RAIS SAMIA AOMBWA KUINGILIA KATI MGOGORO WA WANANCHI NA BARRICK
>>>Wadai Serikali iliwaondoa kwa nguvu
>>>Wamwangukia Rais Samia
Na Daniel Limbe, Kahama
BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Kakola wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wamemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 20 kati yao na mgodi wa Barrick Gold Corporation.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, kuwataka walalamikaji wa fidia kwenye mgodi wa North Mara kujitokeza wakiwa na nyaraka sahihi ili kuhakikiwa wanao stahili waweze kulipwa.
Kutokana na kauli hiyo, imewaibua baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kakola kumwomba Rais Samia kuwasaidia kupata fidia ya maeneo yao ambayo awali waliyamiliki na kuyaendeleza kabla ya ujio wa kampuni ya madini ya Bulyanhuru Gold Mine, Acacia na hatimaye Barrick.
Emmanuel Bombeda miongoni mwa wachimbaji wa madini anayedai fidia, amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kutafuta haki yao kwa zaidi ya miaka 20 pasipo mafanikio huku baadhi yao wameshafariki dunia wakiwa hawajapewa stahiki zao.
"Kitendo cha serikali kutuondoa kwa nguvu kwenye maeneo yetu kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kisha ardhi yetu kuendelezwa na mgodi wa Barrick kwa shughuli za uchimbaji pasipo kutulipa fidia kumesababisha wananchi 363 kuwa maskini wa kutupwa na hata wengine wamekufa pasipo kupata hata jasho lao" amesema Emmanuel
Idadi hiyo inahusisha makundi ya aina tatu wakiwemo,wamiliki wa mashamba,wachimbaji wadogo na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo walioumia wakiwa kazini na kuachishwa kazi mwaka 2007 kwa nyakati tofauti pasipo kupewa stahiki zao.
George Kingi, ambaye ni miongoni mwa wadai wa fidia, amesema kabla ya kuondolewa, maeneo hayo yalikuwa na nyumba za kuishi, mazao na mashimo ya wachimbaji wadogo ambao pia waliondolewa kwa amri ya serikali mwaka 1996.
"Tumemwona rais wetu alivyo mpenda haki na mwenye huruma na watanzania, juzi ametangaza kuwalipa mafao yatokanayo na michango ya mifuko ya jamii watumishi wa vyeti feki ambao ilikuwa ni haki yao, tunaamini hata sisi mgogoro huu ukimfikia ataguswa na kuhakikisha nasi tunapewa haki yetu ambayo imeminywa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi.
"Kwa kipindi chote hicho tumefuatilia haki zetu ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuonana na rais watatu waliopita pasipo mafanikio, kwa hivyo tunaamini nafasi yetu ya mwisho ipo mikononi mwa rais Samia iwapo ujumbe wetu utamfikia" amesema George.
Ameongeza " Licha ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala, Bhikhu Mohamed, kuwasilisha hoja ya mgogoro huo kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania julai 26 mwaka 1996 bado wananchi hao hawakulipwa(Nakala ya hotuba hiyo tunayo)" amesema.
Afisa uhusiano wa mgodi wa Barrick, Agapiti Kisoka, amesema ana muda mfupi tangu amekuwa kwenye ofisi hiyo hivyo baadhi ya madai ya wananchi hayajui huku akidai anachoelewa ni kwamba mgodi unapotaka kuongeza eneo hufanya makubaliano na wananchi kwaajili ya kuwalipa fidia.
Afisa Madini wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Hango, amethibitisha kuwepo kwa malalamiko yanayohusu fidia za wananchi na kusema kwamba suala hilo bado linaendelea kushughulikiwa na mamlaka za serikali.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Festo Kiswaga, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia malalamiko hayo na hatua iliyofikiwa kwaajili ya fidia, simu yake haikupokelewa, DIMA Online Inaendelea kumtafuta mkuu wa wilaya hiyo kuzungumzia mgogoro huo.
NUKUU:
>>>Ibara ya 255 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 inasema; Ni ukweli usio na shaka kuwa, ili CCM iendelee kukubalika na kuaminiwa na wananchi na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi, upo umuhimu mkubwa kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi, kuwa karibu na wananchi kwa kuwatembelea, kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika kuzipatia majawabu.
>>> Ni muhimu pia kwa CCM wakati wote kuwa kimbilio, msemaji na mtetezi wa wananchi wote na hasa wanyonge.
>>> Hii ni muhimu kwakuwa, asili yake, CCM ni Chama cha wakulima na wafanyakazi kinachowatetea wale ambao sauti zao si rahisi kusikika.
Post a Comment