JUMUIYA KUU YA BAPTIST TANZANIA YAMWANGUKIA RAIS SAMIA
Na Fabian Fanuel,Mwanza
UONGOZI wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania, umemwangukia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu,kumuomba kuingilia kati kutatua migogoro ambayo imeibuka katika kanisa na kulifanya kushindwa kupiga hatua katika suala la imani na maendeleo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania Barnabas Ngusa amesema kanisa hilo limeshindwa kupiga hatua kama malengo yake kutokana na migogoro ambayo imeibuliwa na baadhi ya watu ambao wameanzia Imani nyingine.
"Tunashangaa sana sisi kama Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania tuna imani yetu maana kanisa hili limekuwepo muda mrefu. Lina makanisa mengi Tanzania nzima na nimeanzisha miradi mingi sana ila cha kushangaza ni baadhi ya watu wachache waliokengeuka ambao wameamua kuanzisha imani nyingine kwa imani yetu,Msajili wa Taasisi za Kijamii anajua na ameshindwa kulitatua.
"Sisi tuna katiba ambayo imesajiliwa na Msajili, kwanini aruhusu watu wengine walioamua kuanzisha imani yao, kubadilisha katiba na anajua fika sio viongozi halali? Tumeandika barua za kumwomba amalize mgogoro huo ila Msajili hajawahi kutusaidia, kila siku anatupiga danadana kama watoto wadogo"amesema.
Ameongeza "Baadhi ya Makanisa yetu yamefungwa na watu hawasali kama ilivyo kawaida yetu, baadhi ya mali za kanisa la miradi imechukuliwa na kubadilishwa majina na mingine kuuzwa bila ridhaa ya bosi ya wadhamini wa kanisa la Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania ambao ndio wamiliki wa mali zote.
"Tunamuomba Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan atusaidie kumaliza mgogoro huu. Sisi tunachotaka walioanzisha imani nyingine wanaendelea na imani yao na watuachie imani yetu ya kutoka zamani" amesema Barnabas Ngusa Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania.
Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania Mchungaji Nicholaus Luselele Nzella na Katibu Mkuu wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania Mchungaji Elias Kashambagani wamesema migogoro hiyo imeleta kudorora kwa kanisa na kulifanya lishindwe kustawi kama lilivyokuwa hapo awali kabla ya migogoro hiyo kuanzia.
Katibu wa Bodi ya wadhamini wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania Mwinjilisti Vicent Tebho na Mkurugenzi wa vijana Taifa Mchungaji Peter Sangija wameiomba Serikali ya Rais Samia kuingilia katika kuondoa ukengeufu huo ambao umejitokeza kwenye kanisa lao la Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania.
Kanisa hilo la Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania limekumbwa na migogoro takribani miaka mitatu sasa na ofisi ya Msajili wa Taasisi za Kijamii chini ya Ndugu Emmanuel Kihampa imeshindwa kuumaliza mgogoro huo.
Post a Comment