KILIMO BIASHARA CHA MBOGA MATUMAINI MAPYA KWA VIJANA WA KIJIJINI
Shamba darasa lililoandaliwa na vikundi vya vijana wa kijiji cha Matongo waliojiunga na Kilimo Biashara. |
Na Dinna Maningo,Tarime
VIJANA wanaoishi Vijijini Nchini Tanzania wanayo fursa kubwa ya kukuza Uchumi kwa kutumia ardhi iliyopo kijijni endapo watashiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo ambacho ndio msingi wa Maendeleo kwa Taifa.
Jarida la Mkakati wa Taifa wa Vijana kushirikishwa katika kilimo lililotolewa na Jukwaa la Wadau wa Kilimo wasio wa kiserikali (ANSAF) kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo la Septemba,2019 limeeleza dhumuni la kuchapishwa jarida hilo ni kuongeza uelewa wa vijana katika kutambua fursa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo na kuzifanyia kazi.
Mkakati huo ukiwa umelenga kuwakwamua vijana kutoka kweye changamoto ya ajira ili waweze kujiajiri kwenye sekta ya kilimo na kuchangia kukua kwa pato la taifa.
Katika Jarida hilo imeelezwa kuwa kwa mujibu wa Takwimu za Taifa (NBS,2014) utafiti unaonesha asilimia 56 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana hususani wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 na wengi wao hawana ajira.
Jarida limeeleza endapo vijana wakitambua fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo na kuzitumia vizuri,itasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kupunguza tatizo la umaskini kwa Taifa zima.
Jukwaa la wadau wa kilimo kupitia jarida hilo wanasema kumekuwepo na ushiriki mdogo wa vijana katika sekta ya kilimo huku vijana walio wengi wakijihusisha kwenye kilimo cha kutegemea mvua peke yake kilichopitwa na wakati,kwani mvua zinapokosekana au zikiwa kidogo na mahitaji ya mazao,hukauka yakiwa bado shambani hayajakomaa.
"Vijana wengi huchukulia kilimo kama kazi isiyo na staa wakiamini kwamba watapoteza muda wao mwingi wakiwa shambani,lakini sivyo kama wanavyofikiri,kilimo ni kazi yenye staha na ni taaluma kama zilivyo taaluma zingine.
"Kilimo kinatoa fursa za kazi katika uzalishaji,uchakataji, usindikaji na biashara kwa ujumla,hivyo vijana wanaweza kujiajiri na kuajiriwa kwenye sekta hiyo ya kilimo kuweza kufikia matarjio mazuri ya maendeleo binafsi na kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii" imeeleza kwenye jarida.
Wakulima wakichimba Mtaro |
Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Tanzania ya mwaka 2007 ambayo ni maboresho ya Sera ya mwaka 1996,inaeleza kuwa kijana ana haki ya kupata kazi na ujira wa haki ili kumudu maisha yake kwasababu jamii inategemea kumuona akishiriki katika shughuli za maendeleo na kuanza kujitegemea kwa kiasi fulani.
Sera hiyo ya maendeleo ya vijana inaeleza kuwa vijana walio wengi,asilimia 60 ya wale wote wasio na ajira rasmi hawana kazi maalumu.
Maeneo ya vijijiji yaliyo mengi yana ardhi kubwa na yenye rutuba nzuri ya kustawisha mazao kuwezesha vijana kuwekeza katika kilmo chenye tija cha kisasa ili kujiinua kiuchumi kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yatawapatia fedha kuyasongesha maisha yao na familia .
Licha ya kuwepo kwa ardhi ya kutosha maeneo ya vijijini bado maisha ya baadhi ya vijana ni duni japo wengine ni wakulima wa muda mrefu wanaomiliki mashamba waliyoyanunua kwa fedha au kumilikishwa na familia zao lakini siku nenda rudi maisha yao ni yaleyale yasiyo piga hatua.
Baadhi ya vijana nao wanajitetea wakisema ugumu wa maisha kwa vijana waishio vijijini unatokana kutopata elimu ya kilimo bora cha kisasa cha umwagiliaji na kilimo Biashara hivyo kubaki wakipanda mazao kwa mazoea kwa kutegemea msimu wa mvua pekee na zana za kilimo za kizamani.
Wanasema kuwa hali hiyo imesababisha wawe na maisha duni kwakuwa unafuu wa maisha wanaupata wakati wa msimu wa mavuno pekee unaowawezesha kuuza mazao na kupata fedha,baada ya hapo ni maumivu ya maisha.
Kijiji cha Matongo kilichopo kata ya Matongo-Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara, kina wakazi 7,000 kwa mujibu wa sensa ya 2012,idadi ya wakulima 1,050,ekari za kilimo ni 1,500, wanakijiji wanategemea shughuli za kilimo na ufugaji ambazo wameendelea kuzirithi na kuzidumisha kizazi hadi kizazi katika maisha yao.
Kijiji hicho kina vijana ambao wengi wao hawakubahatika kupata elimu ikiwemo ya msingi na sekondari, baadhi yao ni wakulima na wafugaji wakiwa hawana ajira mbadala,wengine hawana kazi wala kujiajiri hivyo kuendelea kulandalanda kijijini.
Kukosekana kwa ajira kwa vijana na kutojishughulisha na kazi zikiwemo za ujasiriamali na zinginezo,baadhi ya vijana walilazimika kutafuta njia mbadala ya kuingia ndani ya Mgodi wa Dhahabu North Mara kuchukua mawe yenye dhahabu kwa nia ya kujipatia fedha ili kujimudu kimaisha.
Kuingia ndani ya mgodi kinyume cha taratibu na sheria kukasababisha baadhi ya vijana wa Matongo na maeneo mengine kukamatwa na Polisi kwa makosa yakiwemo ya uhujumu uchumi,kujihusisha na biashara ya Madini bila kuwa na Leseni na kuingia kwa jinai,wapo baadhi walijeruhiwa,wengine kupata vilema vya maisha na wengine kuuwawa kwa kupigwa risasi wakiwa ndani ya mgodi.
Kitendo hicho kikasababisha kuvunjika kwa mahusiano mazuri baina ya mgodi, serikali na wananchi,chanzo kikubwa kikiwa ni tatizo la ajira kwa vijana iliyochangia waingie mgodini kutafuta riziki huku uongozi wa mgodi nao ukitupiwa lawama ya kutoajiri vijana wanaotoka vijiji vinavyouzunguka.
Wafanyabiashara nao wakilaumu kwamba mgodi umekuwa ukienda kununua bidhaa nje ya wilaya ya Tarime hususani katika mkoa wa Mwanza,Arusha,Dar es Salaam na nchi jirani ya Kenya ikiwemo nyama,nyanya na bidhaa zinginezo licha ya kuuzwa Nyamongo na maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Vijana Matongo wajiunga na Kilimo Biashara,Serikali ya Kijiji, Halmshauri,Mgodi wawaunga mkono.
Malalamiko ya wanachi wakiwemo vijana wa Kijiji cha Matongo kutopata ajira mgodini,Serikali kwa kushirikiana na Mgodi wa North Mara wamekuja na mbinu mpya ya kuwawezesha vijana wa kijiji hicho kujiuga na Kilimo Biashara cha Mboga ili kujipatia fedha badala ya kutegemea ajira mgodi pamoja na kuingia ndani ya mgodi kuiba mawe ya dhahabu.
Katika kuhakikisha vijana wanawezeshwa kiuchumi Mgodi wa North Mara umewafadhili vijana 100 kutoka kijiji hicho ambao wameunda vikundi vya watu kumi kwa kila kikundi na kuanzisha mradi wa Kilimo Biashara cha mboga,vitendea kazi na gharama zote za uendeshaji wa mradi huo zinasimamiwa na mgodi.
Serikali ya kijiji nayo haipo nyuma imetoa eneo la kijiji ekali 10 na kuwakabidhi vijana kwa ajili ya kilimo biashara cha mboga,Halmshauri ya wilaya ya Tarime imetoa watalamu wa kilimo ili kuwasaidia vijana katika shughuli yao ya kilimo biashara kwakuwa hawana elimu ya kilimo cha kisasa,wanawasaidia kuwapa elimu na utalaamu katika hatua zote zinazopaswa kufuatwa ikiwa ni pamoja na namna ya uaandaji bora wa shamba.
Ni majira ya saa tisa alasiri nawakuta vijana kijiji cha Matongo wakiwa shambani wakiandaa shamba kila kikundi kikiwa kwenye eneo lake wengine wakikusanya majani na baadhi wakichimba mtaro,tunazungumza na wanaeleza sababu mbalimbali za kuwepo shambani.
Katibu wa Jumuiya ya vikundi 10 vya wakulima wa kilimo biashara Rejina Joseph mkazi wa kitongoji cha Botanga katika kijiji hicho anasema kuwa wameamua kuwekeza kwenye kilimo biashara cha kisasa ili wajipatie fedha kupitia kilimo hicho.
"Nimejiunga na wenzangu ili nijikomboe kutoka kwenye umaskini,nipo kikundi cha Botanga chenye watu 10,tunaandaa shamba kupanda mbegu za mboga chainizi,sukuma wiki,nyanya na kabeji na mboga zingine,niwaombe wenzangu tusife moyo mafanikio yanapatikana baada ya jitihada"anasema.
Tito Wambura mwana kikundi Kegonga B anasema "Nimeona nijiunge na kilimo biashara baada ya kuona kuna mfadhili mgodi, nikaamini nyenzo zipo za kisasa sitatumia nguvu kubwa kwenye kilimo, ni kweli tumepewa vitendea kazi sisi kazi yetu ni kuandaa shamba na kusimamia, mambo mengine ya kitaalamu na fedha yanafanywa na mgodi na halmshauri"anasema Tito.
Tito anaongeza" Nafurahia kujiunga na hiki kilimo ingekuwa ni kujitegemea mwenyewe nisingekiweza lakini tumewezeshwa,hapa unaponiona sijatoa hata sh 100 kwenye hii shughuli ya kilimo biashara zaidi tu ya nguvu kazi ya mikono tupo kwenye maandalizi ya shamba.
"Wataalamu kotoka halmshauri kwa kushirikiana na mgodi walitupeleka mkoani Arusha kujifunza kwa wakulima wenzetu namna ya kuandaa shamba,upandaji hadi uvunaji namuomba mke wangu anivumilie napokuwa kazini"anasema.
Mwita Gibagiri mwana kikundi cha Kegonga B anasema kuwa ameamua kuwa mkulima kwa sababu kijiji chao kina umaskini na kina kabiliwa na changamoto ya mazao kusombwa na maji shambani wakati wa msimu wa mvua kwakuwa mashamba yao yamepakana na mto Mara, unapojaa maji uhama mkondo yanaingia kwenye mashamba na kuharibu mazao kitendo kinacho sababisha hasara na uhaba wa chakula.
"Ukifika kijijini utaona nyumba za kisasa zilizojengwa kwa kuezekwa kwa bati utasema hawa watu wana maisha mazuri,si kweli zile nyumba zilijengwa baada ya mgodi kuhamisha watu kwenye maeneo kupisha shughuli za mgodi, fedha walizopewa wakajengea nyumba na kiasi kilichobaki wakafanyia mahitaji na zikaisha sasa wana hali ngumu nyumba zimebaki mapambo tu"anasema Mwita.
William Makwahu ambaye ni mwana kikundi cha Kegonga A anasema" Mimi nina mke na watoto watano nina maisha magumu sana baada ya kusikia hii fursa ya kilimo biashara nikaamua nijiunge ili nijiinue kiuchumi ukizingatia vitendea kazi vya kilimo mgodi umebeba jukumu hilo kutusaidia nina shukuru sana mgodi kukikumbuka kijiji cha Matongo.
"Mgodi umefanya jambo la maana sisi huku kijijini vijana wengi hatujasoma imekuwa ngumu kupata kazi mgodini kwa sababu hatuna elimu hatujui kingereza,vijana walikaa bila kazi wakawa wanashawishika kuingia mgodini kuiba mawe ili wauze wapate pesa za matumizi,mgodi umekuja na ubunifu wa kilimo ambacho mtu yeyote anaweza kufanya hata kama hajasoma na akafanikiwa "anasema .
Kilimo Biashara ni shughuli ya kilimo inayohusisha matumizi bora ya elimu ya ujasiriamali katika kujipatia faida.Kilimo Biashara kina faida,kinatoa fursa ya mtu kujiajiri mwenyewe,pato la taifa hasa la ndani (GDP) kinasaidia kuleta pato la ndani kwa kulipa kodi kwa serikali,kukua kwa biashara ,malighafi zinazohitajika viwandani nyingi zinatoka kwenye kilimo,kupata chakula na kupunguza umaskini.
.........Itaendelea
Post a Comment