MLEMAVU WA VIUNGO ANAYEUNDA BAJAJ INAYOTUMIA INJINI YA PIKIPIKI
Na Dinna Maningo, Tarime
" Mimi ni Mlemavu wa Viungo lakini kuwa mlemavu hakunifanyi niwe tegemezi, kila siku naamka na kwenda kibaruani kutafuta riziki, siku zote sitakata tamaa ya maisha, nitajituma na kufanya kazi kwa bidii ili kuisaidia familia yangu " anasema.
Ni Yohana Wilson mwenye ulemavu wa viungo, Mkazi wa Wilaya Tarime Mkoani Mara, mwenye mke na watoto 10 mbunifu anayeunda Bajaj inayotumia injini ya Pikipiki ikiwa na gia yakutumia mkono na mguu na breki yakutumia mkono na mguu, yenye uwezo wa kuendeshwa na mtu yeyote mwenye ulemavu na asiye mlemavu.
Mwenyezi Mungu kamjalia Yohana kipaji na ubunifu wa kuunda vitu, hajawahi kusomea ufundi chuo chochote katika fani ya uundaji wa vitu bali anaunda na kutengeneza vitu kwa kujifunza kwa kuona vitu. Pia ni muundaji wa baiskeli za wamelavu na ukipoteza funguo ya gari, kufuli ana uwezo wa kukuchongea funguo nyingine.
Yohana anasimulia namna anavyofanya kazi zake zinazomwiingizia kipato na kuendesha maisha yake japo kipaji chake bado walio wengi hawakifahamu ama hawajui shughuli zake za uundaji wa vitu kutokana na ulemavu alionao unaosababisha wengine wasiamini kama yeye ndiye anayeunda.
Anasemaa hajawahi kwenda chuo chochote kusomea ufundi wa kuunda vitu isipokuwa amejifunza kwa juhudi zake mwenyewe kwa kuona kupitia vitu vya kisasa vilivyotengenezwa viwandani.
" Sijafundishwa na mtu yeyote kuunda Bajaj isipokuwa nilijifunza kwa kuona bajaj za kisasa nami nikaanza kuunda yangu kwa muundo ambao mlemavu yeyote anaweza kuendesha.
" Bajaj nazounda zinatumia injini ya pikipiki za kawaida, vifaa ninanunua madukani, taili moja inauzwa kuanzia 60,000 inategemea na ukubwa, natumia mabati mazito yale yanayotengeneza milango ya geti, naunda bodi, kava mita moja inauzwa Tsh 15,000 ili itoshe bajaj ni mita sita, naunda mwenyewe viti kila kitu kinachohusika kwenye bajaj natengeneza na kuunda mwenyewe" anasema Yohana.
Anasema hadi sasa amefanikiwa kuunda bajaj tatu za kubeba abilia zenye uwezo wa kubeba watu 8- 10, mbili zilipata wateja, moja ilinunuliwa na mlemavu Nyamongo na nyingine ilinunuliwa na mlemavu wilayani Serengeti na moja anaitumia kwa ajili ya usafiri yeye na familia yake.
"Bajaj ni imara hazina joto hata jua likiwaka, bajaj za kisasa zinatumia gia ya mkono na breki ya mguu, bajaj ninayotengeneza mimi zinatumia breki ya mkono na breki ya mguu,gia ya mkono na gia ya mguu. Pia nina uwezo wa kubadilisha mfumo wa bajaj ya kisasa na ikatumiwa na mlemavu kwa kuiongezea breki na gia za mkono.
"Kuna bajaji gia zipo mguuni na breki zipo mguuni nina uwezo wa kuiongezea gia ya kutumia mkono, nina uwezo wa kuitengenezea gari breki ya mguu na mkono,sclachi ya mkono na mguu, nina uwezo wa kuweka breki ya ziada kwa gari ya mafunzo.
Bajaj iliyoundwa na Yohana
"Mwalimu anapomfundisha mwanafunzi kuendesha gari hiyo gari inakuwa na breki moja mimi naongeza nyingine zinakuwa mbili ya mwalimu na mwanafunzi hata mwanafunzi akisahau kushika breki wewe unaemfundisha unashika breki ya kwako" anasema.
Anasema bajaj inapokamilika anaiuza kwa T.sh Milioni tatu, anasema bajaj za madukani zinauzwa T.sh Milioni 7 hadi T.sh Milioni 9.
Faida ya Bajaj
Yohana anasema bajaj anazounda hazina masharti zinaendeshwa na mtu yeyote mlemavu na asiye mlemavu, zina gia na bkeki ya kutumia mkono na mguu, ni tofauti ya bajaj za dukani.
"Bajaj nayounda inatumiwa na watu wote kama wewe ni mlemavu wa viungo una uwezo wa kutumia gia,breki ya mguu na mkono, tofauti na bajaj za dukani ambazo zenyewe ukinunua kama ni ya kutumia mkono ni mkono tu kama ni yakutumia mguu ni miguu tu yaani mpaka ununue nyingine inayotumia mkono.
Anasema bajaji anayounda ikiharibika inatengenezeka "Ikiharibika wewe peleka kwa fundi wa pikipiki wataitengeneza maana inatumia injini ya pikipiki CC 200 tofauti na bajaj za spesho za madukani zikiharibika zenyewe zina wataalamu wake wanaozitengeneza.
Anaunda Baiskeli za walemavu
Mbali na ubunifu wa kuunda bajaj ni muundaji wa baiskeli ya magurudu matatu kwa ajili ya watu wenye umemavu, huziuza na kupata fedha zinazomsaidia kuendesha maisha yake na familia yake.
" Kazi yangu ya kwanza nilikuwa naziba pancha za baiskeli, kunyoosha baiskeli kwa kujifunza kwa watu wengine nikiwa wilayani Serengeti, kazi niliyoifanya kwa miaka 10 baada ya hapo nikaanza kuunda baiskeli za watu wenye umelavu.
"Niliunda kwa kuangalizia baiskeli yangu niliyokuwa nayo wakati huo ilikuwa mwaka 1998, hadi sasa nimefanikiwa kuunda baiskeli zaidi ya 100 tangu nilipojua kuunda, kwenye uundaji kuna gharama za vifaa.
"Mahitaji ya baiskeli ni pamoja na ringi, tail, mapedo, myororo, bomba, bati zito la kuweka sehemu ya kukanyaga, kuchomelea, kupaka rangi hadi kukamilika kwa baiskeli inasimamia laki tatu na ninaiuza 400,000 hadi 500,000.
Baiskeli iliyoundwa na Yohana
Anaongeza " Hizi baiskeli hazipo madukani mpaka uende SIDO, zipo zile za kusukumwa na mtu, hizi natengeneza kwa rika zote una uwezo wa kuipaki ndani ya gari unapokuwa unasafiri ni nyepesi na ina uwezo wa kupanda sehemu zenye mwinuko, zinatumika katika mazingira yote ilimradi una uwezo wa kuiendesha siyo mpaka usukumwe na mtu kama Wheelchair zinazouzwa madukani ( Viti Mwendo)" anasema Yohana.
Kiti cha Dukani
Changamoto
Anasema kwa mwaka ana uwezo wa kuunda baiskeli tano huziunda pale tu anapopata mteja na kwamba endapo angekuwa na mtaji angeunda nyingi ili mteja akifika ananunua na zingine angeziuza kwa kuzitawanya kwenye maduka ya watu katika Wilaya mbalimbali mkoani Mara ili watu wazipate kwa urahisi wakiwemo watu wenye ulemavu.
" Naunda baiskeli na bajaj pale tu napopata mteja, ningekuwa na mtaji ningeunda nyingi zikakaa hapa nakofanyia kazi mtaa wa Kibasa barabara ya Nyamwaga watu wakipita wanaziona, mtu akitaka anachukua anaondoka, kwakuwa sina mtaji naziunda pale tu napopata oda, mtu anaweza kuhitaji lakini akifika asikute iliyo tayali anaondoka.
Anachonga Funguo
Yohana ni mbunifu hategemei kazi moja kwani ukipoteza funguo za gari ,kufuli au bajaj huna haja ya kuhangaika, fika kwa Yohana yeye ana uwezo wa kuchonga funguo na hajafundishwa na mtu zaidi ya kujifunza kwa kuona.
"Kama umepoteza funguo za gari au za kufuli unaleta kufuli lako au gari lako naiona natengeneza. Hii kazi nimeianza mwaka 2002 nilijifunza kwa kuona nikiwa Mwanza nilikuwa naona wahindi wakichonga nikawa napeleka kufuli zangu au za watu wengine wananichongea funguo.
" Wakati anachonga nami najifunza kwa kutizama anavyochonga pasipo yeye kujua kama najfunza, kiukweli uchongaji wa funguo unaniweka mjini zina kipato na zina soko sema mtaji wa kununua mahitaji ndio shida, Ninawashukuru wanangu huwa wananisaidia kazi.
Anaongeza" nachonga funguo kwa kutumia tupa (file) hii inatumia muda mrefu kukamilisha funguo, natumia nusu saa kukamilisha funguo lakini ningekuwa na mashine ningetumia dakika tano, mashine inauzwa Milioni 5 inapatikana Dar es Salaam," anasema.
Yohana akichonga Funguo
Yohana anaongeza kusema kwa siku anaweza kuchonga funguo kati ya 10-20 na gharama zake ni Tsh 10,000-20,000 kutegemea na aina ya funguo za gari, funguo za kufuli za nyumbani anachonga kwa Tsh 1000 hadi 10,000,vitendea kazi alivyonavyo vya kuchonga funguo vinavyoghalimu 200,000.
Ezra Isiaga (30) mlemavu wa viungo mkazi wa mtaa wa Serengeti anasema Yohana ni mbunifu anafahamu kuunda vitu vingi nakwamba hata yeye anamiliki baiskeli aliyoinunua kwa Yohana kwa Tsh 500,000.
"anafahamu kuunda Bajaj na Baiskeli, baiskeli zake ni nyepesi kuendesha ni rahisi kusafiri nayo iwe kwenye pikipiki, bajaj au gari, inaingia mahali popote unaweka hata ndani, uhifadhi wake ni rahisi ina uwezo wa kuendeshwa kwa kurudi nyuma, mbele , inageuka popote," anasema.
Ezra Isiaga
Ezra anasema changamoto kubwa katika uundaji huo ni upatikanaji wa vifaa " mfano spoku,ringi zenyewe zinapatikana kwa shida ni chache kwasababu ni ringi ambazo hazitumiwi na watu wengi kutokana na saizi ya ringi na unalazimika kuiagiza Musoma au Mwanza gharama ni ghali kwasababu upatikanaji wake ni mgumu.
"Yohana ana kipaji cha pekee ametufundisha hata sisi walemavu uundaji wa vitu Mimi aunda viatu na alinifundisha yeye, hata kuna mlemavu mmoja anafanya kazi halmashauri ya wilaya ya Tarime ameiwekea gari yake breki ya kutumia mkono na wengine wengi wanaotumia bajaj za madukani anaziongezea gia na breki na kumwezesha mlemavu kuzitumia kwa urahisi" anasema.
Elimu
Yohana anasema amezaliwa 1967 katika wilaya ya Serengeti, amesoma shule ya msingi Msati na kuhitimu, alijiunga na elimu ya Sekondari katika shule ya Isango -Mara na kuhitimu kidato cha nne.
Alijiunga na Chuo cha Ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu Yombo kilichopo Dar es Salaam na kusomea Kilimo na Mifugo pamoja na uchomeleaji ngazi ya Cheti kwa kipindi cha miaka miwili na kuhitimu mwaka 1989.
"Sikufanikiwa kupata ajira ndipo nikajiunga na kazi ya kuziba pancha za baiskeli na kunyoosha baiskeli, wakati nasoma Chuo Bajaji hazikuwepo nimejifunza mweyewe kuunda bajaji na Baiskeli kwa kuona kupitia bajaji za kisasa za madukani"anasema Yohana.
Yohana akiwa na watoto wake
Ombi
Yohana Wilson anawaomba wadau mbalimbali kumsaidia kupata mtaji na vifaa vya kisasa kwakuwa anafaya kazi kwa kutumia vifaa duni vinavyosababisha atumie muda mwingi kukamilisha kazi, akiwa na vifaa vya kisasa ataokoa muda na kazi yake itakua kwa ufanisi mkubwa na itamrahisishia kazi yake.
Yohana anapatikana Tarime mjini barabara ya Nyamwaga mtaa wa Kibasa jirani na uwanja wa Serengeti, kwa Mawasiliano zaidi mpigie kwa namba +255762149759.
Sera ya Taifa
Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 inasema ufanisi wa maisha ya kila siku ya mtu mwenye ulemavu unategemea sana upatikanaji wa nyenzo za kujimudu anazotumia katika kukabiliana na mazingira.
Pamoja na umuhimu wa nyenzo hizo upatikanaji wake ni mgumu na watu wenye Ulemavu na ndugu zao hawapati taarifa za kutosha kuhusu wapi pakuzipata, pale nyenzo zinapopatikana zinakuwa ghali na kufanya watu wengi wenye Ulemavu kushindwa kuzinunua .
Kutokana na kukosa nyenzo hizo watu wenye Ulemavu wanashindwa kumudu mazingira hivyo kunyimwa fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika Taifa lao.
Tamko la Sera.
>>> Kwa kushirikiana na vyama vya watu wenye Ulemavu utawekwa utaratibu wa kutoa taarifa kuhusu upatikanaji nyenzo muhimu.
>>>Serikali kwa kushirikiana na wadau itagharamia upatikanaji wa nyenzo za kujimudu kwa wasio na uwezo.
>>>Serikali itagharamia nyenzo hizo itakapodhihirika kwamba mtu mwenye ulemavu hawezi kuzilipia na wala hana mhisani anayeweza kugharamia kwa niaba yake.
>>>Serikali itatoa msamaha wa kulipia ushuru kwa nyenzo zote za kujimudu kwa watu wenye ulemavu zitakazoagizwa kutoka nje ya Nchi.Aidha serikali haitatoza kodi nyenzo zinazotengenezwa nchini.
>>>Utawekwa utaratibu utakaohakikisha kwamba nyenzo bora na za bei nafuu zinazalishwa nchini.
Mwaka 1975 Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba wa Haki kwa watu wenye ulemavu, mwaka 1993 ilisaini mkataba wa Haki na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu na mkataba wa Haki za mtoto uliosainiwa 1989.
Bajaj ya Dukani
Post a Comment