WAFANYABIASHARA MARA WAIPONGEZA TRA KUKUSANYA KODI KIRAFIKI
Na Jovina Massano, Musoma
WAFANYABIASHARA Mkoani Mara wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kukusanya kodi katika mazingira rafiki tofauti na miaka ya nyuma walitumia nguvu kwa kufunga maduka na akaunti za watu.
Pongezi hizo zimetolewa katika kilele cha shukrani kwa mlipakodi zilizoenda sambamba na hafla fupi iliyoambatana na utoaji wa tuzo, iliyofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex.
Kauli mbiu ikiwa na ujumbe usemao "Asante kwa Kulipa Kodi kwa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Nchi yetu; Kazi Iendelee".
Akizumgumza kwa niaba ya Wafanyabiashara, Meneja Mipango wa Kampuni ya CATA Mining, Alnazir Mawji amesema kuwa kitendo walichokifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania cha kuwashukuru walipa kodi kimewapa hamasa ya kuendelea kulipa mapato kwa wakati.
"Kuna wakati sisi wafanyabiashara tunafanya makosa tunashindwa kulipa kodi kwa muda unaotakiwa lakini pamoja na hayo tutajitahidi tulipe kodi kwa wakati kwani hivi sasa hatubanwi sana na TRA kwa kufungiwa akaunti kama zamani, kwa sasa wamejenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara jambo ambalo limesaidia watu kulipa kodi kwa hiari kwa muda muafaka", amesema Alnazir.
Meneja Kampuni ya CATA Mining
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoani hapa Boniphace Ndengo ameipongeza TRA kwa kuendelea kukusanya kodi kwa ustaarabu huku akiwashukuru wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
Amesema ulipaji kodi kwa hiari umewezesha TRA kukusanya kodi kwa viwango vinavyotakiwa ikilinganishwa na miaka iliyopita na kwamba ulipaji kodi ndio msingi wa maendeleo ya Taifa.
"Mfumo wa ulipaji kodi kwa hiari na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara kumechangia kukua kwa ongezeko la mapato" amesema Boniphace.
Kamishna wa walipakodi wakubwa Alfred Mregi amesema TRA inathamini makundi yote katika jamii ambapo kabla ya kilele cha shukrani kwa mlipa kodi wametoa msaada kwa wahitaji katika vituo 4 vinavyohudumia watu wenye uhitaji wakiwemo watoto.
Kamishna wa walipa kodi wakubwa
"Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 ilikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha T.sh Trillion 22.04, imeweza kukusanya kiasi cha T.sh Trillion 21.93 ambayo ni ufanisi wa asilimia 99 ambao ni sawa na ukuaji wa makusanyo ukilinganisha hapo nyuma ukuaji ulikuwa wa asilimia 23.
" Mamlaka ya Mapato Mara imeweza kukusanya T.sh Billion 99.15 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 91 ya lengo la makusanyo ya T.sh Billioni 108.89", amesema Alfred.
Ameongeza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania imetengeneza mpango mkakati wake wa sita unaoanzia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2026/27 wenye malengo ya kuimarisha ukusanyaji mapato, kuongeza uwajibikaji wa hiari miongoni mwa walipakodi.
Pia uboreshaji wa shughuli za mamlaka ikiwemo na taswira nzuri na mtazamo chanya wa shughuli za mamlaka, kujenga imani na ridhaa kwa walipa kodi pamoja na kuongeza matumizi ya mfumo na kuioanisha.
Meneja wa TRA mkoa wa Mara, Adam Ntoga amewashukuru wafanyabiashara kwa kulipa kodi bila usumbufu na kwamba TRA inajivunia mafanikio makubwa katika ukusanyaji kodi kwa hiari ambao umewezesha mapato kuongezeka.
“TRA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria nawakumbusha wafanyabiashara kuendelea kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari bila usumbufu wala misuguano tuzingatie sheria zilizopo" Amesema Adam.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Halfan Haule akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa Jenerali Suleiman Mzee amewapongeza wafanyabiashara wote kwa kulipa kodi kwa hiari ambayo imewezesha TRA kukusanya kodi kwa kiwango stahiki.
"Fedha hizi zinazokusanywa zinaisaidia Serikali katika utekelezaji wake wa mipango ya maendeleo ya nchi yetu katika sekta ya miundombinu katika afya, elimu, maji, viwanja na barabara hivi vyote vinapatikaka katika kodi zinazokusanywa kwenu, utaratibu huu wa kodi uliwekwa kisheria", amesema Haule.
Amewasisitiza TRA kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara ili waweze kuzingatia ulipaji wa kodi kwa mujibu wa sheria lakini pia kuimarisha mahusiano kwa wadau wa maendeleo kulingana na makundi yao ya biashara ili kuwajengea uelewa mpana wa ulipaji kodi.
Post a Comment