HEADER AD

HEADER AD

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AKATISHA ZIARA YA UKAGUZI TARIME

>>>Ni baada ya kutoridhishwa na ujenzi
>>>Aagiza Desemba, 15 picha za ujenzi zimfikie
>>>Asema Desemba,19 atarudi Tarime


Na Dinna Maningo, Tarime

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde, ameacha kuendelea na ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara.

Silinde amefikia uamuzi huo baada ya kufika shule ya sekondari Nyamisangura na kukuta ujenzi wa madarasa ukiwa hatua ya Lenta jambo lililomkera kuendelea kukagua shule zingine  .

Baada ya Waziri Silinde kukagua shule hiyo alitakiwa kwenda kukagua ujenzi wa madarasa shule mpya ya sekondari Turwa B na shule ya sekondari Iganana lakini alikataa kwenda akisema hata kwenye hizo shule zingine anajua hali ni hiyo hiyo.

Silinde ameiagiza Halmashauri hiyo ifikapo Desemba, 15, 2022 kumpatia taarifa ya ujenzi wa madarasa ikionesha na picha za majengo yakiwa na madawati ndani yake huku akiahidi kurudi Tarime Desemba, 19, 2022.

            
         Naibu Waziri akikagua ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Nyamisangura

"Mnasema Tarehe 15 ujenzi utakuwa umekamilika! mna uhakika? kwingine huko ukiliangalia jengo unaona lipo kwenye hatua nzuri, yale ambayo yapo kwenye hatua za mwisho walishapiga plasta, wameshafunga Gypsum na ukamilishaji.

"Hata mtu akikwambia namalizia ndani ya wiki moja unaona kabisa inawezekana, sasa leo mtu anakwambia hapa wanapoweka lenta tarehe 10-15 patakuwa pamekamilika, sawa acha mimi nichukue hilo, lakini narudia tena mnanijua vizuri kwenye hili, sipendi kudanganywa, alafu sipendi mtu anaharibu kazi ya Mhe. Rais" amesema Silinde.

Ameongeza " Katika kitu ambacho tutagombana mapema sana na nitakuja kutolea mfano hapa hapa Tarime haya majengo yasipokamilika, hii nawahakikishia kwa asilimia 100, na niseme ukweli Mh. DC hawa wamekuangusha, wale wa Tarime Vijijini wamefanya vizuri"amesema Silinde.

Naibu Waziri huyo amesema ameshangazwa kuona Halmashauri ya Vijijini ujenzi wake ukiwa kwenye hatua nzuri ambako vifaa vingi wananunua kutokaTarime mjini lakini Halmashauri ya Mji ambayo vifaa vipo karibu ujenzi wake bado ni wa kusuasua.


       Naibu Waziri na DC Tarime wakiwa na bahasha mkononi yenye taarifa ya mradi wa ujenzi shule ya sekondari Nyamisangura.

"Kule Tarime Vijijini wamesema kila kitu wanatoa hapa mjini, simenti wananunua huku huku, mawe, nondo na vitu vingine wamesema wamenunua huku alafu nyinyi mmezubaa, mjini mnashindwa na kijijini! mmetuangusha" amesema Silinde.

Amesema atakaporudi tena Tarime atakagua madarasa yote na kuhusu shule atakazozitembelea hiyo ni siri yake kwasababu vyanzo vya kumpatia taarifa anavyo.

 " Kwa sababu hii hali ipo maeneo yenu madarasa mengi hayajakamilishwa, hata huko Turwa najua mko kwenye hali hii, Mkurugenzi tarehe 15, mwezi wa 12 nataka hiyo taarifa ikionesha picha za majengo yakiwa na madawati ndani yake.

" Narudia tena naongea kama natania tarehe 12, mwezi wa 12 taarifa hiyo mnapotuma Mkoani  na Ofisi ya Rais TAMISEMI ifike na inifikie, na tarehe 19 mwezi wa 12 nitakuwepo hapa nitapita Turwa B nitapita na maeneo mengine, nitachagua sampo mwenyewe shule nitakazozitembelea hamtanichagulia kwasababu nina vyanzo vya kupata taarifa.

Ameongeza " Nitakuja mwenyewe, nitamwambia Mh.DC nakuja taarifa kuhusu natembelea shule gani ataijua ofisini kwakwe siku hiyo, utani kwenye kazi sitaki tusiharibiane kazi, kila mmoja aheshimu kazi ya mwingine, najua mtafuatilia na hii kazi itakamilika" amesema.

           Naibu Waziri Silinde akizungumza 

Silinde amesema hana utani kwenye kazi huku akiuelekeza uongozi wa Wilaya na Mkoa kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa madarasa katika mkoa huo na kwamba ifikapo tarehe, 15 ,Desemba, 2022 madarasa yote yawe yamekamilia.

Amesema siku si nyingi wanafunzi watapangwa kwenye madarasa hayo hivyo ni vyema madarasa yote yakakamilika kwa wakati.

Akisoma Taarifa ya ujenzi wa shule, Mkuu wa shule ya sekondari  Nyamisangura Zakaria Kabengo amesema madarasa sita yanajengwa katika shule hiyo na madarasa matano katika shule mpya ya sekondari Turwa B yatakayogharimu Tsh. Milioni 220.

"Kiasi cha fedha Tsh. 220,000,000 kilipokelewa mnamo tarehe 1, Octoba, 2022, mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa sita shule ya Nyamisangura ulianza rasmi Octoba, 25, 2022, vyumba vitatu vipo hatua ya kuunda kenchi ili vipigwe bati na vitatu vingine vipo hatua ya lenta.

"Hadi sasa kiasi cha Tsh. 129,471,947 kimekwisha tumika kati ya fedha hizo 71,305,515 zimetumika ujenzi wa madarasa shule ya Nyamisangura na Tsh. 58,166, 432 Turwa B ujenzi utakao kamilika Desemba 15, 2022," amesema Zakaria.


Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele amesema sababu ya Halmashauri ya wilaya kuwa katika hatua nzuri ya ujenzi ni kutokana na wao kununua matofali kwa watu mbalimbali.

Amesema Halmashauri ya Mji wao walitegemea matofali kutoka kwenye kiwanda cha matofali cha Halmashauri kinachozalisha tofali za kujenga madarasa yote na hivyo kushindwa kumudu kwa muda unaotakiwa.

Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu imetoa fedha T.sh Milioni 820 katika Halmashauri ya Mji Tarime kujenga vyumba vya madarasa vipatavyo 41ambavyo ujenzi wake unaendelea.



            Baadhi ya madarasa

                      Madarasa


No comments