HEADER AD

HEADER AD

PROF.MKENDA AMESEMA HAJARIDHISHWA NA UJENZI WA VETA SIMIYU


 
Na Annastazia Paul,Simiyu

WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema hajaridhishwa na ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Simiyu unaojengwa kwa gharama zaidi ya Tsh. Bilioni tano baada ya kukagua na kuona mapungufu yakiwemo ya udogo wa vyumba vya kulala wanafunzi (Mabweni).

Waziri Mkenda amewaagiza wataalamu katika Chuo cha Ufundi cha Arusha ambao ndio wasimamizi wa ujenzi kufika chuoni hapo kukagua na kuona palipo na kasoro zifanyiwe marekebisho.


Akizungumza wakati akikagua ujenzi wa VETA Octoba,8,2022 ameagiza hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa. 

"Nakiagiza chuo cha ufundi cha Arusha ndio wanaohusika na ujenzi na kusimamia kazi hii kupitia FDC, walete wataalamu wao wote waje hapa wakague, kuna baadhi ya vitu ambavyo wanatakiwa kuviangalia.


"Mimi si mtaalamu kuna mengine nimeyaona nadhani hayafikii viwango vinavyotakiwa, mfano ile sehemu ya kuingiza magari kwa ajili ya ukaguzi wa magari ujenzi wake haukidhi viwango vinavyotakiwa, nimeangalia mabweni ni madogo mno kwa watu wanne kulala mle ndani"alisema Prof.Mkenda.

Prof. Mkenda alisema anapenda kuona chuo cha  ufundi Arusha kikisimamia kazi vizuri ili watu wengine binafsi wakitafute kwenda kusimamia ujenzi lakini kwa ukaguzi alioufanya amebaini ujenzi haujafikia kiwango kinachotakiwa.


"Wamejitahidi lakini hawajafikia kiwango kinachotakiwa, kwahiyo ni bora niseme siridhiki ningependa nione kazi nzuri, sasa nataka usimamizi wa kazi asikabidhiwe mtu mmoja tu, waje kama menejimenti ya chuo na wataalamu wao wapitie waone mapungufu.

"Kwasababu mie mwenyewe jicho langu haliwezi kuwa na utaalamu wa kutosha, vile vilivyokosewa waviandike ili tusije tukarudia makosa sehemu nyingine, na waoneshe kama kweli wanafahamu kwamba hapa kuna makosa." alisema Prof. Mkenda.


Waziri Mkenda alisema serikali ina mpango wa kujenga vyuo vya ufundi stadi kila wilaya na kusisitiza uwepo wa usimamizi mzuri ili kufanikisha mpango huo.

"Tukitoka hapa tutakwenda Geita kuangalia kazi inavyokwenda tutapita na sehemu nyingine, tunatumia force account tutakwenda wizarani tuangalie namna ya kugawa zile kazi, nyingine tuwape wakandarasi,kwa usimamizi huu haitawezekana sisi kusimamia wilaya 64 ujenzi wa VETA tusidanganyane.

"Tujaribu kuona ni kiasi gani tunaweza kuziruhusu zikaenda kwa wakandarasi na nyingine zitakwenda kwenye force account kwasababu hatuwezi kupewa Bilioni 100 alafu tusizimalize mwaka huu." alisema Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameagiza kukamilika haraka ujenzi ili chuo kianze kutumika kwakuwa ujenzi huo mpaka sasa upo nje ya muda kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kuanza mradi.


Ujenzi huo utagharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 5 hadi kukamilika ukihusisha majengo 25 ambayo ni pamoja na  karakana ,maktaba , jengo la utawala , stoo, sehemu ya chakula ,mabweni manne na  nyumba tano za watumishi.


Mshauri elekezi kutoka chuo cha ujenzi Arusha Mhandisi Jalalya Mabojano alisema watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na serikali ili kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo katika ubora unaotakiwa.


          Mhandisi Jalalya Mabojano

"Tumepokea maelekezo aliyoyatoa Waziri, mapungufu yote aliyoyaelekeza tunaahidi tutayafanyia kazi, tunakiri mapungufu yapo kwa sababu ya presha ya mradi wenyewe ulivyokuwa lakini yote yapo ndani ya uwezo wetu yale ambayo tunaweza kuyarekebisha tutarekebisha kwa wakati kabla hatujakabidhi mradi." alisema Mhandisi Mabojano.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange alieleza kwamba chuo hicho kikikamilika kitakuwa mkombozi kwa wananchi wa Bariadi na maeneo mengine na kitawasaidia mabinti kuepuka ndoa katika umri mdogo.

"Sisi mkoa huu ni wa wafugaji na unajua familia za kifugaji maisha ya watoto hasa mabinti wanakuwa katika hatari ya kuozeshwa mapema, kwa hiyo chuo hiki kitasaidia,tunamshukuru sana Rais maana kitakuwa ndio mkombozi wetu." amesema Kapange.


>>>Machi, 2022 Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga alifika kukagua ujenzi wa chuo hicho ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Mradi huo,Bazil Gibson alisema ujenzi  wa chuo katika awamu ya kwanza yanajengwa majengo 25.

Ujenzi huo ulianza Februari,2022 na utagharimu jumla ya Tsh. Bilioni 5.1 hadi kukamilika,chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja ambapo kati yao 320 watakuwa bweni na wengine 180 wa kutwa.

Ujenzi huo ulipaswa kukamilika Mei,2022,bado ujenzi unaendelea unatakiwa kukamilika Novemba,2022.






 Aliyesimama katikati ni Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda

No comments