SIMIYU KULIMA EKARI MILIONI 1.3 ZA MAZAO
Na Annastazia Paul,Simiyu
MKOA wa Simiyu katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2022/2023 umejipanga kulima ekari Milioni 1.3 za mazao mbalimbali huku ukiwa na matarajio ya kuvuna tani 1, 900,085.
Pia una mpango wa kuzalisha zaidi ya asilimia 70 ya pamba yote nchini, kutokana na mikakati uliojiwekea katika kilimo cha zao hilo ambapo kwa kuanza utekelezaji wa mpango huo umejipanga kuzalisha asilimia 61 ya pamba yote nchini.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda katika kikao kazi kilichowakutanisha maafisa ugani, watendaji wa kata, mitaa na vijiji, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wakuu wa idara mbalimbali mkoani humo huku akisisitiza kuwa mkoa ukiweka mikakati madhubuti utafikia malengo hayo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda
Ameongeza kuwa asilimia 50 ya pamba yote ambayo inazalishwa Tanzania inatoka katika mkoa wa Simiyu na wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi asilimia 61 kwa mwaka huu huku lengo lao likiwa asilimia 72 ya pamba yote nchini itoke katika mkoa huo.
"Maafisa ugani wenzangu tuna kazi kubwa sana ya kuhakikisha tunaweka malengo zaidi ya asilimia 72 ya pamba yote ambayo inataka kuzalishwa ndani ya nchi itoke katika mkoa wetu wa Simiyu.” Amesema Nawanda.
Afisa kutoka ofisi kuu ya Bodi ya Pamba Tanzania Renatus Luneja amesema bodi ya pamba inautazama mkoa wa Simiyu kama mkoa wa kipaumbele kwa kila namna katika uzalishaji wa zao la pamba, hivyo bodi iko tayari kutoa mahitaji yoyote yanayohitajika kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji wa zao hilo la pamba.
"Tupende kukuhakikishia mkuu wa mkoa na timu yako hapa, wakati wowote, shughuli yoyote inayohusiana na zao la pamba bodi ya pamba iko tayari kutoa lolote linalohitajika ikiwa ni pamoja na utaalamu, rasilimali zinazoweza kusaidia kuendeleza zao, pembejeo na mambo yote ya msingi bodi ya pamba ina kuhakikishia kwamba vitapatikana kwa wakati.” amesema Renatus.
Mmoja wa watendaji ambao wameshiriki kikao kazi hicho Sabina Wilson amesema kuwa watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mkuu wa mkoa kutimiza malengo yaliyowekwa ili kuongeza uzalishaji wa zao la pamba katika mkoa huo.
“Tumepokea maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa mkoa tunakwenda kuwaelimisha wakulima wajisajili ili wapate mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali, lakini pia tutaenda kuwaelimisha wafuate kanuni bora za kilimo ili uzalishaji uwe wenye tija katika mazao yao wanayolima.” amesema Sabina.
Post a Comment