WATOTO 66 WAFARIKI ,TMDA YATOA TAHADHARI
Na Andrew Chale,Dar es Salaam.
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limenukuliwa kuwa, inasadikika watoto takribani 66 Nchini Gambia wamefariki dunia kufuatia matumizi ya dawa zenye viambata vinavyosababisha madhara ya kiafya pamoja na vifo kwa watumiaji (hasa watoto).
Dawa hizo ni pamoja na Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup.
Kufuatia hali hiyo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imetoa taarifa kwa Umma juu ya uwepo wa dawa hizo kufuatia kupokea ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo kwenda kwa Umma, imeeleza kuwa, dawa hizo zote zinatengenezwa na kiwanda chenye jina Maiden Pharmaceuticals Limited kilichoko nchini India.
"Dawa hizi zimepimwa na kukutwa na viambata vijulikanavyo kama diethylene glycol na ethylene glycol,viambata hivi husababisha madhara na hata vifo kwa watumiaji"Imeeleza taarifa hiyo.
Dawa zenye Kiambato hai :Promethazine, Pheniramine Maleate, Ammonium chloride, Menthol Chlorphenamine Maleate,
Phenylephrine HBR,
Dextromethorphan syrup
Paracetamol Phenylephrine HCL,
Chlorphenamine Maleate"
Dawa hizo zenye toleo namba ML21-202, ML21-199,ML21-203, ML21-198 ambapo zikiwa na tarehe ya kutengenezwa ya Desemba 21 (Dec-21) huku ikiwa na mwisho wa matumizi Novemba 24 (Nov-24).na lugha ya bidhaa ni Kiingereza.
TMDA inapenda kuuhakikishia umma wa watanzania kwamba dawa hizi zote haziko kwenye soko hapa nchini na hazijawahi kusajiliwa ili kutumika .
"Hata hivyo,Mamlaka inaendelea kuchukua tahadhari zote kupitia mifumo yake ya udhibiti ili kubaini endapo dawa hizi zitafika nchini kwetu." amesema Adam Fimbo.
Ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwenye Ofisi za TMDA zilizopo karibu, Ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya au Vituo vya Polisi endapo yeyote atabaini kuziona mahali popote ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
"Kwa maelezo zaidi wasiliana na Ofisi za TMDA Makao Makuu au Ofisi za Kanda zilizoko Mwanza, Geita, Arusha, Mbeya, Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara na Tabora au kupiga simu bila malipo kupitia Na.0800110084" amesema Adam Fimbo.
Post a Comment