KAYA SABA ZAKOSA MAKAZI BAADA YA UPEPO KUEZUA NYUMBA
Na Dinna Maningo, Musoma
KAYA saba zenye wananchi zaidi ya 20 wakiwemo walimu katika Kijiji cha Bujaga kata ya Bulinga wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara, wamehifadhiwa katika nyumba za majirani baada ya upepo mkali kuezua mabati nyumba sita wanazoishi ulioambatana na mvua kubwa .
Bwire Msese mkazi wa Kitongoji cha Kulugongo Kijiji cha Bujaga amesema Novemba, 23, 2022 majira ya saa 12 jioni upepo ulivuma kwa kasi ulioambatana na mvua kubwa na kuezua nyumba yake moja na vitu vyote kulowana.
"Kila kitu kimeharibika, magodoro yakalowana na unga ukalowa tukalala njaa, nina mke na watoto watano na mjukuu mmoja jirani yangu Masingili Chambui katupatia hifadhi ya chumba kimoja mimi na familia yangu, namshukuru kwa huruma zake.
"Tunaomba Serikali na watu wengine wenye uwezo watusaidie kutuezekea nyumba wenye unga watusaidie, mimi ni mkulima nina umri wa miaka 54 maisha yangu ni ya kubangaiza" amesema Bwire.
Fedson Bezareli shuhuda wa tukio mkazi wa Kijiji hicho amesema " Upepo ulikuwa mkali baada ya mvua kuisha tulizunguka hapa senta kuona madhara ndipo tukaona nyumba za watu zikiwa zimeezuliwa , mvua iliwanyeshea na vitu vyote vikalowana ilibidi tuwasaidie kusomba vyombo tukawapeleka kupata hifadhi ya muda kwa wasamalia wema .
"Ni hifadhi ya muda wanahitaji kusaidiwa kwakuwa ni tukio la dharura hawana uwezo wa kuezeka nyumba kwa haraka tunamuomba Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu kutokana na mazingira ya hapa kijijini atusaidie nyumba ziezekwe "amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kulugongo katika Kijiji hicho Moshi Tasinga amesema hali hiyo itawaingiza gharama kwakuwa baadhi maisha yao ni ya hali ya chini.
"Nyumba zimeezuliwa ikiwemo nyumba moja waliyokuwa wamepanga walimu wawili wa shule ya Sekondari Bulinga ambao wamepewa hifadhi kwenye nyumba anayoishi mwenye nyumba wao kila mtu chumba kimoja, mazao hayajaharibika isipokuwa mti mmoja ndio umeangushwa na upepo, vitu vililowana hadi unga wa kupikia.
Mti ulioangushwa na upepo
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bujaga Jumapili Mtwale amesema jumla ya Kaya Saba zenye watu 23 katika Kitongoji cha Kulugongo na Bujaga zimekosa mahali pa kuishi baada ya nyumba kuezuliwa na upepo ambao kwa sasa wamepewa hifadhi ya muda kwa majirani.
Post a Comment