HEADER AD

HEADER AD

WATAKIWA KUTUMIA SIMU KUSOMA MACHAPISHO MAKTABA YA TET

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Leila Mohamed Mussa  akizungumza katika tukio hilo
 

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Leila Mohamed Mussa amewataka wazazi na wanafunzi kutumia simu zao kuingia katika Maktaba ya mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kusoma na kujifunza machapisho mbalimbali.

Waziri Leila amesema hayo tarehe 1,Octoba,2022 wakati wa makabidhiano ya nakala 4,400 za vitabu vya kidato cha kwanza hadi cha nne kwa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Mwanamke Intiative Foundation (MIF) na nakala 31, 100 za vitabu vya kidato cha Tano na Sita kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali vilivyotolewa na Serikali  kupitia Taasisi hiyo ya elimu yaliyofanyika katika Skuli ya Dkt.Hasnuu Makame iliyopo mkoa wa Kusini Unguja.
"Wazazi na wanafunzi hakuna elimu ya kuhadithiwa, elimu inapatikana katika vitabu tumieni simu zenu kuingia katika Maktaba mtandao ya TET mjipatie machapisho mbalimbali,mkavitumie na kuvitunza  vitabu hivi ili mpate elimu bora kwa Taifa" amesema Leila.

Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema TET imetoa vitabu hivyo vyenye thamani zaidi ya Tsh. Milioni 51 kwa ajili ya wanafunzi wa Kidato cha kwanza hadi cha nne  na nakala 31,100 za vitabu vya kidato cha 5 na 6 vyenye thamani ya Tsh.Milioni 329 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba akizungumza katika tukio hilo

Dkt.Komba ameishukuru MIF kwa kuja na wazo la kutokomeza sifuri (Zero) Unguja na kusema kuwa ni wazi wazo hilo linapaswa kuwa Tanzania nzima kwakuwa bado shule nyingi hazifanyi vizuri.

Amesema ,licha na kukabidhi nakala hizo, wanafunzi na walimu bado wana fursa ya kusoma machapisho mbalimbali katika maktaba mtandao ya TET na kwamba taasisi hiyo ipo tayari kutoa mafunzo kwa walimu wa mkoa wa Unguja ili waweze kupata ujuzi wa kumuandaa mhitimu aweze kujiajiri au kuajiriwa.

Mwenyekiti wa MIF Wanu Hafidhi Amiri ameishukuru TET kwa kukabidhi vitabu ambavyo vitasambazwa katika skuli 33 za mkoa wa Unguja kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Wanu amesema MIF ilifanya tafiti mbalimbali ili kubaini changamoto zinazosababisha wanafunzi wa mkoa wa Kusini Unguja kufeli, moja ya changamoto ni uhaba wa vitabu vya kujifunzia kwa wanafunzi,hivyo MIF ilichukua jukumu la kuomba TET kuwapatia vitabu vya kiada kwa shule za sekondari ambavyo vitasaidia kupunguza sifuri (zero) kwa wanafunzi hao.

Ameongeza kuwa malengo ya MIF ni  kusaidia wanafunzi wa Zanzibar kufaulu kidato cha Nne na kuiondoa Zanzibar katika shule 10 za mwisho Kitaifa katika matokeo ya kidato cha Nne.






No comments