ALIYEOKOA WATU KWENYE AJALI YA NDEGE KUAJIRIWA SERIKALINI
Na Alodia Babara , Bukoba.
WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa amesema,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu ameagiza kijana Majaliwa Jackson (20) aliyesaidia kufungua mlango wa Ndege iliyopata ajari na kusababisha kuokoa maisha ya watu 24 akabidhiwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili aweze kupata mafunzo zaidi na aajiriwe katika Jeshi la Zimamoto na Uokoji.
Majaliwa ameyasema hayo Novemba 7,2022 wakati akitoa salaamu za rambirambi kwa wafiwa na watanzania wote katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kutokana na msiba wa vifo 19 vilivyotokana na ajali ya ndege ya Precision Air aina ya ATR 42-500 yenye namba za usajili 5 H-PWF iliyotokea Novemba, 6,2022 wakati ikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu ameniagiza nimkabidhi kijana Majaliwa Jackson (20) ambaye alisaidia katika kuwaokoa watu waliokuwa Kwenye ndege kwa waziri wa ulinzi mhandisi Hamad Masauni ili akamuunge kwenye kikosi cha wokozi" Amesema Majaliwa.
Awali amesema idadi ya watu wawili iliyokuwa ikionekana kuongezeka ni mmoja kutoka uwanja wa ndege na kijana majaliwa.
Amesema wavuvi waliopo eneo la Nyamkazi karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba watapata mafunzo ya uokozi baada ya kuagiza ofisi kuja kuendesha shughuli hiyo.
Akisimulia kuhusu ajali hiyo
Majaliwa Jackson (20) mkazi wa Nyamkazi ameeleza jinsi alivyofanya jitihada akiwa na wavuvi na kuokoa watu waliokuwa kwenye ajali ya ndege ya Precision Air.
Amesema kuwa akiwa kwenye biashara zake za kuuza dagaa ambazo huzifanyia katika mwalo wa Nyamkazi karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba akitafuta chenji ya mteja wake aliyekuwa amenunua dagaa ndipo aliona ndege hiyo iliyopata ajali ikija na kurudi karibia na kisiwa cha Msira kilichopo ziwa Victoria.
Amesema, kutoka kisiwa cha Msira ndege ilipinda kona kuelekea kastam ya Bukoba na badae ilivyorudi uwanja wa ndege kabla haijatua ilitumbukia kwenye maji ziwa Victoria alikuwa akiiona kwa mbali wakati akitafuta chenji ya mteja aliyemuuzia dagaa.
“ Sehemu nilipokuwa walikuwepo wavuvi watatu nikawaomba twende kuokoa na muda huo watu waliokuwa kwenye ndege walikuwa wanapitisha mikono kwenye madirisha kuashiria kuomba msaada ndipo kwa kutumia mitumbwi ya kasia iliyokuwepo eneo la Nyamkazi tuliendesha mitumbwi kuelekea ndege ilipokuwa ziwani” Amesema Jackson.
Jackson amesema baada ya kufika karibu na mlango wa ndege akaufungua na watu wakaanza kushuka kuingia kwenye mtumbwi na kwakuwa watu waliokuwa wanaingia kwenye mtumbwi walikuwa wengi alishuka kwenye mtumbwi huo na kushika kipande cha bawa la ndege lililokuwa limekatika linaelea juu ya maji.
Amesema aliona upande wa rubani kuna mtu anapiga kwenye kioo na kuelekeza mkono wake kwenye mlango wa daharura kama kuomba msaada wa kufunguliwa mlango ndipo alielekea kwenye mlango huo na kujaribu kuufungua bila mafanikio.
Amesema alifanikiwa kuona mkanda kwenye maji kama wa mkoba wa kike na kuuchukua kisha kufunga kwenye mlango alipoanza kuvuta kufungua mlango mkanda ulikatika ukampiga jicho la kulia na kupoteza fahamu alipozinduka alijikuta hospital ya mkoa.
Post a Comment