HEADER AD

HEADER AD

GACHUMA : WAMENICHAGUA KWA SABABU WANA IMANI NA MIMI


Na Jovina Massano, Musoma.

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) akitokea Mkoa wa Mara, Christopher Gachuma amesema wapiga kura wana imani na uongozi wake kwakuwa ni mchapakazi katika Chama na amekuwa akijituma muda wote kukitumikia ndio sababu wamemchagua.

Akizumgumza na Mwandishi wa DIMA ONLINE Gachuma amesema wenye maamuzi ya kumchagua kiongozi ni wapiga kura wakikukubali watakuchagua utashinda na wakikukataa hawatakupigia kura .

"Nawashukuru wapiga kura kwa kuniamini na kunichagua ,nitaendelea kukitumikia Chama na kufanya kazi kwa bidii, nitaongeza idadi ya wanachama ambao watakuwa tayari kukipigania chama" amesema Gachuma.

Amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kina hitaji viongozi ambao wanawajibika na kukipenda Chama kwa dhati, kukitumikia kwa hali na mali na waliotayali kufanya kazi kwa hali zote.


"CCM inahitaji viongozi wawajibikaji, wazalendo, waadilifu, waminifu na wanaokitumikia kwa kukifanyia kazi kwa bidii wakati wote na kujitoa kwa moyo na hakina ubaguzi" amesema.

Gachuma amesema atashirikiana na wagombea wenza katika kukijenga chama na ameahidi kuacha alama katika mkoa huo kwa kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano hapo baadae.

Je Gachuma atagombea tena nafasi hiyo ya uongozi uchaguzi ujao wa 2027 ? naye amesema; " Mungu ndie anae panga akisema uongoze utaongoza akisema hauongozi huwezi kuongoza, kwahiyo siwezi kusema nitagombea au sitagombea kwa sababu kila jambo linapangwa na Mungu "amesema.

Baadhi ya wapiga kura wamesema Gachuma anatosha katika nafasi hiyo ndio sababu wamemchagua kwakuwa amekuwa ni mwajibikaji mzuri huku wakimuomba kuendelea kuitendea haki nafasi aliyopewa kuhakikisha anakipambania Chama pamoja na maendeleo katika mkoa wa Mara.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi  Kata ya Itiryo wilayani Tarime Gibuka Matala amewaomba viongozi waliochaguliwa kuzitendea haki nafasi zao na wawajibike kwakuwa wameaminiwa na wanachama.


"Sifa ya mgombea ni kuwa mwanachama hai, mwajibikaji katika chama ndio maana Mwenyekiti wetu ambae ndie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu ameweza kutenda haki kwa kuchagua wagombea sahihi, kwani wote wanawajibika kikamilifu katika kukijenga Chama.

" Lakini pia wagombea wameonesha nia ya kuleta mabadiliko katika mkoa wetu na hii itatimiza dhana ya kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo. Waliochaguliwa waelewe kuwa dhamana tuliyowapa ni kubwa waitendee haki walete mabadiliko ya kimaendeleo katika mkoa wetu", amesema Gibuka.

Mwanachama wa Chama hicho Joyce Sokombi amempongeza Christopher Gachuma kwa kuaminiwa tena kwa kupata kura nyingi kutoka kwa wajumbe kwani hiyo inaonesha kuwa amekuwa ni mwajibikaji katika Chama na kwa wanachama ndio maana amepata ridhaa hiyo.

"Hakuna asiyejua uwajibikaji na uadilifu wa Gachuma katika Chama walio nje ya chama wanaweza walisijue hilo ila sisi tulio kwenye chama ndio tunajua umuhimu wake kwenye chama, anafanya kazi kwa bidii, hata baadhi ya wagombea wamepita mikononi mwake kawakuza kisiasa.

"Pia nawapongeza wajumbe kwa kufanya maamuzi na hatimaye mshindi kapatikana, hata waliopungukiwa kura wasijisikie vibaya kwani ni mwanzo mzuri wa mafanikio yao hapo baadae subira yavuta heri hiyo ndio demokrasia na kukomaa kisiasa" amesema Sokombi.

Novemba 21,2022 Chama hicho kilifanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi nafasi mbalimbali kimkoa ambapo Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo aliyetoka Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dodoma, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga alimtangaza Gachuma kuwa mshindi kwa kuwashinda wagombea wenzake.


Christopher Gachuma aliibuka kidedea kwa kura 754, Ramadhani Marwa kura 279, Christopher Kangoye kura 21 na Daines Shindika kura 12, kura zilizopigwa na  wajumbe 1066 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mara.

Rejea uchaguzi

Baada ya kushinda uchaguzi huo Gachuma hadi kufika 2027 atakuwa ameongoza nafasi hiyo ya ujumbe NEC kwa vipindi 7 mfululizo vya uchaguzi katika Chama hicho tangu mwaka 1992 hadi sasa ataendelea na nafasi hiyo atakayoiongoza hadi 2027 utakapofanyika uchaguzi mwingine.

Ameongoza nafasi hiyo 1992-1997, 1997-2002, 2002-2007, 2007-2012, 2012-2017, 2017-2022 na sasa ataongoza tena kwa mwaka 2022 hadi 2027, na atakuwa ameongoza katika nafasi hiyo kwa miaka 35 mfululizo.






No comments