HEADER AD

HEADER AD

UKOSEFU KITUO CHA KUPOZA UMEME NI KERO KWA WATEJA




Na Mwandishi Wetu,Simiyu

UKOSEFU wa Kituo cha kupoza Umeme ni moja ya sababu inayochangia kutokuwepo kwa huduma ya uhakika ya umeme katika mkoa wa Simiyu,hali ambayo imesababisha Shirika la Umeme (TANESCO) kulalamikiwa na wananchi umeme unapokatika.

Shirika hilo limekiri kuwepo kwa changamoto kubwa katika upatikanaji wa umeme wa uhakika kwani limekuwa likitegemea vituo vya kupoza umeme kutoka mkoa wa Mara,Shinyanga na Mwanza.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuwatembelea wateja wanaopata changamoto ya umeme Octoba 6,2022 ikiwa ni wiki ya huduma kwa wateja, Meneja wa Shirika la Umeme mkoa wa Simiyu, Alistidia Clemence amesema mkoa huo una changamoto kubwa ya umeme na kwamba wanazichukulia kama fursa katika kuboresha huduma.

"Shirika linaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba huduma zinaimarika na zinakuwa nzuri ili wateja wazidi kufurahia na kuepuka hasara zinanazoweza kusababishwa na kutokuwa na umeme.



"Naomba tuwe na subira,tunaendelea kuboresha huduma zetu siku hadi siku ili changamoto zipungue, hakuna kituo cha kupoza umeme tunaendelea na mpango wa kujenga kituo cha kupozea umeme, tayari tenda zimetangazwa na mkandarasi atakapo patikana zoezi litaanza mara moja na changamoto zitapungua "amesema Alistidia.

Ameongeza kuwa huduma ya mfumo wa mtandao (Kidigitali) inayomwezesha mteja kupata huduma bila kufika katika ofisi za TANESCO (Ni-konekt) mkoa wa Simiyu imewezesha wateja 1340 kuunganishiwa umeme kupitia huduma hivyo kufanya jumla ya wateja wa TANESCO kufikia 3945 katika vijiji 269 na kusalia vijiji 201 ambavyo havijapata umeme.

Boaz Ogola ni miongoni mwa wateja wakubwa wanatumia nishati ya umeme kuendesha shughuli za uzalishaji kiwandani amesema umeme hukatika mara kwa mara hali inayokwamisha shughuli zao.

"Umeme unakatika ghafla unaleta madhara una tukwamisha kweye shughuli zetu za uzalishaji unapokatika yaani ni kero, tunalazimika kutumia nishati ya mafuta jambo ambalo linaongeza gharama za uzalishaji ikilinganishwa na uzalishaji wa kutumia umeme, unapokatika inapunguza ufanisi wa mashine inachukua muda zaidi  ili mashine ziwe sawa," amesema Ogola.

Huduma ya kuwafikia wateja majumbani imeambatana na kutoa zawadi kwa wateja wakubwa ambapo baadhi ya wateja wametunukiwa vyeti vya shukrani.

>>>Kwa mujibu wa Tovuti ya Wizara ya Nishati wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa wilaya 15 ambazo kutajengwa vituo vya kupoza umeme vitakavyoanza kujengwa Octoba ,2022 ambapo Serikali imetenga fedha Bilioni 500 katika mwaka wa fedha 2022/2023.

No comments