DC KISWAGA AMESEMA WANANCHI WANAODAI FIDIA HAWATALIPWA
Na Mwandishi Wetu, Kahama
MKUU wa Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga Festo Kiswaga amesema Wananchi wa Kijiji cha Kakola wanaodai fidia ya ardhi hawatalipwa kwakuwa walifanyiwa uthamini wakati wa sheria iliyokuwa ya kikoloni ambayo haikutambua malipo ya fidia ya ardhi.
Akizungumza na DIMA Online kuhusu malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kakola wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati yao na Mgodi wa Barrick Gold Corporation amesema;
"Huu mgogoro naujua, ukweli ni kwamba wakati mgodi unachukua maeneo kulikuwa na sheria iliyokuwa inatumika ya mkoloni ambayo haikutambua haki ya fidia ya ardhi, ulipofanyiwa uthamini ulikuwa hulipwi fidia ya ardhi.
" Kwahiyo watu waliofanyiwa uthamini wakati wa sheria hiyo ya ardhi hawakulipwa kwakuwa ardhi haikuwa na thamani, ulilipwa vile vilivyoendelezwa kama umejenga nyumba au umepanda miti, miembe unalipwa ila ardhi hulipwi mgogoro umetokana na hiyo sheria, hao hawatalipwa chochote" amesema Festo.
Amesema mgogoro huo ulishafika hadi Ofisi ya Waziri Mkuu majibu ni yaleyale kuwa hawawezi kulipwa vivyohivyo na Wizara ya ardhi ambapo wananchi walielezwa hawastahili kulipwa kwasababu ya sheria ya wakati huo.
" Waliofanyiwa uthamini kabla ya kutungwa kwa sheria ya mwaka 1999 hawakulipwa ardhi zaidi ya kulipwa maendelezo, kwahiyo hata huyo anaesema anadai fidia aje ofisini ataona vielelezo, kama walifanyiwa uthamini 1996 hawakulipwa ardhi maana ardhi ilikuwa hailipwi kwasababu ya sheria haikutambua fidia ya ardhi.
" Tuna vielelezo vyao hata hao wanaolalamika wakija ofisini kwangu watakuta hizo barua kama kweli walikuwepo wao wenyewe na siyo mchimbaji maana palikuwa na eneo la uchimbaji sasa mchimbaji kwenye kupewa fidia hayumo , ila kama alikuwa amejenga nyumba, amepanda miti, mazao walilipwa wote" amesema.
Festo amesema wapo wananchi waliofanyiwa uthamini mwaka 2003 kutokana na Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 wao walilipwa mali zao pamoja na ardhi na kwamba kuna malalamiko ya wananchi wapatao 180 wanaodai kupunjwa fidia ambapo kati yao waligundulika kufanya udanganyifu wakati wa uthamini ambao haukuwa wa uhalisia na walioonewa walilipwa.
" Ilipotungwa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 waliotathminiwa mwaka 2003 malipo yalifanyika vizuri watu wakalipwa maendelezo pamoja na ardhi wakatoka kwenye maeneo, tatizo lililotokea wakati wa uthamini kuna wananchi 180 wanadai kupunjwa kwenye fidia, tulishaunda kamati, Tume ilishaundwa majibu ni hayohayo hawawezi kulipwa kwakuwa kulifanyika udanganyifu" amesema Festo.
"Mgogoro huo ulichangiwa na afisa ardhi mmoja alikuwa anahongwa pesa akawa anaongeza viwango vya malipo kwenye uthamini ili wapate malipo makubwa, ili na yeye apate hela, sasa wakati Barrick inataka kulipa ikaonekana gharama ni kubwa kuliko uhalisia wakakataa kulipa.
Kiswaga amesema" Wakakata rufaa wakaomba wabadilishiwe mthamini, mfano mtu anaandikiwa ana katani laki nne ekali zenyewe zipo mbili, anaandikiwa Tsh Milioni 40 lakini haki yake ni kulipwa Tsh Milioni 20 au 10 hivyo hawakulipwa kama walivyotaka kwakuwa walizidishiwa viwango vya malipo" amesema.
"Walipokuwa wakihojiwa wakasema afisa ardhi aliwaambia watalipwa kiasi kadhaa ambacho kilikuwa kikubwa hakikuwa sahihi, waliothibitika kufanyiwa uthamini kwa kupunjwa walilipwa, afisa ardhi aliongeza viwango ili watu wapate pesa nyingi kwakuwa alihongwa pesa. Niliyoyakuta ndiyo hayo, ila yote hayo yamechangiwa na Rushwa iliyosababishwa na baadhi ya watumishi wa ardhi" amesema Festo.
Ameongeza" Kwasababu lipo namna hiyo sisi tunaishi nalo hivyohivyo, walishapeleka malalamiko hadi kwa Waziri mkuu, Wizara ya Ardhi mara tatu wanaambiwa haiwezekani,Waziri wa Madini analijua hilo hata mbunge alivyoingia ana taarifa zote na yeye alishalipeleka kwa Waziri mkuu akaambiwa halitawezekana" amesema.
Awali wakizungumza na DIMA Online baadhi ya wananchi akiwemo Emmanuel Bombeda ambaye ni miongoni mwa wachimbaji wa madini anayedai fidia, alisema wamefikia hatua hiyo yakumuomba Rais kuingilia kati mgogoro huo baada ya kutafuta haki yao kwa zaidi ya miaka 20 pasipo mafanikio huku baadhi yao wameshafariki dunia wakiwa hawajapewa stahiki zao.
"Kitendo cha serikali kutuondoa kwa nguvu kwenye maeneo yetu kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kisha ardhi yetu kuendelezwa na mgodi wa Barrick kwa shughuli za uchimbaji pasipo kutulipa fidia kumesababisha wananchi 363 kuwa maskini wa kutupwa na hata wengine wamekufa pasipo kupata hata jasho lao" alisema Emmanuel
Idadi hiyo inahusisha makundi ya aina tatu wakiwemo,wamiliki wa mashamba,wachimbaji wadogo na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo walioumia wakiwa kazini na kuachishwa kazi mwaka 2007 kwa nyakati tofauti pasipo kupewa stahiki zao.
George Kingi, ambaye ni miongoni mwa wadai wa fidia, alisema kabla ya kuondolewa, maeneo hayo yalikuwa na nyumba za kuishi, mazao na mashimo ya wachimbaji wadogo ambao pia waliondolewa kwa amri ya serikali mwaka 1996.
"Tumemwona rais wetu alivyo mpenda haki na mwenye huruma na watanzania, juzi ametangaza kuwalipa mafao yatokanayo na michango ya mifuko ya jamii watumishi wa vyeti feki ambao ilikuwa ni haki yao, tunaamini hata sisi mgogoro huu ukimfikia ataguswa na kuhakikisha nasi tunapewa haki yetu ambayo imeminywa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi.
"Kwa kipindi chote hicho tumefuatilia haki zetu ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuonana na rais watatu waliopita pasipo mafanikio, kwa hivyo tunaamini nafasi yetu ya mwisho ipo mikononi mwa rais Samia iwapo ujumbe wetu utamfikia" alisema George.
Aliongeza " Licha ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala, Bhikhu Mohamed, kuwasilisha hoja ya mgogoro huo kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania julai 26 mwaka 1996 bado wananchi hao hawakulipwa(Nakala ya hotuba hiyo tunayo)" alisema.
Afisa uhusiano wa mgodi wa Barrick, Agapiti Kisoka, alisema ana muda mfupi tangu amekuwa kwenye ofisi hiyo hivyo baadhi ya madai ya wananchi hayajui huku akidai anachoelewa ni kwamba mgodi unapotaka kuongeza eneo hufanya makubaliano na wananchi kwaajili ya kuwalipa fidia.
Afisa Madini wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Hango, alithibitisha kuwepo kwa malalamiko yanayohusu fidia za wananchi na kusema kwamba suala hilo bado linaendelea kushughulikiwa na mamlaka za serikali.
NUKUU YA SHERIA:
MFUMO WA MILKI YA ARDHI WAKATI WA UKOLONI (1890- 1960)
Tanganyika ilitawaliwa na Wajerumani na Waingereza:-
Wajerumani (1890–1919)
>>> Tamko la Wajerumani la mwaka 1895 liliweka bayana kuwa ardhi yote ni mali ya Mfalme Kaiza wa Ujerumani.
>>>Walianzisha umiliki kwa njia ya Hati.
Waingereza (1919–1961)
>>>Walitunga sheria ya Ardhi na 3 ya 1923 kuweka msisitizo katika mfumo ulioanzishwa na Wajerumani na kutamka kuwa ardhi yote ni mali ya umma chini ya Gavana.
>>>Umiliki wa hati ulikuwa na nguvu kisheria dhidi ya umiliki wa kimila
Katika kipindi cha ukoloni wazawa walipoteza sauti juu ya ardhi yao.
C. KIPINDI CHA UHURU HADI SASA
Kipindi cha miaka ya 1961- 1990
>>>Mamlaka ya Gavana juu ya ardhi ilihamishiwa kwa Rais.
>>>Mwaka 1967 Azimio la Arusha lilitangazwa kuweka misingi ya uzalishaji mali mikononi mwa umma.
>>>Sheria zilizotungwa katika kipindi hiki ni pamoja na Sheria ya Utwaaji Na. 47 ya 1967 ambayo iliwezesha utwaaji wa ardhi kwa matumizi mbalimbali kama vile uanzishwaji wa Mashamba ya NAFCO na NARCO na Sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa Na. 21 ya 1975 ambayo ilihalalisha uanzishwaji wa Vijiji vya ujamaa.
Kipindi cha kuanzia 1991 hadi sasa
>>>Licha ya kuwepo kwa Sheria hizo bado vijiji vingi viliendelea kuwa na migogoro kutokana na kuingiliana kwa haki na maslahi kati ya wakazi wa vijiji vipya na vya zamani
>>> Migogoro hiyo ilipelekwa kuundwa kwa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Masuala ya Ardhi mwaka 1991.
>>>Mwaka 1992 ilitungwa Sheria ya Milki ya Ardhi Tanzania ambayo ilifuta Vijiji vya asili na kuhalalisha vijiji vya ujamaa.
Tume ilitoa mapendekezo yake mwaka 1992 ambayo ni pamoja na:-
>>>Ardhi ipewe ulinzi wa Kikatiba
>>>Kuwepo na Sera na Sheria ardhi za kizalendo
>>>Kuweka milki ya hatma kwenye vyombo vyenye uwakilishi mpana wa wananchi
>>>Kuunda mfumo wa usuluhishi na utatuzi wa migogoro ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji
>>>Ardhi igawanywe katika makundi
Mapendekezo hayo yalipelekea kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria za Ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999.
Post a Comment