duniani siyo nzuri kwani asilimia 40 ya watu wote duniani hawapati mlo kamili unaoweza kuwafanya wawe na afya bora.


Mwakilishi wa FAO Charles Tulahi

“Hali ya chakula duniani siyo nzuri sana, karibu theluthi mbili ya watu duniani wana upungufu wa lishe ya chakula ambacho kinampatia mtu lishe bora, watu wanaokabiliwa na upungufu duniani kote ni karibu 3.1 sawa na asilimia 40 ya watu wote ambao hawapati mlo sahihi wa kuwaletea afya bora kila siku.” amesema Tulahi,

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ametaja kiwango cha udumavu mkoani humo kuwa kipo juu ya wiwango vinavyowekwa na mashirika ya kimataifa ya WHO na UNICEF huku akiwasisistiza wazazi mkoani humo kuwapatia mlo kamili watoto wao ili kuwaepusha na utapiamlo.

  
     Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda

“Takwimu zinaonesha kuwa hali ya udumavu katika mkoa wa Simiyu ni asilimia 31.2, viwango vya udumavu zaidi ya asilimia 30 ni vya juu kwahiyo katika mkoa wetu kuna kiwango cha juu cha udumavu kwa kadri ya viwango vinavyowekwa na mashirika ya kimataifa yaani WHO na UNICEF ambayo ni chini ya asilimia 20.

"Juhudi zinahitaji ili kuhakikisha viwango hivi tunavishusha kwa mkazo mkubwa ikiwa ni katika kubadili tabia ya ulaji kwa kuzingatia mlo kamili wa ulaji kwa bora watoto wetu, watoto wakikosa lishe bora na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaweza kukabiliwa na changamoto nyingi za lishe na kupata utapiamlo.” amesema Dkt Nawanda.

Maadhimisho ya siku ya chakula duniani mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo,"Uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora, na maisha bora kwa wote, habaki mtu nyuma", ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Simiyu.
                                                 


                                   

         

   

No comments