HEADER AD

HEADER AD

TURWA WAKUBALI BARABARA IJENGWE LAKINI KWA MASHARTI


>>>Ni barabara ya mtaa iliyogomewa kujengwa

>>>Wakasirika nyumba kubomolewa

>>>Wataka Serikali ifanye mapatano


Na Dinna Maningo, Tarime

WANANCHI wa Kata ya Turwa Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, wamekubali barabara ijengwe ambayo ujenzi umesimama baada ya kugomewa na baadhi ya wananchi waliobomolewa nyumba zao na mazao kufekwa.

Nyumba hizo zinadaiwa kubomolewa na Halmashauri ya Mji Tarime ili kupitisha barabara kitendo ambacho kimepingwa vikali kwenye mkutano mkuu wa wananchi .

Wanachi wamesema barabara ijengwe lakini Viongozi wa Kata hususani Diwani na Halmashauri ya Mji Tarime wahakikishe wanakaa na wananchi waliobomolewa nyumba na kuondolewa kwenye maeneo waliyokuwa wakiishi na mazao yao  kufekwa kuwasikiliza malalamiko yao na kuyafanyia maamuzi sahihi ili pande zote ziridhike.

Wananchi wamesema maamuzi yaliyofanyika ya kupitisha barabara na nyumba za watu kubomolewa na mazao kufekwa hayakufuata taratibu zikiwemo za kuwshirikisha wananchi kupitia mkutano mkuu wa wananchi.

Mkutano wa Kata ya Turwa uliitishwa na Diwani wa Kata hiyo Chacha Machugu ulihohudhuliwa na Viongozi Ngazi ya Kata akiwemo Mtendaji wa Kata Boniphace Mzurikwao,Wenyeviti  wa Mitaa na Wajumbe wa Serikali za Mitaa.

Mkutano uliohusu kusikiliza maamuzi ya wananchi kama wanakubali au kukataa ujenzi wa barabara baada ya TARURA kusimamisha ujenzi kutokana na kutokuwepo makubaliano ya wananchi ili kupitisha barabara ambayo ikilimwa itapita kwenye maeneo ya watu.
Diwani Chacha Machugu akizungumza mbele ya wananchi amesema maeneo ambayo baadhi ya wananchi waliishi na kujenga nyumba, kupanda mazao ni maeneo ya serikali ambayo awali yalikuwa ya kijiji ambayo kwa sasa ni Mtaa wa Kebikiri, Kokehogoma na Uwanja wa Ndege.

Diwani amesema siyo yeye aliyetoa kibali cha kubomoa nyumba ya mtu yeyote isipokuwa Halmashauri ya Mji Tarime ndiyo iliyombomoa kwa sababu ya watu hao kujenga bila kuwa na kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri.

"Nawashukuru kwa kuitikia mkutano lengo la mkutano wenu tunataka kusikia kutoka kwenu je mko tayari barabara ijengwe au hamko tayari? maendeleo yanapokuja yanaleta faida na hasara wapo watakaoumia na ambao hawataumia, kazi yangu ni kusimamia maendeleo kuhakikisha wananchi wangu wanapata maendeleo.

"Kusimamia vipaumbele vilivyopitishwa na wananchi, kuhakikisha serikali inatoa fedha za miradi ya maendeleo, Serikali imetoa zaidi ya Milioni 5 kujenga barabara ambayo inaunganisha mitaa mitatu itakayohudumia wananchi, lakini greda lilipokuja ili kulima barabara baadhi ya wanachi wakazuia.

" Wakafungua kesi mahakama ya Ardhi TARURA ikasimamisha ujenzi mpaka kwanza mkutano ukae kama wananchi watakubali ijengwe ndio ujenzi uendelee, mkikataa tutakosa barabara na fedha hii itaenda kufanya kazi maeneo mengine naomba nisikilize maoni yenu mpo tayali barabara ijengwe au hampo tayali ?" amesema Diwani.

Wananchi wakatoa ya moyoni yao huku wengi wao wakiilaumu Serikali kwa kitendo cha kuharibu mazao na kubomoa nyumba za watu hili hali viongozi wa serikali ndiyo walitwaa sehemu ya eneo la Kijiji na kuwauzia wanachi waliyoyanunua kwa fedha lakini imewageuka na kuwaondoa kwenye maeno waliyouziwa kihalali na viongozi.


Tumaini Abel mkazi wa Mtaa wa Kebikiri amesema maendeleo yanapokuja ni faida ya wananchi lakini huwa yanashirikisha wananchi na maendeleo hayahitaji kelele na kilichosababisha kelele ni baada ya wananchi kuona katapila likilima barabara bila wao kushirikishwa.

"Mimi nimebomolewa nyumba yangu niliyoijenga tangu mwaka 2000 nilijibana kwa kudunduliza fedha lakini nyumba yangu imebomolewa kwenye uongozi wa huyu Diwani bila hata kuambiwa njoo uchukue mabati yako, Meneja wa TARURA alikataa kwa sababu eneo lina mgogoro.

"Nilipiga simu kwa Mwenyekiti wangu wa Mtaa kuuliza kama yeye ndiye karuhusu nyumba yangu ibomolewe na mazao yafekwe wakati hajanipa tarifa ya mimi kubomoa nyumba na kuondoa mali zetu akasema yeye hana hizo taarifa za kubomoa nyumba, lakini watu walijibebea madaraka wakabomoa.

" Tulienda Polisi kutoa taarifa wakasema tuletee barua nikaenda kwa Mwenyekiti wa Mtaa aniandikie barua akakataa, hata mimi nataka maendeleo lakini ni maendeleo gani ambayo hayafuati utaratibu haya sio maendeleo ni kuathiri watu," anasema Tumaini.

Ameongeza"Kama nyumba yangu ilijengwa kimakosa Diwani alipaswa kunishirikisha ili nitoe mwenyewe mali zangu, tulinunua haya maeneo kutoka kwa watu ambao waliyamiliki tangu mwaka 1980 na uongozi wa serikali ulikuwepo wakasema maeneo ni ya wananchi na unapouziwa eneo Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wake ni mashahidi ndiyo wanaokuandikia barua alafu wananibomolea nyumba," amesema Tumaini.

Yohana Nyeika amesema" Tuliwahi kukaa mkutano hapahapa kwenye hili eneo la Rikorong'era hivi kile kikao kiliamua nini? tusomewe muhtasari uliopita" anasema .


Karebu Mwita amesema" Hili eneo limetengwa kujenga shule na tayali ujenzi umeanza na barabara lazima iwepo, sasa kama eneo ni la shule mnataka tena kibali cha kujenga barabara? hii inaonesha kuwa nyie viongozi hamkuwa mmejipanga.

"Ila mmetuita ili tuonekane kwenye mhitasari wa mahudhulio kuwa wanachi tumekubali barabara ipite, sasa tufafanulieni shida ni nini, madarasa yameshajengwa, eneo mnasema ni la shule sasa tunajadili barabara ili iweje badala ilimwe?" alihoji.

Marwa Munge Balozi Mtaa wa Uwanja wa Ndege shina namba 4 amesema" Trekta iliyokuja hapa siyo ya Diwani hii baraba mpaka kulimwa Wenyeviti wanajua, mimi kuna shamba langu barabara imepanuliwa.

" Eneo langu likachukuliwa kupitisha barabara mazao yakaharibiwa nilikubali kutoa eneo maana ni faida tutaitumia kupeleka wagonjwa hospitali, shule ikijengwa watoto watapita lakini hapa ni migogoro"amesema.



Charles John Mkazi wa Mtaa wa Uwanja wa Ndege amesema" Hata kwangu wamepitisha barabara sijapinga na barabara hiyo sitapita mwenyewe watapita watu wengi na nisingekubali barabara ipite kwenye eneo langu haohao wananchi wangelalamika kuwa nimekataa barabara isipite!".

"Barabara ikipita huwa kuna makubaliano pale inakopita barabara wananchi wa upande wa kulia wanatoa hatua kadhaa na wa upande wa kushoto wanatoa hatua kadhaa barabara inalimwa hii barabara ilikuwa haina kipimo ndio maana haijalimwa" amesema.

Nyamahende Cleophace amesema" Barabara inajengwa na Wataalam sasa kama barabara inapita mtaani na wananchi hawakushirikishwa basi wasikilizwe ili kuondoa malalamiko tutumie haki katika kutafuta maendeleo" amesema.

Baadhi ya wananchi wameshauri maendeleo yafanywe kwenye eneo lisilo na mgogoro lakini lile lenye mgogoro liachwe kwanza kwakuwa kesi tayali imeshafunguliwa mahakamani.

Miongoni mwao wamesema barabara isilimwe hadi hapo mahakama itakapotoa maamuzi juu ya watu waliofungua kesi kulalamika kuondolewa kwenye maeneo yao, kubomolewa nyumba na mazao kuharibiwa.

Charle Chacha amesema" Hili eneo tunalopigania lilikuwa eneo la baba yangu, serikali haijui majukumu yake, wakati inatenga maeneo ingeweka bikoni kwenye maeneo yake lakini kutokana na udhaifu wa viongozi wake hao hao wakahujumu ardhi hii.


"Wale viongozi wakachukua wapambe wakawagawia maeneo nao wakayauza kwa watu, mtu anajenga nyumba kwasababu ya udhaifu wa Serikali alafu leo unambomolea nyumba!, je anaenda wapi? ushauri wangu maendeleo yafanywe kwenye eneo ambalo halina mgogoro kunakojengwa shule eneo lenye mgogoro liachwe kwakuwa kesi ipo mahakamani"amesema.

Zephania Mwita mkazi wa Mtaa wa Kokehogoma amesema" sisi ni wageni hatukujua kama eneo lilikuwa la serikali na tuliuziwa na haohao viongozi wa serikali ambao walitambua kuwa maeneo wanayotuuzia ni ya serikali.Kwakuwa barabara imepita eneolenye mgogoro basi Serikali iangalie na kuwalipa wape fidia au iwape eneo lingine wajenge.

" Jamani ujenzi ni mgumu hali yenyewe ya sasa ni ngumu, jambo likiwa halijakupata utaona ni sahihi lakini likupate ndio utaona maumivu yake , Viongozi tumieni busara kutatua changamoto" amesema Zephania.

Kioma Mwita mkazi wa Mtaa wa Rebu yeye amesema katika vikao vilivyopita wananchi walipendekeza shule ijengwe kwenye eneo hilo na wanachi waliojenga nyumba wafidiwe kwakuwa makosa ni ya serikali baada ya viongozi wake kuwauzia waanchi ardhi ya Kijiji.

Kioma amesema Halmashauri imekosea kubomoa nyumba za watu kwakuwa mwenye kuruhusu nyumba ibomolewe au mazao yaondolewe ni kibali cha Mahakama pekee na si kiongozi kujiamlia kupitia madaraka yake huku akisisitia eneo lenye mgogoro liachwe kwakuwa kesi tayali ipo Mahakama ya Ardhi.


"Kuna Mkutano tulikaa wananchi na Diwani tukakubaliana shule ijengwe na wale ambao walijenga kwenye maeneo kwakuwa walipewa kinyume wafidiwe sasa kwanini wabomolewe nyumba bila kulipwa fidia?, viongozi mnakiuka makubaliano yaliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa wananchi" amesema Kioma.

Ameongeza " Hili eneo kabla hatujawa Mitaa lilikuwa ni eneo la Serikali ya Kijiji lilikuwa na Ekali 70 maeno yakauzwa leo ndio mnadai haka kakipande kamwananchi mmoja na isitoshe mwenye kibali cha kubomoa nyumba ya mtu ni Mahakama siyo Diwani wala Halmashauri wala nani" amesema Kioma.

Antony Wambura yeye amesema" Mnasema ardhi ni ya serikali lakini mjue serikali haiwezi kutawala ardhi bila wananchi, viongozi waishapewa madaraka wanayatumia vibaya, mimi na uzee wangu nimeshindwa kujenga nyumba huyu kijana kajibana kajenga kajumba kake alafu anabomolewa.

" Hivi haya yanayofanyika serikali kuu inayajua ? Rais mama Samia anajua? huyu Diwani nilimpigania, mimi nimetembea mikoa mingi ila sijaona haya yanayofanyika Tarime mwananchi anajenga nyumba alafu anabomolewa bila taratibu za kisheria kweli?" Alihoji.

Diwani amesema yupo tayari kufa

Diwani Chacha Machugu ameweka  msimamo wake kwamba eneo walilokuwa wakiishi wananchi hao ni la serikali ambalo awali lilikuwa shamba la Kijiji na baadae kuwa chini ya Halmashauri ya Mji Tarime lakini liliuzwa kinyume na viongozi wasio waadilifu.


"Serikali yetu imetupatia Tsh Milioni 200 kujenga Madarasa 10 shule mpya ya Sekondari na TARURA imetoa Tsh zaidi ya Milioni 5 kujenga hii barabara , wale watu wamejenga bila kufuata utaratibu wa ujenzi na mgogoro wa ardhi upo mahakamani na kesi ikiwa mahakamani haijadiliwi ,sisi tujikite kwenye barabara.

"Zipo nyumba zilibomolewa ikajengwa barabara ya Lami na shule zikajengwa ,shule inayojengwa siyo yangu, barabara siyo yangu ni ya wanachi, nyie mmenituma kusimamia maendeleo, mimi sijengi shule wanaojenga ni serikali  na nguvu za wananchi.

Ameongeza " Mimi mkisema barabara isilimwe hamtaona greda hadi miaka yangu mitano ya uongozi inaisha, mimi ni Diwani mwenye mitaa 8, mimi naishi mtaa wa Mkuyuni siishi kweye eneo hili inakopita barabara, nipo tayari kufa mnizike lakini Kata ya Turwa ipate maendeleo, Kata ya Turwa imekuwa ya kisiasa.


" Kama mmeona mimi siwezi kazi nipo tayali kuacha kazi, kuongoza wananchi ni kazi, unakuta wengine wanataka hiki wengine hawataki, nasema hivi shule hii lazima ijengwe tupende tusipende na Barabara italimwa, hii ni faida kwetu na watoto wetu, hii barabara kila mtu atapita na tayali imetolewa fedha ya barabara"amesema.

Diwani akiwa anahitimisha mkutano akawauliza wananchi kama wamekubali barabara ijengwe au hawataki ijengwe.

Diwani akauliza : Wananchi mnakubali barabara ijengwe au isijengwe?

Wananchi wakapaza sauti zao nakusema : Barabara Ijengweeeee.

Diwani: Barabara ijengwe au isijengwe?

Wananchi : Barabara ijengweeeeee, kisha Diwani akafunga mkutano na Wananchi wakatawanyika.

No comments