DKT. MOLLEL: MAISHA YETU YAPO MIKONONI KWENU
Na Englibert Kayombo-WAF, Dar es Salaam.
WATAALUMA wa Maabara ni kiungo muhimu katika upatikanaji wa matibabu sahihi kwa mgonjwa,lakini wakikosea matokeo ya uchunguzi ugharimu maisha ya watu.
Kwakutambua umuhimu huo,Serikali imewataka wataaluma wa maabara kuboresha ubora wa huduma za maabara ili kuwezesha upatikanaji wa matokeo sahihi ya uchunguzi wa magonjwa yatakayowezesha wananchi kujua afya zao pamoja na kupata matibabu sahihi.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema hayo Octoba,6,2022 akiwa amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwenye ufunguzi wa Kongamano la 35 la Kisayansi la Wataalam wa Maabara lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.
“Watu wa maabara mkikosea, matokeo yake yanaonekana mara moja na wakati mwingine yanagharimu maisha ya watu, Waziri mkuu amewaomba mkifika kwenye maeneo yenu ya kazi mkasimamie ubora wa huduma kwa sababu maisha yetu yapo mikononi kwenu” amesema Dkt. Mollel.
Amesema wanataaluma wa maabara ni kiungo muhimu katika upatikanaji wa matibabu sahihi kwa mgonjwa hivyo Serikali inatambua na kuthamini mchango wao katika kuboresha huduma bora za afya nchini.
“Tumepitia vipindi vya milipuko tofauti ya magonjwa ikiwemo, UVIKO-19, Homa ya mgunda na sasa Ugonjwa wa Ebola nyie mmekuwa msingi wa kutuvusha na kutuweka sisi salama” amesema Dkt. Mollel
“Maabara ni moyo wa Hospitali, Hospitali zetu zinetegemea ufanisi wa Idara hii kwa ajili ya usalama wa afya zetu, tunawashukuru sana” amesema Dkt. Mollel.
Ameongeza kuwa serikali imepokea changamoto iliyowasilishwa ya masuala ya kimuundo wa utumishi wa kada ya wataaluma wa maabara na kuahidi kuwa maoni ya wadau hao yamepokelewa na Serikali itayafanyia kazi ili kuwa na muundo wenye tija na kuinua taaluma hiyo.
Mtaaluma wa Maabara ni mtu anayetoa majibu sahihi ya uchunguzi wa kimaabara ili kumsaidia daktari kufanya maamuzi sahihi ya kimatibabu kwa mgonjwa.
Post a Comment