WANANCHI WA KWANGWA WAOMBA MAHINDI YA SERIKALI
Na Jovina Massano, Musoma
WANANCHI wa Kata ya Kwangwa katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kuwasaida mahindi yanayotolewa na serikali.
Wananchi wamefikia uamuzi huo kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula ambayo imesababisha washindwe kununua bidhaa zingine kwa kuwa pesa wanayopata inaishia kununua vyakula.
Ombi hilo limetolewa na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara baada ya Afisa Kilimo wa Kata hiyo Ibrahim Wandet kutoa elimu ya Kilimo huku akiwaasa wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na msimu wa mvua kuchelewa kuanza.
Mkazi wa mtaa huo Mshua Jamali amesema" Sisi wananchi tuna changamoto hususani kwenye suala zima la chakula, bei zimepanda sana, mzunguko wa fedha ni mdogo na kusababisha hali iwe ngumu kimaisha.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano
" Sisi wananchi tunamuomba Rais wetu Samia Suluhu popote pale alipo anaposikia taarifa hii, sisi wakazi wa Kwangwa tunaomba walau tuweze kuletewa mahindi ya ghalama nafuu ili kila mwananchi aweze kupata chakula nilisikia wenzetu wa wilaya ya Bunda na Ukerewe wamepelekewa mahindi hayo ya bei nafuu tusaidiwe na sisi".
Afisa Kilimo Ibrahim Wandet amesema mwaka huu mvua inanyesha kwa kusuasau kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo ni vema wananchi waandae mashamba mapema lakini pia wapande mazao yanayostahimili ukame ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula.
"Kuhusu habari za upungufu wa chakula kitaalam tunahamasisha wananchi katika msimu huu wa mvua ambao tayari umeishaanza japokuwa inasuasua.
" Wakulima waandae mashamba mapema ili mvua zinapoanza kunyesha ziwe za kupandia na wapande mazao yanayokomaa mapema na kustahimili ukame, mfano mihogo ,viazi,na mengineyo yenye kuhimili kipindi cha mvua chache kwa maana ya mbegu bora" amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na wananchi kuomba mahindi ya serikali, tayari wameishawasilisha taarifa hizo za kila mwezi na za robo, kuhusu hali ya chakula ambayo siyo nzuri, amesema tayari mamlaka husika wanafuatilia na watakapokamilisha mchakato huo watapata taarifa.
Diwani wa Kata hiyo Fredrick Mganga wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA )amesema Serikali imepokea taarifa kupitia maafisa wake wa Kilimo waliopo katani hapo hivyo amewaomba wananchi kuwa wavumilivu ili mamlaka husika iweze kufanya utaratibu wa kuleta mahindi ya bei nafuu.
"Hivi Sasa kilo moja ya mahindi inauzwa kwa kiasi cha Tsh 1300 kutoka Tsh 900 hivyo kuwa na ongezeko la Tsh 400 na mchele umepanda kutoka 1300 hadi kufikia 2800, debe la mahindi ni 26000-30,000 hali hii ni changamoto kwa wananchi walio na vipato vya chini" amesema Fredrick.
Post a Comment