JESHI LA POLISI TARIME RORYA LINAVYOPAMBANA KUDHIBITI UHALIFU
Na Dinna Maningo, Tarime
JESHI la Polisi lipo kwa lengo la kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao, kudumisha amani na utulivu katika jamii, pia kuzuia, kubaini na kupambana na uhalifu.
Katika mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Jeshi la Polisi limekuwa na mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza na kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyosababisha kutokuwepo amani ya kutosha.
Kabla ya kuanzishwa mkoa huo wa Polisi matukio mbalimbali ya uhalifu yalikithiri yakiwemo ya wizi wa mifugo, migogoro ya ardhi na mipaka, mapigano ya koo yaliyodumu kwa muda mrefu.
Matukio hayo ya uhalifu yalisababisha kuvunjika kwa amani na kuongeza hofu na mashaka juu ya usalama wa raia kutokana na kujitokeza mara kwa mara yaliyosababisha jamii ya kabila la wakurya kupigana wao kwa wao pamoja na mapigano ya kabila hilo na kabila la Wajaluo .
Kuibiana mifugo kulisababisha umwagaji damu huku wengine wakisalia kupata ulemavu wa maisha pamoja na uharibifu wa mazao.
Hali hiyo ilirudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwani mapigano yalipotokea familia zilikimbia nyumba zao kwa kuhofia kuuwawa kwakuwa koo moja ilipovamia koo nyingine waliuwa familia mbalimbali wakiwemo watoto na wajawazito huku nyumba zao zikochomwa moto.
Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2011 zilizotolewa wakati wa madhimisho ya siku ya "Police Day" Mapigano ya koo yalitokea kati ya koo ya Wahunyaga na Wasweta mwaka 2008, Warenchoka na Wanchari ( 2008), Wanchari na Wakira (2008), Wamera na Wajaluo (2009) pamoja na Wanyabasi na Wairegi (2009).
Jumla ya watu 52 waliuwawa na wengine 91 walijeruhiwa na nyumba zipatazo 519 zilichomwa moto, ekali 49 za mazao ya chakula ziliharibiwa na kusababisha kutokea njaa katika vita hivyo vya koo mwaka 2008-2009.
Mapigano ya koo yalichochea wizi wa mifugo kwani mwaka 2008-2009 zaidi ya ng'ombe 1,630 waliporwa kati ya hao ng'ombe 580 tu ndio waliokolewa wakati wa mapigano hayo, huku silaha 2 shotgun moja na pisto moja kutoka kwa wamiliki zilikamatwa.
Mapigano ya koo, wizi wa mifugo, unyang'anyi wa kutumia silaha ulioambatana na mauwaji pamoja na kilimo cha bangi yaliathiri jamii.
Mwaka 2009, Serikali ikalazimika kuanzisha mkoa wa Polisi Tarime Rorya uliotangazwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo Lawrence Masha (Mb) kupitia gazeti la Serikali, No. 28/2009, hivyo kuunganishwa kwa wilaya mbili za kiserikali Tarime na Rorya kuwa mkoa wa Polisi makao yake makuu kuwa Tarime.
Kuanzishwa kwa mkoa wa polisi kulienda sambamba na kuundwa kwa wilaya sita za Polisi ambazo ni Tarime, Nyamwaga, Rorya, Sirari, Kinesi na Shirati.
Sababu ya kuundwa wilaya hizo ni kukithiri vitendo vya uhalifu. Hadi mwaka 2011 mkoa huo wa Polisi ulikuwa na jumla ya askari 610 wakiwemo maafisa ukaguzi, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.
Ushirikiano wa wananchi kupitia mpango wa polisi jamii/ulinzi shirikishi umepelekea kupata taarifa mbalimbali za uhalifu na kuzifanyia kazi mapema.
Tangu kuanzishwa kwa mkoa huo matukio ya uhalifu yamekuwa yakizidi kupungua huku jeshi la polisi usiku na mchana limekuwa likiendelea kuimalisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao, kudumisha amani na utulivu katika jamii, pia kuzuia, kubaini na kupambana na uhalifu.
Ushirikiano wa jeshi la polisi na wadau mbalimbali wa amani umekuwa ni mchango mkubwa sana katika kurejesha amani, usalama na utulivu, baadhi ya watu huwafichua wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
ACP Geofrey Sarakikya ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya anaeleza mafanikio mbalimbali katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika kipindi cha Mwezi Julai 01, hadi Octoba, 31, 2022.
Kamanda huyo wa polisi anasema jeshi hilo limekuwa likiendelea kuimalisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao kutokana na misako na operesheni mbalimbali zilizofanyika katika wilaya zote za Polisi.
Pia anasema mafanikio yamepatikana ya kesi zilizofikishwa mahakamani kama vile uhujumu uchumi, wizi wa mifugo, mauwaji na unyang'anyi wa kutumia silaha.
Kupatikana na silaha, risasi
Kamanda ACP Sarakikya anasema jumla ya silaha 02 zilikamatwa, moja ikiwa ni bastola aina ya Pietro Berretta yenye Na. za usajili TZ CAR 76091 Pisto na Shortgun isiyokuwa na namba iliyokuwa imekatwa mtutu pamoja na risasi 82 za AK 47.
Kupatikana na Pombe ya Moshi
Anasema jumla ya watuhumiwa 236 wamekamatwa wakiwa na lita 2,370 za pombe haramu ya moshi (Gongo).
Kupatikana Dawa za Kulevya
Anasema watuhumiwa 35 wamekamatwa wakiwa na Kilogramu 4,241 za bangi pamoja na pikipiki 09 na gari moja zilizokuwa zinatumika kusafirishia bangi na watuhumiwa 03 wamekamatwa wakiwa na mashamba Ekari 9.5 yaliyolimwa bangi ambayo yaliteketezwa moto na wamefikishwa mahakamani, watuhumiwa 06 wamekamatwa na kilo 80 za mirungi.
Wizi wa Mifugo
Kamanda Sarakikya anasema watuhumiwa 28 wanaojihusisha na wizi wa mifugo wamekamatwa na 20 kati yao wameshafikishwa mahakamani waliobakia upelelezi bado unaendelea watafikishwa wakati wowote.
Watuhumiwa sugu
Anasema kuanzia Julai hadi Octoba, 2022 watuhumiwa sugu 69 wanaojihusisha na wizi wa pikipiki, unyang'anyi wa kutumia silaha, uvunjifu na wizi wamekamatwa pamoja na pikipiki 04. Pikipiki hizo zimeibwa kutoka maeneo mbalimbali ya Tarime Rorya na kwenda kuziuza katika mkoa wa wa Geita, Mara, Mwanza na Simiyu.
Kukamatwa wavamizi, wachimbaji
Anasema Jeshi hilo limekamata wavamizi na wachimbaji wa madini wasiofuata utaratibu wanaozunguka Mgodi wa Barrick North Mara. Jumla ya Viroba 2,367 sawa na Tani 35.5 za mawe yadhaniwayo kuwa na dhahabu vilikamatwa.
Anasema kemikali aina ya Mekyuri ikiwa na ujazo wa gramu 200 pamoja na vilipuzi vya miamba 03 aina ya V 16 visivyo na vibali, watuhumiwa 10 walikamatwa na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.
Wahamiaji Haramu
Anasema wahamiaji Haramu 09 walikamatwa kwa kuingia nchini bila kibali na kukabidhiwa Idara ya Uhamiaji kwa hatua za kisheria.
Watuhumiwa wa mawe ya dhahabu
Kamanda ACP Sarakikya anasema jumla ya watuhumiwa 11 wakiwemo wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara walikamatwa wakiwa na jumla ya Kilogramu 61.16 za mawe yadhaniwayo kuwa na dhahabu.
Anasema watuhumiwa hao wakiwemo watumishi wa Mgodi huo wa Dhahabu watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Mafanikio Mahakamani
Kamanda anasema katika kesi za unyang'anyi wa kutumia silaha jumla ya watuhumiwa 09 walifungwa miaka 30 jela kila mmoja.
Kesi za Kubaka/Kulawiti
Anasema jumla ya watuhumiwa 03 walifungwa miaka 30 kila mmoja kwa makosa ya kubaka na mtuhumiwa mmoja kufungwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Makosa ya kupatikana Nyara za Serikali
Anasema jumla ya watuhumiwa watatu walifungwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.
Kamanda anasema pamoja na mafanikio hayo ya kuzuia, kupambana na kupunguza hofu ya uhalifu katika mkoa huo wa polisi, jeshi hilo limeendelea kuishirikisha jamii kwa kutoa elimu mbalimbali kupitia redio za Kanda ya Ziwa na vyombo mbalimbali vya habari, mikutano ya polisi jamii na mazoezi ya pamoja ya kila mwezi.
Anatoa wito kwa jamii nzima kuendelea kutoa ushirikiano kuwafichua wahalifu wote popote walipo, anawahakikishia kuwa taarifa zozote za uhalifu na wahalifu zitachukuliwa kwa uzito na sheria itafuata mkondo wake.
Pia anawaonya wale wote ambao wanafikiri kwamba wanaweza kutumia Silaha/ Bunduki kutenda uhalifu katika mkoa huo wa polisi wajue kwamba watakamatwa.
Anasema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kukabiliana na wahalifu hivyo anawatahadhalisha wale wote wanaojihusisha na uchimbaji haramu na wizi wa madini ya dhahabu kutoka mgodi wa North Mara kuwa watasakwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Anasema kila mwananchi afuate sheria katika kujipatia kipato na kwamba misako na operesheni ni endelevu hivyo jeshi la polisi linawasihi wananchi wote wenye mapenzi mema na mkoa wao kuendelea kutoa taarifa wasifiche uhalifu ili mkoa wa Tarime Rorya uendelee kuwa salama.
Post a Comment