JESHI LA ZIMAMOTO LACHUNGUZA MADUKA MATATU YALIYOTEKETEA
Na Alodia Dominick, Bukoba.
JESHI la Zimamoto na uokoaji linaendelea na uchunguzi wa maduka matatu yaliyoteketea kwa moto yaliyoko mtaa wa Guinea kata ya Miembeni Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ili kubaini chanzo cha moto huo.
Jengo hilo lililoungua ni mali ya Badiru Kichwabuta ambapo moto ulizuka majira ya saa mbili za usiku Oktoba 31, 2022, bado kiasi cha vitu vilivyoteketea hakijafahamika na kwamba jeshi hilo linaendelea kufuatilia kujua hasara iliyotokea.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera Zabrone Muhumha amesema kupitia namba yao ya dharula 114 walipata taarifa ya moto huo na hivyo kuchukua hatua haraka kufika eneo la tukio na kuanza kudhibiti moto huo kwa kutumia magari yao ya zimamoto.
"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kupitia namba yetu ya dharula 114 tulifika eneo la tukio na kuanza kuudhibiti moto na hatimaye tulifanikuwa kuuzima kabla haujashika nyumba jirani," amesema Muhumha
Ofisa uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Kagera Samweli Mandali amesema baada ya moto huo kutokea walichukua hatua za kukata umeme ili kama umetokana na shoti ya umeme usiweze kuleta madhara makubwa.
Mmoja wa mashuhuda Jamal Ramadhani amesema, Majira ya usiku alishuhudia moto mkubwa ukiwaka kutokea kwenye duka moja linalouza magodoro na baada ya muda mfupi magari ya zimamoto yalifika na kuanza kuuzima ingawa jengo hilo lilikuwa limeishaanza kuteketea.
Niclous Basmaki shuhuda wa tukio hilo amelishukuru jeshi la zimamoto na uhokoaji kwa kuweza kudhibiti moto huo usiweze kusambaa na kuleta madhara makubwa.
Mbali na maduka hayo kuteketea kwa moto hakuna majeruhi wala kifo kilichosababishwa na moto huo.
Post a Comment