TET KUUNGANA NA SEKTA BINAFSI KUKUZA USOMAJI WA VITABU
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesema itaendelea kuungana na sekta binafsi katika kuhakikisha usomaji wa vitabu unakua kwa kiasi kikubwa nchini na kusisitiza kuwa,usomaji wa vitabu vyote wa kiada na ziada kwa mwanafunzi unajenga Taifa lenye maarifa.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt.Aneth Komba katika Tamasha la 31 la kimataifa la vitabu Tanzania lililozinduliwa Okotoba 11,2022 litakaloendelea hadi Oktoba 15, kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama Dar es Salaam,lililowashirikisha wachapishaji mbalimbali wa vitabu nchini.
"Tunasisitiza usomaji wa vitabu vyote kwa kila mwanafunzi vya kiada na ziada,anapojisomea vitabu tunajenga Taifa lenye maarifa katika kujenga nchi yetu, tutaendelea kuhimiza ari ya usomaji wa vitabu, tusome vitabu vyote kwa ajili ya kupata maarifa’’amesema Dkt.Komba.
Mgeni rasmi katika maonesho hayo Prof Evaristo Liwa aliyemwakilisha Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia amesema maonesho hayo ni muhimu kwani vitabu ni nyezo muhimu katika suala la ufudishaji na ujifunzaji na kusema kuwa serikali itaendelea kuhamasisha jitihada za usomaji nchini .
Prof.Liwa amesema usomaji wa vitabu unatoa ufahamu na uelewa wenye kutoa maarifa ambayo yanaishi,amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutambua umuhimu wa uchapishaji nchini .
‘’Usomaji wa vitabu ni jambo muhimu sana nchini hivyo tamasha hili ninaamini litasaidia katika kuendelea kuhamasisha usomaji wa vitabu kwa lengo la kupata maarifa " amesema Prof. Liwa.
Ameongeza kuwa, kwa sasa Wizara iko kwenye mchakato wa maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala na baada ya maboresho hayo itaaandaliwa uandishi wa vitabu itakayofanyika kwa ushirikiano wa serikali na waandishi binafsi vitakavyotumika katika shule nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Nchini(PATA) Gabriel Kitua amesema tamasha hilo litasaidia katika uhimizaji wa usomaji wa vitabu nchini na kwamba kupitia vitabu masuala muhimu kama maadili yanapatikana na kuwa na ufahamu mkubwa katika usomaji wa vitabu.
Tamasha hilo limewakutanisha wachapishaji mbalimbali na wananchi wa kawaida ambao watapata nafasi ya kusoma vitabu mbalimbali vinaoneshwa kwenye maonesho hayo.
Post a Comment