SIMIYU YAJIPANGA MAONESHO WIKI YA CHAKULA
Na Annastazia Paul,Simiyu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dk.Yahaya Nawanda
MKOA wa Simiyu unatarajiwa kuwa mwenyeji wa wiki ya chakula duniani kitaifa ambayo itaadhimishwa kuanzia Oktoba 10 hadi 16 mwaka huu 2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, mkuu wa mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuchochea na kuhamasisha uzalishaji na upatikanaji wa chakula bora na salama mkoani humo na taifa kwa ujumla, ikiwa ni sambamba na maagizo ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu aliyewataka wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanaboresha lishe katika kaya za mikoa yao.
"Rais ametutaka wakuu wote wa mikoa na wilaya kuhamasisha wananchi kupata lishe bora katika ngazi ya kaya ili kuongeza ufanisi na kupunguza udumavu katika kaya zetu" amesema Dk. Nawanda.
Mkuu huyo wa mkoa wa Simiyu amesema ili kukamilisha maandalizi ya maadhimisho mkoa utashirikiana na wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, afya, washirika wa maendeleo wakiongozwa na shirika la chakula na kilimo duniani FAO.
Amesema kuwa maadhimisho hayo yataambatana na utoaji wa elimu ikiwemo maonesho ya teknolojia mbalimbali za uzalishaji, usindikaji, uhifadhi, uandaaji wa chakula, ulaji bora pamoja na huduma zingine zinazotolewa na wadau na taasisi mbalimbali katika mnyororo wa thamani.
"Tunaenda kuwaonesha wananchi sisi watu wa Simiyu tunalima nini na tunazalisha nini, lakini pia tunakula nini, kwahiyo ni fursa mojawapo kuja kuona chakula cha wananzengo mfano matobolwa, choroko, dengu, ugali mwekundu, uwele n.k." Amesea Dk. Nawanda.
Dk. Nawanda ameitaja idadi ya mifugo iliyopo mkoani humo wakiwemo ng'ombe 1,500, 093, mbuzi zaidi ya 7,700,071 kondoo 200,089 pamoja na kuku zaidi ya 2,300,000 hivyo wananchi wataenda kuhamasika kupitia mazao ya mifugo ambapo mkoa huo ni wa tatu kwa ufugaji.
Maonesho hayo yanaenda sambamba na kauli mbiu isemayo" uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora kwa wote habaki mtu nyuma " huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa waziri wa kilimo Hussein Bashe.
Post a Comment