HEADER AD

HEADER AD

MIAKA 18 TANGU LITENGWE ENEO KUJENGWA SOKO BADO HALIJAJENGWA




Na Jovina Massano,Musoma

WAKAZI wa Kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamesema ni miaka 18 tangu litengwe eneo ili kujengwa soko lakini hadi sasa halijajengwa.

Wakizungumza na Mwandishi wa DIMA Online wamesema wanalazimika kutembea mwendo mrefu kufanya manunuzi ya bidhaa katika soko lililopo Kata ya Matare na Nyasho,hivyo wameiomba Halmashauri ya Manispaa hiyo kuruhusu kuanzishwa kwa soko hilo.


         Eneo lilitotengwa kujengwa soko

Catherine Kataka mkazi wa Mwisenge mtaa wa Mtakuja 'A' amesema " Tuna shida sana tunapotaka mahitaji ya nyumbani ukitaka kununua mboga unawaza namna ya kwenda Nyamatare, Nyasho, Nyakato au mjini,lazima ujipange nauli ya kwenda na kurudi zaidi ya 1000  hali yenyewe ya sasa ni changamoto mzunguko wa fedha ni mdogo tunaiomba serikali itusaidie hili soko letu lianze " amesema.

          Catherine Kataka

Nao wafanyabiashara wa Dagaa wakazi wa mtaa wa sokoni lililopo soko hilo wameiomba Halmashauri kuruhusu wananchi kuwekeza katika eneo hilo kwa kuwa ni muda mrefu tangu eneo hilo litengwe kwa ajili ya soko.

Wakazi hao wamesema kuwa kama Serikali imeshindwa kujenga soko iwaeleze ili wajenge wenyewe kwa madai kuwa eneo lilitengwa kwa ajili ya soko lakini imeshindikana kuanzishwa.

                Wakazi wa mtaa wa Sokoni

"Sisi tunaishangaa serikali kama hawawezi kujenga watupatie sisi wananchi tujenge, watupe utaratibu wa hapo ili tuweze kufanya biashara zetu kwa uhakika jirani na maeneo tunayoishi iwe rahisi kuangalia familia zetu " amesema " Sara Ndalo.

Tausi Hamis amesema " Kipindi cha Kampeni 2020 kuna mama anaitwa Joyce Sokombi aliliongelea soko hili sasa hatuelewi kama serikali ilimsikia mawazo yake ya umuhimu wa soko hili au ilimpuuza, tena Kata yetu ya Mwisenge yenye historia ya baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere ! "amesema.


Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sokoni George Faustine Mtete amesema  eneo hilo lilitengwa tangu mwaka 2004 kwa ajili ya soko Halmashauri iliwaruhusu wananchi kujenga lakini ujenzi ulipoanza waliwasimamisha wananchi hao na kuwaeleza kuwa wasubiri waletewe ramani ya namna ya kujenga katika eneo hilo na kuwapa mkataba.

"Halmashauri ilileta ramani haikuleta mkataba na kusababisha wananchi kushindwa kuendeleza ujenzi kwa kuhofia kupoteza haki zao hapo baadae naiomba halmashauri iwahishie mkataba huo ili kusaidia upatikanaji wa mahitaji na hata serikali kujipatia mapato katika eneo hili na ikiwezekana kuwepo gurio mara moja kwa wiki "amesema George.

     
Mwanasiasa na mfanyabiashara Joyce Bitta Sokombi amesema "ukiongelea Kata ya Mwisenge unaongelea kata pekee mkoani Mara inayofahamika kitaifa na kimataifa kupitia Hayati baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Mwisenge ambapo viongozi wengi hutembelea  shuleni hapo,lakini ni Kata inayosahaulika kwa huduma za msingi kwa wananchi wake kulingana na historia yake hiyo.


       Joyce Sokombi

"Mwisenge ni Kata kubwa lakini haina soko wakazi wa eneo hilo huenda Kata za jirani kujipatia huduma na kujitafutia kipato ilihali maeneo yaliyotengwa yapo yanayoweza kusaidia upatikanaji wa huduma za kijamii karibu. 

Joyce amesema kuwa ikifika wakati siasa za kukwamisha maendeleo kwa jamii ziachwe,viongozi waweke alama katika uongozi wao,huo ndio uwakilishi sahihi kwa wananchi.


 "Tunawashauri viongozi wa serikali kuwahudumia wananchi ipasavyo soko hili likiwepo serikali inaongeza chanzo kipya cha mapato badala ya kuweka tozo kwenye miamala tumsaidie Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ili kutengeneza mzunguko wa fedha kwa jamii na kukuza uchumi wa maeneo yetu,hii nchi ni yetu sote na Rais ni wetu tushirikiane  na yeye anahitaji mawazo yetu"amesema Joyce.

Ameongeza kuwa soko ni mradi wa maendeleo kwakuwa wananchi watawekeza katika soko hilo endapo ukiandaliwa utaratibu mzuri,amemuomba Mkurugenzi wa Manispaa kupitia wataalam wake wa Idara ya Biashara kuliangalia hilo na kulifanyia kazi kwa uharaka ili wananchi wa Mwisenge wajikwamue kiuchumi kuleta maendeleo na kuongeza mapato ya Serikali.



No comments