ASKOFU MKUU AICT TANZANIA AWEKWA WAKFU
Na Fabian Fanuel, Mwanza
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania ( AICT) Musa Masanja Magwesela amesimikwa wakfu baada ya kuchaguliwa katika mkutano wa Sinodi kuu ya Kitaifa uliofanyika mwezi wa tisa mwishoni katika kanisa la hilo Buzuruga mkoani Mwanza.
Katika tukio hilo la kuwekwa Wakfu ambalo limefanyika Nevemba, 6, 2022 limehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka serikalini na watumishi wa kanisa hio ambapo pia Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga Zakayo Bugota amesimikwa kuwa Askofu Mkuu Msaidizi.
Tukio la kuwekwa Wakfu kwa Askofu Mkuu na Msaidizi wake limefanyika katika kanisa la AICT Makongoro kuanza asubuhi saa 2 hadi saa 8 mchana, lililohudhuriwa na umati mkubwa wa waumini kutoka madhehebu mbalimbali Mkoani Mwanza na nje ya mkoa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali Mgeni Rasmi wa sherehe hizo Waziri wa Madini Dkt Doto Biteko amempongeza Askofu Mwageswela na Msaidizi wake Askofu Bugota kwa kuaminiwa katika nafasi hizo na kuomba wawaunganishe waumini wa Kanisani hilo ili liendelee kuongezeka kwa idadi ya watu.
Waziri Doto Biteko
"Baba Askofu Mkuu na Msaidizi wake mmeaminiwa sana, mmepewa nafasi ya kumtumikia Mungu na kanisa la AICT Tanzania, fanyeni kazi ya kuhubiri Neno la Mungu kiroho na kimwili ili kanisa hili liwe na maendeleo makubwa" alisema Waziri Biteko.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu iko bega kwa bega na wewe katika kuwasaidia wananchi wapate kuponywa katika mambo ya kiroho na kimwili maana kanisa lina nafasi kubwa katika maisha ya mtu"
Dkt. Biteko amesema anaamini katika uongozi wa Askofu Mkuu Musa Magwesela na Msaidizi wake Askofu Zakayo Bugota, ndio maana wamepewa miaka mingine kuongoza kanisa hilo katika muhula wa pili.
Akitoa salama za kanisa baada ya kuwekwa Wakfu Askofu Mkuu Magwesela amesema wanashukuru kupewa nafasi hiyo kumtumikia Mungu, wameomba kupewa ushirikiano ili waweze kutimiza matarajio ya kanisa.
Pia ameiomba Serikali kutatua migogoro iliyopo kwenye umiliki wa viwanja mali ya kanisa ambavyo vimeingiliwa na watu kinyemela.
Post a Comment