SERIKALI YATENGA BILIONI 10.7 KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Na Mwandishi wetu , Dodoma
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali imetenga Tsh Bilioni 10.7 kwa ajili ya kutekeleza mpango mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Mollel amesema hayo Novemba, 2,2022, wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Mtoni Idrissa Juma katika kikao cha pili cha Bunge la 9, Jijini Dodoma.
Amesema mpango mkakati huo, umeainisha mikakati mahsusi ya udhibiti wa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo, Kuimarisha uratibu na ushirikishwaji wa sekta mtambuka, kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma.
Amesema kuwa mipango mingine ni pamoja na kuimarisha uwezo watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti pamoja na kuhamasisha wananchi kuhusu njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na kujenga tabia ya kufanya mazoezi.
Dkt. Mollel amesema Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya afya kwa wote pindi sheria hiyo itakapopitishwa na bunge ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi, hasa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Mollel ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu ametenga kiasi cha Tsh Bilioni 149.77 kwaajili ya kuwapatia Bima wananchi wasio na uwezo.
Post a Comment