DEREVA AFARIKI KWA AJALI,RPC NA MSAIDIZI WAKE WAJERUHIWA
KAMANDA wa Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda amejeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso mita chache kabla ya kufika eneo la mzani Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa huo ACP Shadrack Masija amesema ajali hiyo imetokea Oktoba 02 ,2022 majira ya 2:15 usiku barabara ya Bariadi - Lamadi baada ya gari yenye namba za usajili T. 462 BBD Toyota Harrier iliyokuwa ikiendeshwa na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda, kugongwa na gari yenye namba za usajili T. 766 CCZ Toyota Mark II iliyokuwa ikitokea Bariadi kwenda Lamadi.
Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na askari polisi F 5814 koplo ( CPL) Timoth Philipo Shadrack ambaye ni askari wa jeshi la polisi wilayani Busega, na kusababisha majeraha kwa madereva wote wawili na msaidizi wa kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu Emmanuel Kadelya.
" Kwenye gari ya kamanda Chatanda ambayo ilikuwa gari yake binafsi alikuwa na msaidizi wake wa kazini ,askari polisi H.7123 polisi Konstebo ( PC) Emmanuel Kadelya na wote watatu walikimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu kwa ajili ya matibabu lakini askari polisi Timoth Philipo Shadrack alifariki dunia Oktoba 3, 2022 akiwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo " amesema ACP Masija
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu ACP Masija amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari yenye namba za usajili T 766 CCZ aina ya Toyota Mark II ambaye alihama upande wake kwenda upande wa kulia kisha kuigonga uso kwa uso gari aina ya Toyota Harrier yenye namba za usajili T 462 BBD iliyokuwa ikiendeshwa na kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda.
Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu linatoa pole kwa familia ya askari polisi huyo aliyepoteza maisha na litashirikiana na familia ya marehemu katika shughuli zote za mazishi ambayo yatafanyika wilayani Magu mkoani Mwanza .
Post a Comment