HEADER AD

HEADER AD

AGREY MWANRY : WAKULIMA TUMIENI MVUA ZA MWANZO KUPANDA PAMBA



Na Mwandishi Wetu, Simiyu

WAKULIMA wa zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu wametakiwa kuwa na desturi ya kuandaa mashamba yao mapema sambamba na kutumia mvua za mwanzo kupanda ili waweze kupata tija ya zao hilo pamoja na wadudu waharibifu.

Ili kufikia uzalishaji wenye tija katika zao la zao la pamba, wataalam wa kilimo wametakiwa kuwasisitiza wakulima kuandaa shamba mapema na kutumia mvua za mwanzo kupanda kwa lengo la kukabiliana na baadhi ya wadudu wasumbufu wa zao hilo.

Rai hiyo imetolewa na Balozi wa pamba hapa nchini Agrey Mwanry Novemba, 26, 2022 wakati akihamasisha matumizi ya teknolojia katika zao la pamba Wilaya ya Busega katika mkoa huo. 

Balozi Mwanry amesema kuwa wakulima wengi wamekuwa wakitumia mvua za mwanzo kuandaa mashamba badala ya kutumia kupandia hali inayopelekea mazao yao kuharibiwa hivyo kushindwa kunufaika na zao hilo.


Amesema pindi wanapochelewa kupanda mazao yao huharibiwa kwa urahisi na wadudu wasumbufu aina ya kiyenze pamoja na mchwa ambao wametajwa kuwa waharibifu zaidi na kusisitiza kuwa njia pekee ya kuepukana na wadudu hao ni kupanda mapema.

"Wakulima wengi wamekuwa wakitoa malalamiko mengi mara kwa mara wakidai dawa haziui wadudu waharibifu wa zao hilo kumbe chanzo ni kuchelewa kupanda hali ambayo hupelekea  vinyenze na mchwa ambao ni waharibifu zaidi na huwa hawasikii dawa" amesema Balozi Mwanry

Ameongeza kuwa, mbali na changamoto hizo kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kwenye zao hilo ikiwemo wakulima kupanda kwa kutumia kamba(vifaa maalum vya kupandia) badala ya kurusha mbengu na kuongeza kuwa katika Mikoa 17 inayolima zao la pamba Mkoa wa Simiyu unaongoza kwa mapato yatokanayo na zao hilo.


Mkaguzi wa zao la pamba katika wilaya ya Busega Hamis Jamvi amesema mlipuko wa ugonjwa wa mnyauko na wakulima kutotambua visumbufu ni miongoni mwa changamoto zilizoathiri uzalishaji wa zao hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Busega Gabriel Zakaria, amesema pamoja na mapokeo chanya ya wakulima kuhusu kulima kisasa wamekuwa wakikabiliana na  changamoto ya kufikiwa na huduma za ugani na pembejeo kwa wakati.

Zakaria ameongeza kuwa wakulima wengi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kulima zao hilo kutokana na ongezeko la bei ya pamba ya msimu uliopita hali iliyopelekea kuona fahari ya kulima pamba ambapo wamenufaika na jasho lao tofauti na nyuma walikuwa wakitumia gharama nyingi lakini hawapati tija.

Katika hatua nyingine Zakaria amewaonya watendaji wasio kuwa waaminifu wenye tabia ya kuhujumu pembejeo za kilimo, kuwa hatosita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika .

Kwa msimu 2022/23 Wilaya ya Busega imeweka lengo la kulima ekali 95,000 sawa hekta 38.4.
     


No comments