KILIMO BIASHARA CHA MBOGA MATUMAINI MAPYA KWA VIJANA WA KIJIJINI - 3
Na Dinna Maningo,Tarime
KIJIJI cha Matongo Kata ya Matongo -Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kina ardhi yenye rutuba ya kustawisha mazao, hali ya hewa nzuri na vyanzo vya maji lakini bado wakulima hawajaitumia vyema fursa ya Kilimo Biashara-Mboga.
Kijiji hicho kina vijana ambao wengi wao hawakubahatika kupata elimu ikiwemo ya msingi na sekondari, baadhi yao ni wakulima na wafugaji wakiwa hawana ajira mbadala,wengine hawana kazi wala kujiajiri hivyo kuendelea kulandalanda kijijini.
Katika kujikwamua kiuchumi baadhi ya vijana wapatao 100 katika kijiji hicho wameamua kujiunga kupitia vikundi vya watu 10 kwa kila kikundi na kuanzisha kilimo biashara cha mboga.Serikali ya kijiji imewapatia ekari 10 kwa ajili ya uzalishaji wa mboga.
Shamba lililoandaliwa na wakulima
Halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia wataalamu wa idara ya kilimo wanatoa elimu kwa vijana hao kulima kitaalamu huku Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wao wakiwa ndio wafadhili wa fedha na wawezeshaji wa miundombinu yote ya mradi huo .
Sylvanus Gwiboha ni Afisa Kilimo Halmashauri ya wilaya ya Tarime anasema pamoja na fursa nzuri ya kilimo cha mboga bado wakulima hawajaitumia kikamilifu kwani uzalishaji uko chini na hivyo kutegemea mboga na matunda kutoka nje ya wilaya mfano Geita, Sengerema, Kiabakari, Bunda, Busega, Magu, Lamadi na Singida.
Kwanini Kilimo Biashara kilimwe Matongo?
Gwiboha anasema katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime kuna jumla ya ekari za kilimo 74,870 kati ya hizo ekari 62 ni za kilimo cha mboga, wakulima wanaojishughulisha na kilimo biashara ni 980,vikundi vinavyojishughulisha na kilimo biashara ni 23.
Anasema sababu ya kilimo biashara kulimwa Matongo ni kwakuwa kuna eneo linalofaa lenye rutuba ya kustawisha mazao,hali ya hewa nzuri (vuli na masika) pia joto la wastani 14°-20°c vyanzo vya maji katika mito,mfano mto Tigithe, mto Mara na nguvu kazi ipo.
"Kuanzisha mradi huu wa kilimo biashara ya mboga kwa Matongo kutatoa ushindani katika soko la Tarime na nchi jirani ya Kenya,soko lipo la uhakika wanajamii na wafanyakazi zaidi ya 3,000 wa mgodi, mpaka wa Sirari na nchi jirani ya Kenya hivyo kuanzisha mradi huu jamii itapata mapato pamoja na Halmashauri.
"Mpango wa mradi huu ni kulima ekari 10 za mboga kwa kuanzia, wanufaika ni vijana waliojiunga katika vikundi na kufanya kazi, idadi ya vijana ni 100, kila kikundi kikiwa na wakulima 10.
Gwiboha anasema mbali na kipato mradi umelenga kuboresha lishe kwa vijana pamoja na kaya zao, pia mradi utatoa ajira kwa vijana watakaofanya vibarua katika mnyororo wa thamani.
"Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mradi utatoa zana za umwagiliaji kwa matone katika utekelezaji, vijana watakuwa ni wawekezaji kutokana na miundombinu rahisi ya umwagiliaji maji kwa matone ambapo madumu yenye ujazo tofauti yatatumika" anasema.
Afisa kilimo anasema aina mbalimbali za mboga zitapandwa kulingana na uhitaji wa soko, vijana wataelekezwa na wataalamu namna ya uzalishaji ili wakati wote kuwe na mazao sokoni kusiwe na upungufu,na mafunzo ya stadi za maisha (cross cutting issues) yataendelea kutolewa.
Anasema vijana wamepata elimu iliyotolewa na wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mboga (TAHA) lenye makao makuu mkoani Arusha,mwezeshaji wa mradi ni mgodi wa Norrh Mara.
Gwiboha anasema tayari vijana wameshaandaa vitalu vya mbegu kwa ajili ya kupanda miche bora katika shamba kuu na kwamba mavuno mazuri huanzia maandalizi kwenye kitalu.
"Unaweza kuwa na mbegu bora lakini kama maandalizi ya kitalu sio mazuri utaishia kupata mavuno hafifu.Kauli mbiu inasema " Lima Mboga Uboreshe Lishe na Kipato cha Familia/Kaya". Kuna fursa kubwa katika kilimo cha mboga,vijana wachangamkie fursa mavuno utapata baada ya miezi mitatu au minne tangu ulipopanda"anasema Gwiboha
Gwiboha anasema kilimo cha mboga Tanzania kinakua kwa 7% ikilinganishwa na kilimo cha mazao mengine yanayokua kwa 3 - 4% kwa mwaka.
Afisa Kilimo Halmashauri ya wilaya ya Tarimea Sylvanus Gwiboha akiwa katika shamba moja la nyanya
Anasema sekta hiyo mbali na kukua kwa kasi kimeajiri takribani watanzania Milioni 6.5, Tanzania ni mojawapo katika nchi 20 bora duniani inayozalisha mboga (FAOSTAT DATA) .
"Mboga zinachangia 38% ya fedha za kigeni katika kilimo yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika kilimo cha mboga, shambani wakati wa uzalishaji,sokoni -kuuza mboga, kutengeneza juice au kutengeneza vifuangashio,kuwekeza katika kituo cha uchambuzi wa mboga,kupeleka sokoni ndani na nje ya nchi na kufungua duka la kuuza pembejeo.
Mgodi wa North Mara wawahakikishia vijana soko la uhakika.
Mgodi wa North Mara umekuwa ukichangia maendeleo katika vijiji vinavyouzunguka ikiwa ni pamoja na kuviwezesha fedha vikundi,ujenzi wa miradi kama ukarabati wa shule,ujenzi wa vituo vya afya ,ujenzi wa ofisi ya kata,matengenezo ya barabara.
Meneja Mahusiano ya Kijamii wa Mgodi wa North Mara Gilbert Mworia anasema kuwa mradi huo wa kilimo cha mboga katika kijiji cha Matongo ni wa majaribio na kwamba lengo la kuwezesha vijana ni kuongeza fursa za kujikwamua kiuchumi na kujipatia ajira badala ya kuingia mgodini.
Mnufaika wa mradi wa kilimo biashara akiwa na Meneja Mahusiano wa Mgodi Gilbert Mworia (kulia) na Meneja Msaidizi wa Mgodi (katikati) wakiwa shambani.
Anawahakikishia vijana kuwa soko la kuuza mboga lipo,mgodi utakuwa mnunuzi mkuu wa mboga na unafanya hivyo ili kuongeza mzunguko wa fedha kwenye maeneo ya mgodi hivyo watumie fursa hiyo ili fedha ya mgodi isiende nje ya Tarime.
"Wasiwe na wasiwasi soko lipo sisi mgodi ndio tutakuwa wanunuzi wa kwanza,najua kuna wafanyakazi wa Mgodi wanaoishi nje ya mgodi nao watanunua mboga,lengo letu pesa izunguke hukuhuku isiende nje.
"Nawaomba vijana watumie fursa hii ya kilimo biashara cha mboga ili fedha isiende nje,tumekuwa tukinunua bidhaa nje ya hapa ,ila kwa huu mradi mboga tutanunua hapahapa kijijini Matongo"anasema Mworia.
Anasema mgodi unasaidia uwezeshaji wa mazao katika kilimo hicho, umwagiliaji wa matone,kupulizia dawa na miundombinu mbalimbali inayohusiana na kilimo na kwamba mbegu zitakazotumika ni za kisasa na uzalishaji utakuwa mkubwa kwakuwa watatafutiwa soko kutoka nje ya Tarime.
"Ni mradi wa majaribio tumeanza na vijana 100 ,serikali ya kijiji imetoa eneo ekari 10, halmashauri wao wanawezesha utaalamu,kwa sasa tupo kwenye hatua za mwanzo za maandalizi ya shamba kwa kutumia Teknolojia,fursa ya masoko ipo mgodi utanunua mboga,kuna kampuni ya AKO watanunua na tutatafuta masoko na maeneo mengine.
"Zitatumika mbegu bora za kisasa kuhakikisha uzalishaji unakuwa wa tija,tunashirikiana na Chama cha Mboga Tanzania (TAHA )wao nao wana uelewa wa masoko,tulishawapeleka wataalamu kwenye mafunzo TAHA na Dayosisi ya KKKT mkoani Arusha.
Meneja anasema "Tuliwapeleka wanakikundi wakaenda kujifunza walikaa Arusha siku nne maana yale mafunzo ni mageni kwao inahitaji nguvu ili kuifanya, wapo watu tuliowapeleka kwenye maonesho ya nanenane Nyakabindi -Simiyu" anasema Meneja huyo.
Meneja anasema mradi huo ni kitu kigeni kwa wanakijiji ambao hawakuuzoea hivyo itawachukua muda kuelewa lakini tayali wameanza kupata mwanga. Anasema lazima wanakikundi wausimamie mradi wao wazalishe mboga kwa wingi wawe na nia na imani.
Mwaka 2017 Mgodi huo ulitoa taarifa ya miradi ya Jamii kwa mwaka 2017 na mipango ya mwaka 2018 iliyoandaliwa na ofisi za Jamii endelevu Mgodi wa North Mara,iliyosomwa kwenye maonesho ya wiki ya mahusiano na ujasiriamali ikiwa na kauli mbiu "Kilimo Bora na Maendeleo ya Viwanda 2018",ilielezwa kuwa mgodi utaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza uchumi wa wajasiriamali .
Taarifa hiyo inasema kuwa kilimo bora kinawezesha chakula,mapato ya kifedha kwa ajili ya mahitaji ya kila siku,malighafi kwa ajili ya viwanda ambapo viwanda vinasaidia kuongeza thamani ya mazao au malighafi ya shamba na kumpatia mkulima kipato kwa ajili ya mahitaji yake pamoja na kuboresha kiwango cha maisha baada ya kukuza kipato.
Imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa katika miradi ya maendeleo haikufanyika vizuri ambapo kulikuwa na miradi 24 lakini hadi kufikia mwaka huo miradi 10 haipo hai, changamoto ikitajwa kuwa ni kutokuwepo kwa uaminifu katika kutumia pesa kadri ya mipango,ukosefu wa utaalamu wa uendeshaji miradi na udhaifu katika kufuatilia maendeleo ya miradi.
Taarifa inasema kutokana na changamoto hizo Mgodi wa North Mara ukaahidi kuandaa utaratibu mpya wa namna ya kuboresha usimamizi wa miradi watakayoianzisha na kuwashirikisha wadau wengine kama serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia katika kuboresha utendaji wa miradi yao ambapo katika mwaka huo wa 2017 gharama ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo ilikuwa Tsh. Bilioni moja.
Katika Mpango wa mwaka 2018 Mgodi wa North Mara ukaeleza kunuia kuwekeza nguvu zake za kusaidia jamii katika kujipatia kipato kwa shughuli endelevu hata baada ya maisha au uhai wa mgodi ambapo mpango huo ulizingatia mpango mkakati wa wilaya ya Tarime kwa mwaka 2018.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mgodi utajikita kwenye kilimo bora kwa ajili ya uzalishaji wa mazao/chakula cha ziada kutokana na mauzo.
Utafiti wa Mgodi katika taarifa hiyo ukashauri kuwa,mazao kama mahindi,mchele,alizeti pamoja na mbogamboga ni chanzo bora cha pato na utekelezaji wa adhima hiyo utaanza kwanza kwa kushirikisha wadau serikali za vijiji,serikali ya wilaya kuangalia namna na mbinu za utekelezaji kwa mafanikio.
Pia ikaelezwa kuwa mgodi utawekeza nguvu katika kuimarisha viwanda vidogovidogo ambavyo vipo na ambavyo vitahitaji kuanzishwa na wadau watahusishwa katika kutekeleza lengo hilo.
Mwenyekiti Kijiji cha Matongo Daud Itembe
Post a Comment