WAENDESHA BAISKELI TWENDE BUTIAMA WAPANDA MITI KUMUENZI HAYATI NYERERE
Na Jovina Massano,Musoma
WAENDESHA Baiskeli wa Tendwe Butiama wamepanda miti katika shule ya msingi Nyerere iliyopo wilaya ya Bunda mkoa wa Mara kwa lengo la kuhifadhi mazingira kwa kumuenzi kwa vitendo Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Juliusi Nyerere.
Pia wametembelea Hifadhi ya Serengeti,eneo kulikojengwa ofisi ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) Kanda ya Magharibi na kupanda miti, wamesema Hayati Nyerere alikuwa ni mhifadhi wa mazingira na alipinga adui mkuu wa maendeleo ambae ni ujinga umaskini na maradhi.
Mwenyekiti na mkuu wa msafara wa Twende Butiama Gabriel Landa amesema lengo la kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Butiama mkoani Mara ni kumuenzi kwa vitendo baba wa Taifa kwa kuhifadhi Mazingira na kuhamasisha uchangiaji wa pesa kwa ajili ya kutengeneza madawati.
"Tunapanda miti na kuhamasisha uchangiaji wa pesa kwa ajili ya kutengeneza madawati ambayo huwa tunayakabidhi katika shule zenye uhitaji, utaratibu huu tulianza mwaka jana tuligawa madawati kwa shule tatu Wilayani Butiama, mwaka huu pia tumefanikiwa kugawa katika shule tatu mikoa ya Pwani,Morogoro na Dodoma tunaendelea kupokea michango ya Madawati na tutaipeleka kwenye Shule zenye uhitaji.
"Nawashukuru sana wananchi pamoja na viongozi wa serikali wa mkoa wa Mara,mapokezi yalikuwa ni makubwa hatukutegemea tulianza kutembelea shule ya msingi Nyerere iliyopo wilayani Bunda na mwaka jana tuliitembelea tukapanda miti ambayo imekua yote ina afya nzuri" amesema Landa.
Landa amesema msafara wa Twende Butiama una jumla ya washiriki 48 kati yao wanaume ni 43 na wanawake 5,ulioanzia Msasani -Dar es Salaam nyumbani kwa Hayati Nyerere,ulianza October 2 mwaka huu wenye km 1500 hadi kufika Butiama.
Afisa Mwandamizi kutoka Hifadhi za Taifa (TANAPA) Kanda ya Magharibi Godfrey Kitundu ameushukuru msafara huo kwa kupanda miti kwa kuweka alama lakini pia katika kutekeleza uhifadhi kwa vitendo,amewaomba kuendeleza uhifadhi kwa kurithisha vizazi vya sasa na vya baadae.
"Nashukuru kwa kumuenzi baba wa Taifa kwa kupanda miti na kutekeleza dhana ya uhifadhi kwa vitendo na kwa mahusiano mliyoyaweka kwetu hasa kwa kufanya pia kutangaza Utalii wa ndani kwa Watanzania " amesema Kitundu.
Mkurugenzi wa Twende kutalii Albert Benadicto Chenza ameupongeza msafara wa Twende Butiama kwa kushiriki na kupunguza changamoto za madawati katika sekta ya elimu lakini pia kutangaza Utalii wa ndani na kuibua hisia mbalimbali za baba wa Taifa kwa Watanzania za kumuenzi .
Mkurugenzi wa Twende kutalii Albert Chenza akiendesha baiskeli mbele ya gari
"Kwa kutambua uhifadhi alioufanya baba wa Taifa msafara umeweza kufika katika pori la akiba la Kijereshi na wamefanikiwa kuingia katika mbuga ya Serengeti na kufanya utalii wa ndani kuhamasisha watanzania katika Utalii na kuongeza uchumi wa Taifa letu,"amesema Chenza.
>>>Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni Rais wa kwanza Nchini Tanzania,alizaliwa 13,Aprili 1922 wilaya ya Butiama,alifariki 14,Oktoba,1999 akiwa na umri wa miaka 77.
Post a Comment