HEADER AD

HEADER AD

KANISA LA SDA LIMESEMA LINA IMANI NA RAIS SAMIA


Na Dinna Maningo, Dodoma

KANISA la Waadventista wa Sabato (SDA) nchini Tanzania limesema lina imani na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwakuwa ni mwenye upendo na mapenzi makubwa aliyonayo kwa watanzania na kwamba litaendelea kumuombea.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Kanisa la Waadventista Wasabato Mch. Jeremiah Izungu wakati akisoma Taarifa ya Kanisa hilo, katika Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kati mwa Tanzania, yaliyofanyika katika makao yake makuu Jijini Dodoma, Novemba, 19, 2022.

Mch.Jeremiah amesema Rais Samia anaongoza vyema katika nyanja mbalimbali kwani katika uongozi wake miradi inajengwa ukiwemo ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, huduma ya maji ambapo pia amesema kanisa linatoa shukrani za dhati kwa kazi inayofanywa na mhimili wa bunge na mahakama.


"Kanisa la Waadventista wa Sabato tunakupongeza kwa moyo wa dhati kwa namna ambavyo unatuongoza vyema, tumeshuhudia moyo wako wa upendo na mapenzi makubwa uliyonayo kwa watanzania katika kila nyanja.

"Kuhusu elimu madarasa yamejengwa kwa wingi hii imewapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia ujenzi wa madarasa, kwenye afya vituo vya afya na hospitali vimejengwa kwa wingi na tiba imeboreka kwa upatikanaji wa vifaa tiba na madawa.

"Huduma ya maji kweli umewatua wakina mama ndoo kichwani, kwa upande wa miundombinu tunajionea miradi inayoendelea kuimalishwa katika nchi hii, sisi kanisa tuna imani na wewe na jukumu letu kubwa ni kuendelea kukuombea kwa mwenyezi Mungu aendelee kukupatia afya njema wewe na familia yako na viongozi wote wanaokusaidia kuongoza nchi yetu.

" Tunawaombea Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Kanisa linatoa shukrani za dhati kwa kazi nzuri kutokana na uongozi wako mahiri.

Mch. Jeremiah amesema changamoto zinazowakabili , Serikali anayoiongoza Rais Samia huzipatia ufumbuzi hivyo wao kama kanisa wanaahidi kushirikiana na serikali yake anayoiongoza na mwenyezi Mungu ambariki na kumpa afya njema amani, furaha na maisha marefu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Dkt. Mch. Godwin Lekundayo amemshukuru Rais Samia kwa moyo wa upendo na unyenyekevu aliouonesha kwa wananchi bila kujali itikadi za kidini.

Hivyo amemthibitishia kuwa, kanisa litaendelea kumwombea na kushirikiana na Serikali pamoja na kuiombea nchi iendelee kuwa na umoja na utulivu ambazo ni tunu kwa Taifa.


" Kwa niaba ya waumini wote wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania tunakushukuru sana Rais kwa kutupa kbali kuabudu pamoja nawe kiongozi wetu mkuu wa nchi kwa unyeyekevu mkubwa, wananchi wako tunafurahi mipango mizuri na maono uliyonayo katika kuiongoza nchi "amesema.

Rais Samia ameshukuru kanisa hilo kwa maombi yao ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa ajili ya serikali na Taifa kwa ujumla  nakwamba kupitia maombi ya viongozi wa dini Taifa linaendekea kudumu katika umoja, amani na mshikamano.

Hata hivyo Rais Samia amewaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kumwomba mwenyezi Mungu kuyanusuru madhara yatokanayo na uhalibifu wa mazingira na kushusha mvua, huku akiwasisitiza viongozi hao kutoa elimu kwa waumini ya utunzaji wa mazingira, upandaji wa miti pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.








No comments