HEADER AD

HEADER AD

DKT. MPANGO ASISITIZA SANAA YENYE UASILI NA MAADILI



Na Andrew Chale, Bagamoyo

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewahakikishia Wasanii kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu itaendelea kuunga mkono wasanii wote.

 Pia ameitaka sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kuwanufaisha vijana wengi zaidi hapa nchini.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akizindua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.

“Sanaa ndiyo roho ya taifa lolote pia hatuna budi kuhakikisha tuna sanaa yenye asili na maadili yanayotuwakilisha sisi watanzania, nawasihi watanzania wenzangu hasa wasanii wetu wa kizazi kipya kuepuka tabia ya kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili yetu.

“Pale inapolazimika kuiga sanaa na tamaduni za mataifa mengine, basi mhakikishe mnaiga sanaa zinazoendana na maadili na tamaduni zetu, tusipoteze asili, heshima na utambulisho wetu.”

Amesema wasanii wanaweza kuiga yale mazuri yanayofaa na yanaendana na maadili ya watanzania lakini yale yasiyotufaa wawaachie wenye tamaduni zao.

Ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui ya kazi zao wakikumbuka kwamba wasanii ni kioo cha jamii.

Makamu wa Rais amewataka wasanii kutengeneza taswira nzuri katika jamii, walezi na wazazi ambayo haitawafanya wawe wagumu kuruhusu vijana wao kujihusisha na sanaa kupitia muziki na filamu.  

Dkt. Mpango ametoa maagizo nane kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kuendelea kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kikamilifu ili ziendelee kuwa na mchango thabiti katika uchumi wa taifa, kuendelea kusimamia shughuli za michezo na Sanaa vema kuanzia shuleni kwa sababu kwa sasa zinatambuliwa kama taaluma kamili na ajira.

Pia viongozi katika mamlaka zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waendelee kushirikiana na Wizara yenye dhamana katika kuendeleza shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo.


Ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhifadhi, kutunza na kutangaza tamaduni za makabila yote ya Tanzania kupitia utalii wa kiutamaduni na kutoa nafasi kwa makabila yaliyopo nchini kuonesha tamaduni zake za chakula, dawa za asili, mavazi, makazi na aina za ngoma na burudani zake.

Ameagiza kila mkoa uweka utaratibu wake wa kuendeleza utamaduni wa mkoa husika iwe sehemu ya utalii wa kiutamaduni wa mkoa huo.

Akizungumza na timu ya taifa ya Serengeti Girls Julai 2022 Ikulu amezitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana juu ya namna bora ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Utamaduni ili kuongeza ufanisi katika shughuli zitakazochagiza ukuaji wa uchumi na ajira kwa vijana kupitia sekta  sekita ya burudani.

“Katika suala hili Waziri nataka ripoti au taarifa limefikia wapi utekelezaji wake na naomba taarifa hii inifikie kabla ya Desemba 30, 2022 kabla ya kufunga nusu mwaka ya mwaka wa fedha” amesema Dkt. Mpango.

Pia ameiagiza wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ishirikiane na wadau husika kuendelea kutoa elimu na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zote zinazohusiana na Hakimili, Hakishiriki, mirabaha na mikataba katika sekta za Utamaduni na Sanaa kwa ujumla wake.

Amesema Tamasha la Bagamoyo liendelee kuboreshwa kila mwaka ili lifikie hadhi ya matamasha mengine makubwa duniani, wizara itoe kipaumbele katika kukitangaza Kiswahili duniani kuanzisha kituo cha sanaa cha watoto na vijana wenye vipaji na ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa elimu, kuanza ujenzi wa nyumba changamani na uzalishaji wa filamu, kuanzisha shule maalumu ya kukuza vipaji vya wanamichezo (sports Academy) wazo hilo litekelezwe.

Ameongeza kuwa tamasha la Bagamoyo liendelee kuzingatia masuala ya Muungano kwa kuhakikisha vikundi vingine zaidi kutoka Zanzibar na sehemu zote za Tanzania Bara vinapata nafasi katika tamasha na kwamba maagizo hayo yakitekelezwa wizara itapiga hatua kubwa.


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema kazi ya wizara hiyo ni kuwaletea furaha na faraja watanzania pamoja na kubuni mambo mbalimbali ambayo yataleta furaha na amani katika nchi.

Waziri Mchengerwa amesema tamasha la Bangamoyo limeendelea kuboreshwa na kuwa tamasha la kimataifa ambalo litakuwa na washiriki wengi kutoka nje ya nchi ambapo mwaka huu vipo vikundi kutoka Canada, Zambia, Burundi na Visiwa vya Mayote kutoka nchini Ufaransa. 

“Malengo yetu katika tamasha hili na lile la Sauti za Busara kutoka Zanzibar ni kuyaendeleza matamasha haya ili kuyafanya kuwa ya kimataifa, tumeshapokea maelekezo kutoka kwa Rais ili kushirikiana nao pamoja.

"Pia kuhakikisha tamasha la Bagamoyo pamoja na Tamasha la Sauti za Busara la Zanzibar yanaendelezwa kuwa na taswira ya kimataifa katika siku za usoni hatua itakayosaidia kulitangaza taifa  ndani na nje ya nchi kimataifa” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amemweleza Makamu wa Rais kuwa Wizara hiyo imeanza kutelekeza programu ya mtaa kwa mtaa nchi nzima ili kusaka vijana wenye vipaji katika sekta ya Sanaa na Michezo ili kuvikuza na kuviendeleza na kuwa taifa la watu wenye furaha na amani kupitia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

No comments